NA MWANDISHI WETU
ZIKISALIA siku 21 kabla ya kufanyika kwa Tamasha la kimataifa la muziki wa Injili kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam hapo Aprili 24, waimbaji waliothibitisha, wameanza mazoezi ya kujiweka fiti kabla ya tukio hilo la kimataifa.
Hili ni tamasha la Pasaka litakalofanyika pia katika uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro siku ya Aoprili 25 kabla ya kuhamia uwanja wa CCM Kirumba, siku ya Aprili 26.
Kamati ya maandalizi kwa upande wake chini ya Alex Msama ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya Msama Promotions inayoratibu Tamasha hilo, anasema hadi sasa maandalizi yote muhimu yamekamilika.
“Namshukuru Mungu kwamba maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa kiwango kikubwa, na kilichobaki ni kuzidi kuwaombea wote wanaotamani kufika Diamondi Jubilee, Jamhuri na CCM Kirumba, kwamba kwa uwezo wake Mungu, wafanye hivyo bila kukosa,” anasema.
Msama amewataka wadau ambao wamekuwa wakiliombea tamasha hilo, wazidi kufanya hivyo wakiwaombea wote akiwemo Rais Jakaya Kikwete atakayekuwa mfeni rasmi katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Kuhusu waimbaji, Msama anasema wote ambao wameshathibitisha kushiriki tamasha hilo linalotarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake, wameanza maandalizi ili kila atakayefika ukumbini, asiondoke kama alivyokwenda.
“Kamati yangu imejitahidi kufanya kila iwezalo kuhakikisha tamasha hili linakuwa lenye kiwango
cha ubora wa hali ya juu, anasema Msama.
Wakati Msaka anayasema hayo, je waimbaji ambao siku hiyo ndio watapamba jukwaa mbele ya Rais Kikwete, wanasemaje?
Rose Muhando, malkia wa muziki wa injili wa mwaka 2009, anasema hawezi kusema mengi, isipokuwa anatoa wito kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili, kufika kwa wingi Diamond Jubilee.
Katika hali ya kawaida, binadamu unaweza ukapanga hivi, lakini Mwenyezi Mungu akapanga vinginvyo, hivyo niseme tuombe tuifike siku hiyo.
Muhando ambaye hivi karibuni alishirikishwa na Annastazia Mukabwa wa Kenya katika albamu ya ‘Kiatu,’ anasema Tamasha la Pasaka kwake ni kitu cha kipekee.
Rose aliyetamba na kung’ara na vibao mbalimbali katika anga ya muziki wa injili, anasema ana sababu mbili zinazolifanya Tamasha la injili kuwa la kipekee kwake.
Anasema, sababu ya kwanza, Pasaka ni alama ya ushindi wa Yesu Kristo dhidi ya dhambi kwa niaba ya wanadamu, hivyo ni fumbo lenye maana kubwa kwa maisha ya kiroho.
Rose anaongeza kuwa, kwa vile Pasaka huadhimishwa mara moja tu kwa mwaka, hivyo uwepo wake katika jukwaa la Diamond Jubilee siku hiyo, ni njia mojawapo ya kuisindikiza Pasaka.
“Sababu ya pili inayofanya Pasaka iwe ya kipekee kwangu, ni kwamba siku hiyo nitakuwa nikishambulia jukwaa huku nikikumbuka siku ya ubatizo wangu” anasema Rose.
Mwimbaji mwingine aliyezungumzia Tamasha hilo, ni Mukabwa ambaye kwa sasa anatamba na albamu ya
‘Vua Kiatu’ aliyomshirikisha Rose Muhando.
Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi, Kenya, Mukabwa amesema tayari alishaanza mazoezi kwa lengo la kutoa burudani ya uhakika siku hiyo mbele ya mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete.
Mbali ya kibao cha Kiatu kilichobeba jina la albamu, vibao vingine vilivyomo kwenye albamu hiyo ni
‘Ee Mungu’, ‘Tabu zangu’, ‘Usiwe Manamba’, ‘Nzizilela’, ‘Nishike Mkono Bwana’ na ‘Wanaokudharau’ na Mfalme.
“Naomba Mungu anijalie uzima na afya siku hiyo, mimi binafasi, ninaitamani sana siku hiyo kwa sababu ni heshima ya aina yake kuimba mbele ya mkuu wa nchi, pia kukutana na waimbaji wengine kama dada yangu Rose,” anasema Mukabwa.
Kuhusu tamasha, Mukabwa anasema ingawa itakuwa mara ya kwanza kwake kushiriki, anaamini litakuwa lenye mvuto wa aina yake kutokana na uzoefu wa Msama na Kamati yake.
Msama na kamati yake, ndio imechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki wa injili kupitia matamasha mbalimbali ya Pasaka, krismas au uzinduzi wa albamu kadha wa kadha tangu mwaka 2000.
Mwimbaji mwingine aliyezungumzia tamasha hilo na maandalizi yake, ni Solomon Mukubwa, mwimbaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo anayeishi nchini Kenya .
Mukubwa ambaye si mara ya kwanza kwake kutumbuiza kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, anasema yupo fiti licha ya kubaki na mkono wake mmoja wa kulia kwani huohuo unatosha kufanya vitu vya kumtukuza Mungu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.
Mukubwa anayetamba na wimbo wa 'Mfalme wa Amani', anasema hiyo ni nafasi muhimu kwake kushirikiana na wengine kushambulia Jukwaa la Diamond Jubilee mbele ya Rais Jakaya Kikwete.
“Pamoja na kubaki na mkono mmoja, haunizuii kumuimbia Mungu, hivyo wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili waje washuhudie na kupata baraka za Mungu kupitia uimbaji,” anasema.
Mukubwa anayekiri kwamba kwenda kwake nchini Kenya ilikuwa ni kumfuara mwimbaji wa nyimbo za Injili Angela Chibalonza ambaye kwa sasa ni marehemu, anaamini kila atakayekuja kwenye Ukumbu wa Diamond Jubilee, ataondoka na baraka za Mungu.
Mbali ya Mukubwa aliyetokea familia ya watoto tisa (saba wa kiume), waimbaji wengine watakaopamba tamasha hilo la kimataifa, ni Boniface Mwaitege na Pamela Wanderwa.
Mukubwa aliyemwoa Betty Japheth tangu Machi mwaka jana, ni kati ya waimbaji mahiri wa muziki wa injili katika ukanda wa Afrika mashariki na Kati wenye mapenzi makubwa na Tanzania .
Mwaitege ambaye kwa sasa aliyewahi kutamba na vibao mbalimbali kama ‘Mke Mwema’ na ‘Utamtambuaje’ kwa sasa anatesa na albamu yake ya Mama ni Mama iliyojaa vibao vyenye ujumbe wa kuvutia.
Akizungumzia tamasha hilo, Mwaitege amesema hana mengi ya kuzungumza isipokuwa amewataka wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili, kufika Ukumbi wa Diamond Jubilee kusikia ujumbe wa neno la Mungu kupitia vipawa vya uimbaji kutoka kwa waimbaji watakaohudumu siku hiyo.
“Nashukuru kupata nafasi hii ya kuimba kwenye Tamasha kubwa la Pasaka, ni nafasi ya kipekee kwangu kujumuika na waimbaji wengine kufurahia ushindi wa Yesu Kristo pale Msalabani,” alisema Mwaitege kwa njia ya simu.
Kuhusu maandalizi, Mwaitege amesema tayari ameshaanza kujipanga kwa ajili ya tamasha hilo kwa lengo la kutoa burudani ya kutosha kwa kadri Mungu atakavyomjalia.
Naye Upendo Nkone ambaye ni kati ya waimbaji watakaopamba jukwaa la Diamond Jubilee mbele ya Rais Kikwete, anasema ni furaha kubwa kwake kujumuika na waimbaji wengine kwenye tukio hilo la aina yake.
Anasema, Pasaka ni alama ya ushindi wa Yesu Kristo dhidi ya dhambi baada ya kuteswa, kufa na kufufuka kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu kutoka katika vifungo vya dhambi, hivyo kujuika na wengine siku hiyo, kwake ni siku ya kipekee.
“Nashukuru sana kupata nafasi hii ya kujumuika pamoja na waimbaji wengine na wananchi kwa ujumla bila kujali kama ni mkristo au vinginevyo kwa sababu sote tu wana wa Mungu,” anasema Nkone.
Anasema, anamwomba Mungu amjalie uzima na afya ili siku hiyo aende Diamond kuchota baraka za Mungu kwa sababu wakusanyikapo wawili watatu kwa jina la Mungu, naye huwepo mahali hapo, hivyo Mungu atakuwepo Diamondi Jubilee.
Anasema pamoja na malengo mengine ya uwepo wa tamasha hilo kwa mfano sehemu ya kile kitakachopatikana kuwafariji yatima, wajane na wengine wenye shida, anatoa wito pia kwa kila atakayefika Diamond Jubilee, autumie nafasi hiyo kusamehe wengine.
“Natoa wito kwa wote watakaofika Diamond Jubilee kuwa na furaha pamoja na ufufuko wa Yesgu Kristo kwa kungua mioyo yao kwa kuwasamehe hata wale waliowakosea badala ya kuhama kiti
kimoja hadi kingine kumkimbia mwenzako,” anasema Nkone.
Christina Shusho kwa uopande wake, hakuna na mengi ya kusema isipokuwa amewawataka wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili wasikose kwenda ukumbi wa Diamond Jubilee siku ya Aprili 24 kupata baraka za Mungu kupitia uimbaji.
Amedokeza kuwa, ni furaha kubwa watu kujumuika pamoja wakipata burudani ya nyimbo za kumsifu na kumwinua Mungu kwa matendo yake makuu ya kumleta mwanaye Yesu Kristo kuzifia dhambi Msabani ili wanadamu waweze kupata ukombozi.
Kwa upande wake Msama, Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu Tamasha hilo, anasema baada ya Diamond Jubilee, waimbaji wote ambao watahudumu hapo, siku inayofuata watakuwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na Aprili 26, CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Msama, anasema sambamba na kuwakutanisha wengi kufurahia ufufuko wa Yesu Kristo, lengo jingine la Tamasha hilo, ni kutumia sehemu ya fedha itakayopatikana kuwasaidia watoto yatima na wajane.
Aidha, Msama amesema fedha nyingine itaelekezwa kwa waathirika wa mabomu yaliyotokea Februari 16, katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Gongo la
Mboto, Dar es Salaam .
Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi sita ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia .
Kiingilio cha Diamond, ni sh. 4,000 kwa viti vya kawaida; viti vya maalumu (B) sh. 10,000 na viti maalumu (A) sh. 20,000.
Msama alisema tiketi za viti maalumu vya VIP A zitakazokuwa kama meza za familia, watakaohitaji watalazimika kupiga simu selula 0713 383838, 0786 383838 na 0786 373737 ili kupata ufafanuzi zaidi.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa