0digg Leon BahatiRAIS Jakaya Kikwete ameinadi kwa wawekezaji Mikoa ya Rukwa, Kigoma na Katavi akiwahakikishia kuwa Serikali iko mbioni kukamilisha miundombinu muhimu ya mawasiliano ikiwamo barabara na umeme.Alisema hayo jana katika mkutano wa wawekezaji uliofanyika wilayani Mpanda na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta hiyo pamoja na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini. Rais Kikwete aliwaonya Watanzania wasipuuzie mikakati ya kuwakaribisha wawekezaji hasa wa nje ya nchi akisema bila ya kufanya hivyo, nchi haiwezi kuwa na maendeleo. “Maendeleo ni uwekezaji… uwekezaji ni chachu ya maendeleo. Ule mtindo wa kuiachia Serikali ifanye shughuli zote za uchumi, umepitwa na wakati,” alionya Rais Kikwete katika mkutano huo ambao ulionyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa, TBC1. Aliwahakikishia wawekezaji wa viwanda kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kuwa Serikali iko mbioni kukamilisha uboreshaji wa miundombinu kama vile ya barabara, usafiri wa majini, viwanja vya ndege na upatikanaji wa nishati ya umeme ya Gridi ya Taifa. Rais Kikwete alitaja baadhi ya faida anazoweza kupata mwekezaji katika mikoa hiyo kuwa ni pamoja na uhakika wa soko la ndani, masoko kwa nchi jirani za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Burundi. Alisema rasilimali ya mikoa hiyo mitatu, ukiwapo mpya wa Katavi ambao mchakato wa kuuanzisha uko ukingoni, ina rasilimali zinazofanana hivyo akawaalika wawekezaji kuitembelea na kuitathmini. Alisema mikoa hiyo ya pembezoni, ambayo imekuwa nyuma kimaendeleo kutokana na mawasiliano mabaya ya barabara, sasa inatarajiwa kuwa na bandari nzuri katika Maziwa ya Nyasa, Tanganyika. Rais alitaja fursa nyingine za uwekezaji kuwa ni usafiri wa uhakika wa meli na viwanja vya ndege. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Mary Nagu aliwakaribisha wawekezaji kutembelea mikoa hiyo na kushuhudia ilivyo na rasilimali nyingi. Alisema kuwa bila ya wawekezaji wenye uwezo wa kifedha, wakazi wa mikoa hiyo hawataweza kufaidi rasilimali zinazowazunguka. |
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa