Translate in your language

Tuesday, May 17, 2011

SAUT wajipigia debe tuzo za ‘Excel with Grand Malt’


Na Mwandishi wetu,
Mwanza 

KATIKA hali inayoonekana kuwa ni kujipigia debe katika kinyang’anyiro cha tuzo za Excel with Grand Malt, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) cha Mwanza juzi walionyesha vipaji tofauti katika tamasha la uzinduzi wa promosheni ya tuzo hizo lililofanyika katika viwanja vya Chuo hicho jijini Mwanza.
Tamasha hilo lilishuhudia wanafunzi kutoka SAUT wakionyesha vipaji katika fani ya muziki, sanaa ya kuiga sauti za viongozi mbalimbali na hatimaye kucheza soka kati ya wanafunzi wa kozi ya shahada ya juu ya sheria na shahada ya juu ya Elimu, ambapo sheria waliibuka kidedea kwa ushindi wa mikwaju ya penati.
Washindi walioshiriki katika kuonyesha vipaji vyao katika tamasha hili walizawadiwa zawadi mbalimbali zikiwemo mabegi ya kubebea kompyuta za laptop, fulana za Grand Malt na kinywaji cha Grand Malt.
Tamasha hilo lilikuwa ni mwendelezo wa matamasha ya uzinduzi wa tuzo za Excel With Grand Malt ambayo yameishafanyika katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Morogoro na Iringa kama njia mojawapo ya kuhamasisha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kushiriki katika kinyang’anyiro cha tuzo hizo.
Excel with Grand Malt ni promosheni inayoendeshwa na kampuni ya bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake kisicho na kilevi cha Grand Malt, yenye lengo la kutoa tuzo za aina mbalimbali kwa wanafunzi kutoka vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.
Washindi watajinyakulia zawadi mbalimbali ambapo zawadi kubwa itakuwa hundi ya kununulia vitabu yenye thamani ya shilingi 400,000. Tuzo hizo zinashindaniwa katika makundi manne ambayo ni utamaduni na burudani, huduma za jamii na mazingira, ugunduzi na kipaji maalum.
Mbali na chuo cha SAUT, vyuo vingine vilivyoshiriki katika kinyang’anyiro cha tuzo hizo ni Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara na Taasisi ya Jamii.
Vingine ni Chuo Kikuu Cha Elimu (DUCE), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa na Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa.
Washindi watapatikana kwa njia ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu ya mkononi kwenda namba 0658-517517, kupitia tovuti ya Grand Malt ambayo ni http://www.excelwithgranmalt.com/. Pia kutakuwa  na viboksi vya kura katika maeneo mbalimbali ya vyuo vinavyoshiriki kama vile kwenye maduka, hosteli, kwenye migahawa .

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)