Translate in your language

Saturday, July 16, 2011

Wabunge wamkaanga Waziri Ngeleja





Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akiwa amejishika kichwa wakati Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2011/2012, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
WABUNGE jana walimweka kitimoto Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja baadhi yao wakimtuhumu kwa kudanganya kwenye bajeti yake na kurundika miradi ya umeme jimboni kwake (Sengerema) na kwa maswahiba wake ambao pia ni mawaziri.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Bungeni jana, wabunge hao walisema bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2011/12, ni mbaya na mbovu isiyofaa hata kupitishwa.

Wakichangia makadirio ya matumizi ya wizara yaliyowasilishwa Bungeni jana asubuhi na Waziri Ngeleja, wengi wao walieleza kutoridhishwa na mipango iliyomo katika hotuba ile.

Mbunge wa Same Mashariki (CCM) Anne Kilango Malecela na mwnezake wa Nkasi,  Ally Mohamed pia wa CCM ndio walioanza kumwashia moto Ngeleja  na kisha  kufuatiwa na wabunge wengine.

Kilango, ambaye amekuwa mpambanaji dhidi ya ufisadi alilalamika kuwa utekelezaji wa miradi ya umeme umependelea zaidi mawaziri wakati kwenye jimbo lake
wamelaghaiwa.

Alitaja baadhi ya mawaziri alidai wamependelewa ni Dk David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) wa Jimbo la Same Mashariki, Aggrey Mwanri (Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- Tammisemi) kutoka  Jimbo la Siha na Profesa Jumanne Magembe (Kilimo, Chakula na Ushirika) ambaye  pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga.


Kilango alilalamika kwamba kwenye hotuba ya Ngeleja alitaja vijiji ambavyo vimesambaziwa umeme kwenye jimbo la Same Mashariki, lakini ukweli vyote vipo Same Magharibi, kwa waziri mwenzake, Dk Mathayo.Kilango hakuvitaja vijiji hivyo, lakini kwa mujibu wa hotuba ya Ngeleja ni Mhezi, Ijinyu, Kijom, Msindo, Mbakweni, Kizungo na Digo.

Alimtaka waziri huyo kuacha kudanganya Watanzania na huku akionyesha upendeleo wa wazi kwa kupeleka miradi mingi ya umeme kwenye majimbo ya maswahiba wake.Mbunge huyo alilalama, "Sisi (wabunge) wote tuko hapa kwa kazi moja tu nayo ni (kujadili) namna ya kuondoa matatizo ya Watanzania. Lakini, mengine tunayoyafanya ni ya kitoto."

Akionyesha kukasirishwa na kuzungumza kwa jazba, Kilango alisema tatizo la umeme linawatesa sana Watanzania.

Akaitaka Serikali iachane na mpango wa kufikiria yenyewe namna ya kutatua tatizo la umeme nchini badala yake iwashirikishe na  wengine.

Katika hatua nyingine, Kilango alisema serikali haitaweza kutatua tatizo la umeme nchini iwapo itaendelea na tabia yake ya kubeba miradi mingi kwa wakati mmoja.

Alisema kitendo hicho husababisha miradi hiyo kushindikana kutekelezwa ama maendeleo yake kwenda kidogo kidogo na kutofikia malengo yake kwa wakati uliokusudiwa.Alisema tatizo la umeme nchini ni la muda mrefu, lakini utatuzi wake umekuwa ni mgumu kwa sababu katika mikakati yake, upo utitiri wa miradi.

Tatizo hilo, alisema linatokana na Serikali kutohusisha mawazo ya watu wengine katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la umeme.Naye Mbunge wa Nkasi (Ally Mohamed)  katika mchango wake alimlaumu Ngeleja kwa kile alichosema ni kudanganya kwenye hotuba yake kuwa katika wilaya yake tayari mradi wa kusambaza umeme umetekelezwa kwa asilimia 62.

Mohamed alisimama baada ya Ngeleja kumaliza hotuba yake na kuomba kutoa taarifa kuwa waziri huyo alikuwa amelidanganya Bunge.

"Alisema (Waziri Ngeleja) kuwa njia ya umeme wa msongo mkubwa umekamilika na usimikaji wa nguzo umetekelezwa kwa asilimia 62. Huu ni uongo. Hakuna hata nguzo iliyochimbiwa ardhini," alilalamika Mohamed.

Alisisitiza kwamba hataunga hoja ya waziri huyo kwa sababu kuna udanganyifu mwingi na kuonya kwamba kama ni maofisa wake, basi walimpelekea taarifa potofu.

Kauli ya Ngeleja
Awali, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake jana, Waziri Ngeleja aliorodhesha utitiri wa miradi ya umeme ambayo inalenga kumaliza tatizo la umeme nchini.

Alisema kuwa mpango wa bajeti hiyo umezingatia mikakati mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa kama vile, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano, Malengo ya Maendeleo ya Milenia na sera za CCM."Lengo la Serikali ni kuimarisha na kuboresha sekta ya nishati na kuongeza fungamanisho la sekta ya madini na sekta nyingine," alisema Ngeleja.

Alitaja miradi 16 akisema ni miongoni mwa ile itakayotekelezwa na Serikali ili kuongeza uzalishaji wa umeme, kupanua na kuboresha njia za umeme, kuendeleza na kupanua miundombinu ya gesi asilia.

Miongoni mwa miradi aliyoitaja Ngeleja ni ule wa mitambo ya kufua umeme ya megawati 100 jijini Dar es Salaam ambao alisema utakamilika Desemba mwaka huu na megawati 60 jijini Mwanza ambao utakamilika Juni mwakani.

Miradi mingine pamoja na muda wa kukamilika kwenye mabano ni Kinyerezi (Dar es Salaam) wa megawati 240 (2013/14), Mnazi Bay (Mtwara) wa megawati 300 (2013/14), Somanga Fungu (Kilwa), megawati 230 (2013/14)Ruhudji, megawati 358 (2015/16).

Mingine ni mgodi wa makaa ya mawe Kiwira (Mbeya) megawati 200 (2013/14), Ngaka wa megawati 400 (2014/15), Mchuchuma megawati 600 (2014/15), Murongo/Kikagati (Kagerea) wa megawati 16 ambao utategemea kukamilika kwa makubaliano kati ya Serikali ya Uganda na Tanzania.
Aliitaja miradi mingine kuwa ni Rusumo (Kagera) wa megawati 63 ambao upo kwenye taratibu za kutafutiwa fedha, Stiegler's Gorge (Pwani) wa megawati 2,100 na Mpanga wa megawati 165 (2015/16).

Pia, aliitaja mingine kuwa ni Rumakali wa megawati 222 (2018), Dar es Salaam-Tanga ambayo ni ya dharura ikijumuiasha Symbion (megawati 112.5), Aggreko (megawati 100), ununuzi wa mitambo itakayofungwa Majani Mapana, Tanga wa megawati 70 na  ule wa gesi wa IPTL, Tegeta jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo aliitaja miakakati mingine ya kuboresha sekta ya nishati ni kuunganisha makao makuu zote za wilaya, kuendelea kusambaza umeme vijijini, utekelezaji wa miradi iliyopo chini ya MCC pamoja na miradi mingine midogo ya umeme ukiwepo unaotokana na nishati ya jua.

Akizungumzia kuhusu sekta ya madini, Ngeleja alisema Sheria ya Madini ya mwaka 2010 imefanyiwa marekebisho mbalimbali ili kuboresha usimamizi wa sekta hiyo."Marekebisho hayo ni pamoja na mfumo wa ukokotoaji wa mrahaba na viwango vipya na ada mbalimbali za leseni za madini," alisema Ngeleja.

Alifafanua kuwa, "Kisheria marekebisho hayo yatawagusa wawekezaji wapya na kampuni ambazo hazina miakataba na serikali."Alisema kuwa Serikali ipo katika mikakati ya kuwasiliana na kampuni ambazo tayari zina mikataba ili sheria hiyo mpya waitekeleze.Migodi hiyo aliitaja kuwa ni Bulyanhulu, Resolute Tanzania Limited, Geita Gold Mine na Buzwagi Gold Mine.Ili kutekeleza miradi hiyo, Ngeleja aliliomba Bunge liidhinishe Sh402.4 bilioni ikiwa ni pamoja na matumikzi ya kawaida.


Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ameliambia Bunge kuwa uhaba wa umeme unaolikumba Taifa kwa sasa unatokana na tatizo la uongozi.

"Hakuna 'seriousness' (umakini) katika kutatua tatizo la umeme," alisema Mbowe wakati akichangia hotuba hiyo ya waziri Ngeleja. Alisema tatizo la umeme limekuwa likilikumba taifa kutokana na mipango yake ya utekelezaji kufanywa kisiasa.Alionya kuwa tatizo hili limekuwa likionekana ni dogo lakini linawaathiri watu wengi hasa kampuni na viwanda vilivyowekezwa nchini na linavitishia kuviangamiza kabisa.

Hali inavyonekana kwa sasa, alisema inaashiria kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja amezidiwa kutokana na kurundikiwa mambo mengi ayafanya kwa wakati mmoja.Kwa sababu hiyo akapendekeza wizara hiyo igawanywe mara mbili kutokana na unyeti wa mambo iliyo nayo juu ya sekta ya madini na nishati.

Alitoa mfano kuwa suala la madini na nishati limekuwa na wawekezaji wajanja sana kiasi kwamba mtu anapokuwa ameelemewa na mambo mengi, anaweza kujikuta akiingia kwenye mikataba mibovu.

Hata hivyo, baada ya kumaliza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alitoa taarifa kuwa kamati ya Makamba ina wajibu wa kuikosoa serikali.Alisema kamati ile inajumuisha wabunge wa pande zote hivyo si ya CCM na ina wajibu wa kuikosoa na kuishauri serikali.

Mbunge wa Kibakwe George Simbachawene, aliwataka wachimbaji wodogo kufuata sheria ili kuepuka matatizo yasiiyokuwa ya lazima."Mtu ukianza kuchimba madini huwezi kufanya shughuli nyingine atachimba madini tu, serikali iwasaidie hawa wachimbaji wadogo siyo kuwasaidia wakubwa tu,"alisema Simbachawene.

Mbunge wa Kasulu Vijijini kwa tiketi ya NCCR Mageuzi  Agripina Buyogera, alisema kukosa umeme wa uhakika katika Mkoa wa Kigoma, ni matokeo ya kukosa viongozi wazuri wa kuhakikisha Mkoa huo unapata umeme wa uhakika.

Alieleza kwamba, mkoa huo unarasilimali za kutosha ambazo zinauwezo mkubwa wa kuhakikisha Mkoa huo unakuwa na Nishati kubwa ya umeme."Kila Mwezi Kigoma umeme unaozalishwa na majenereta unakatika kwa zaidi ya wiki moja, hii ni kutokana na kukosekana kwa mafatuta, kwanini isitumike maporomoko ya mito Iliyopo ili kuondoa kero hii,"alisema Buyogera.
 

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)