Na Andrew Chale
MEI 8 kila mwaka tunakumbuka siku ya kuanzishwa kwa Chama cha Msalaba Mwekundu kilichoasisiwa na mfanyabiashara Mswisi, Henry Dunant, kufuatia mapigano ya Solferino yaliyotokea wakati wa vita ya Austria dhidi Italia na Ufaransa mwaka 1859.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Uwe na moyo wa kujitolea" na sherehe za kitaifa za mwaka huu zimefanyika Mei 8 mkoani Mara.
Historia ya chama
Hadi karne ya 19, hapakuwa na utaratibu rasmi wa matibabu na huduma ya uuguzi kwa wanajeshi walioathirika na majanga ya vita na hasa majeruhi.
Hivyo kama bahati kwa Dunant alipokuwa akisafiri nchini Italia mnamo Juni 24, 1859, akiwa njiani kuelekea kuonana na mfalme Kaizari wa Ufaransa Napoleon wa III, kwa lengo la kujadili matatizo ya kibiashara yaliyokuwa yakiwatokea nchini nchini Algeria, ambayo kwa wakati huo Algeria ilikuwa ikimilikiwa na Ufaransa.
Dunant alipofika mji mdogo wa Solferino ilikuwa jioni ya Juni 24, ambapo alishtushwa na hali ya kutisha baada ya kushuhudia Vita ya Solferino.
Vita hiyo ilikuwa ni moja wapo ya mapigano kati ya Vita ya Austro-Sardinian, ambapo kwa siku moja, takriban askari 40,000 pande zote mbili walikufa huku wengine wakiwa wamejeruhiwa.
Kwa hali hiyo, Dunant alishtushwa na mateso ya askari waliojeruhiwa na uhaba wa matibabu na huduma za kimsingi.
Anatupilia mbali madhumuni ya hapo awali ya safari yake na kwa siku kadhaa akajitolea kusaidia katika matibabu na kuwauguza waliojeruhiwa.
Anafanikiwa kupanga msaada wa dharura kwa kuwahamasisha wakazi kutoa misaada bila ubaguzi. Anaporudi kwao mjini Geneva , anaandika kitabu kiitwacho 'A Memory of Solferino'.
Katika kitabu hicho aliweza kuandika mambo mbalimbali ikiwemo kubuniwa kwa mikataba ya kimataifa kuhakikisha ulinzi wa madaktari wasioegemea upande wowote wa hospitali katika maeneo ya vita ili kusaidia askari waliojeruhiwa vitani.
Februari 9, 1863, Dunant akiwa mjini Geneva , aliungana na raia wengine 5 na kuanzisha kamati maalum ya kusaidia waathirika wa vita iliyofahamika kama tume ya uchunguzi ya Geneva Society for Public Welfare.
Wajumbe hao ni Gustave Moynier,(mwanasheri), Louis Appia (Daktari), Theodore Maunoir(Daktari) na Guillaume Henri Dufour (Jenerali wa Jeshi la Uswisi).
Siku nane baadaye, kamati hiyo inaamua kubadili jina la kamati na kuanza kujulikana kama Kamati ya Kimataifa ya Kutoa Misaada kwa waliojeruhiwa wakati wa Vita (International Committee for Relief to the Wounded).
Kamati hiyo kwa sasa inajulikana kama Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (International Committeee of the Red Cross-ICRC).
Mwaka 1864) serikali ya Uswisi ilipitia Mkataba wa Geneva na kuboresha hali ya askari , majeruhi katika eneo la vita na mataifa hayo yote yalitiliana saini.
Mkutano huo pia ulibainisha masharti mawili maalum ambayo yangelitambulisha shirika la kitaifa la kutoa misaada kwa kamati ya kimataifa ambapo shirika hilo la kitaifa lazima litambuliwe na serikali ya taifa kama shirika la kutoa misaada kulingana na mkataba huo.
Matumizi ya alama ya Msalaba Mwekundu yalianza kutumika kwa mara ya kwanza kwenye vita ya Dybbøl ( Denmark ) mwaka 1864, kufuatia mgogoro wa silaha kati ya nchi hizo ambapo Louis Appia na Charles van de Velde, kapteni katika jeshi la Uholanzi walikuwa wajumbe wa kwanza wasioegemea upande wowote kufanya kazi chini ya Msalaba Mwekundu katika vita hiyo.
Mwaka 1876, kamati ilijipa jina la 'Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu' (ICRC) ambalo ndilo jina lake rasmi hadi hivi sasa.
Miaka mitano baadaye, Shirika la Msalaba Mwekundu la Marekani lilianzishwa kwa juhudi za Clara Barton.
Nchi zaidi zilitia saini mkataba wa Geneva na kuanza kuuheshimu kwa uhalisi wakati wa vita na katika muda mfupi tu, Shirika la Msalaba Mwekundu lilipata kasi kubwa kama shirikisho la kuheshimika kimataifa.
Tuzo ya Amani ya Nobel ilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1901, Kamati ya Nobel ya Norway iliamua kumtuza Henry Dunant pamoja na Frédéric Passy, mwanaharakati wa kimataifa.
Mwaka 1906, mkataba wa Geneva wa 1864 uliundwa upya kwa mara ya kwanza na baadaye mkataba wa Hague X, ulioratibiwa katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Amani mjini Hague, ulipanua mkataba wa Geneva kujumuisha pia vita ya majini.
Muda mfupi kabla ya Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia kuanza mwaka wa 1914, na miaka 50 baada ya kuanzishwa kwa ICRC na kupitishwa kwa mkataba wa Geneva , tayari kulikuwa na vyama vya kitaifa 45 duniani kote.
Mnamo Oktoba 15, 1914 punde tu baada ya kuanza kwa vita, ICRC ilianzisha uwakala wake wa kimataifa kwa wafungwa wa vita (POW), ambao walikuwa 1,200 wengi wao wakiwa wafanyakazi wa kujitolea kabla ya mwisho wa 1914.
Mnamo Desemba 10, 1963, shirikisho hili pamoja na ICRC zilipokea tuzo ya Amani ya Nobel na mwaka 1983, shirikisho lilibadili jina na kuitwa 'Ligi ya Vyama vya Msalaba na Hilali Nyekundu' kuonyesha kuongezeka kwa idadi ya vyama vya kitaifa chini ya Chama cha Hilali Nyekundu.
Jina la ligi lilibadilishwa tena mwaka wa 1991 na kuwa rasmi la 'Shirikisho la kimataifa la Msalaba Mwekundu na vyama vya Hilali Nyekundu'.
Siku hii ya Chama cha Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu ilisherekewa kwa mara ya kwanza duniani kote Mei 8, 1948.
Tokea hapo, mwaka 1953, siku ya Msalaba Mwekundu duniani imekuwa ikilenga kila mwaka kwa ujumbe unaohusu kazi za chama hicho duniani.
Mwaka wa 1997, ICRC na shirikisho zilitia saini mkataba wa Seville ambao uliainisha majukumu ya mashirika ndani ya muungano ambao uligawanywa sehemu kuu 3.
Muungano huo ni Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) na vyama vya kitaifa vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (NATSOC).
Kwa jumla, kuna watu milioni 97 duniani kote ambao hutumikia ICRC, Shirikisho la kimataifa na vyama vya kitaifa.
Kanuni saba za msingi
Kongamano la kimataifa la 1965 mjini Vienna liliratibisha kanuni saba za msingi ambazo zilifaa kutumiwa na pande zote za muungano na ziliongoza kwa masharti rasmi ya muungano mwaka 1986.
Kanuni hizo ni ubinadamu, kutopendelea, kutoegemea upande wowote, uhuru, kazi ya kujitolea, umoja na ujumuiya.
Kuanzishwa kwake Tanzania
Kwa hapa nchini Chama cha Msalaba Mwekundu kilianzishwa kwa sheria ya Bunge ya mwaka 1962. Kabla ya hapo chama kilikuwa tawi la Chama cha Msalaba Mwekundu cha Uingereza lililoanzishwa mwaka 1949.
Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), pia kilitambulika kama chama cha kimataifa na kukubaliwa kwenye jumuiya ya kitaifa mwaka 1962 baada ya serikali kutiliana saini mikataba ya Geneva Desemba 12, 1962.
Hitifaki za nyongeza zilitiwa saini Februari 15, 1983 na hatimaye Bunge la Tanganyika lilipitisha sheria Na. 71 ya mwaka 1962.
Chama hicho kimeweza kufanya shughuli mbalimbali za uokoaji ikiwemo vita ya Kagera, ajali ya Mv Bukoba, ajali ya treni Dodoma,Milipuko ya Mabomu Mbagala,Gongolamboto.
Matukio mengine ni pamoja na Mafuriko ya Kilosa,Mvomero NK...ambapo kikosi kazi maalumu kwa kushirikiana na wanachama wamekuwa mstari wa mbele kutoa huduma ya kwanza na uokoaji.
Mbali na kufanya shughuli hizo, pia chama kinajishughulisha na kutoa huduma kwenye matukio ya uwanjani wakati wa michezo na matembezi mbalimbali ambapo wanakuwa katika hali ya utayari kusaidia kutoa huduma ya kwanza.
Makala hii imeandaliwa na Andrew Chale,ambaye pia ni mwanachama wa Msalaba Mwekundu Tanzania na mjumbe wa Kikosi cha Maafa na Uokoaji mkoa wa Dar es Saalaam,(Action Team).
Makala hii pia imeandaliwa msaada wa mtandao pamoja na kitabu cha Habari na Uhamasishaji cha Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS).
Mwisho
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa