Patricia Kimelemeta
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jana liliwapeleka polisi, maharamia saba wenye asili ya Kisomali waliotaka kuiteka meli ya Sam S Allgood iliyokuwa ikifanya utafiti wa mafuta katika Kisiwa cha Mafia, kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Juzi, maharamia hao walifikishwa katika Kikosi cha Maji (Navy) kwa ajili ya maandalizi ya kukabidhiwa kwa polisi.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Kapambala Mgawe alisema maharamia hao walikabidhiwa mikononi mwa polisi juzi jioni ili waweze kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria.
“Tumewapeleka polisi ili waweze kuwahoji, na kuwachukulia hatua zaidi za kisheria, kwa sababu sisi upelelezi wetu umekamilika, bado upande wao ili na wenyewe waweze kujiridhisha,” alifafanua Mgawe.
Alisema kutokana na hali hiyo, jeshi hilo linaendelea kusimamia ulinzi na usalama wa nchi, na kutaka wananchi wasiwe na hofu juu ya tukio hilo na kusisitiza kwamba, JWTZ iko makini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kamishna, Robert Manumba alikiri kupokea maharamia hao na sasa wanaendelea kuwachunguza ili waweze kubaini chanzo cha utekaji huo kabla ya hatua za kisheria.
“Ni kweli jana (juzi), tuliwapokea maharamia saba waliokuwa wanashirikiwa na Jeshi la Wananchi, lakini bado tunaendelea na uchunguzi wa kisayansi ili tuweze kubaini kiundani zaidi,” alisema DCI Manumba.
Aliongeza kwamba, ni vigumu kuwafikisha mahakamani kwa sasa kwani ni mapema mno kutokana na maofisa wa jeshi hilo kuendelea na uchunguzi wao, utakaowapa taarifa nyingine muhimu.
DCI Manumba alisema kutokana na hali hiyo wataendelea kuwahoji ili waweze kupata taarifa nyingi zaidi ambazo zitawasaidia katika kazi zao, pamoja na kuwatambua mahali walipotoka.
“Wanaonekana wana asili ya kisomali, lakini hatuwezi kuwaamini kama wametoka Huko bila ya kufanya nao mahojiano ya muda mrefu, kwa sababu Raia wa Somalia, Ethiopia, Sudan wanafanana, kutokana na hali hiyo tutaendelea kuwahoji,” aliongeza.
Alisema kutokana na hali hiyo, wanatumia mbinu mbalimbali ikiwamo ya kisayansi ili waweze kuwabaini kwa undani zaidi na ikiwa watakamilisha zoezi hilo watatoa taarifa kwa wananchi juu ya hatua stahiki zitakazochukuliwa dhidi ya maharamia hao.
Tukio la kukamatwa kwa maharamia hao lilitokea Oktoba 3 mwaka huu, ambapo maharamia hao walifanya tukio hilo umbali wa kilomita 40 Kaskazini Mashariki mwa Kisiwa cha Mafia Mkoa wa Pwani.
Hata hivyo, JWTZ, iliripoti kuwakamata maharamia saba waliotaka kuteka meli iliyokuwa ikifanya utafiti wa mafuta ambapo meli mbili zilizokuwa zinatumiwa na askari wa JWTZ za Froshibre na Monck ziliwasili katika eneo hilo na kuwasha taa, huku wakiwaona maharamia hao wakiwa nje ya meli wanatembea.
Maharamia hao walianza kurusha risasi hewani jambo ambalo lilisababisha wanajeshi hao kujibu mapigo, baada ya kuona wamezidiwa wakaamua kutupa silaha zao na kujisalimisha. |
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa