SOFAPAKA KULA SAHANI MOJA NA SIMBA SC ![]() WAWAKILISHI wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati 'Kombe la Kagame', Simba wamepangwa Kundi C pamoja na Sofapaka wa Kenya, URA ya Uganda na wenyeji Atraco ya Rwanda. Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki (Cecafa), Nicholas Musonye imesema wawakilishi wa Zanzibar Mafunzo wamepangwa kundi B pamoja na timu nyingine ya Rwanda Rayon Sport, St Georges ya Ethiopia na Heartland ya Nigeria. Kundi A lina timu za APR ya Rwanda, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Vital 'O' ya Burundi na Telkom ya Djibout. Musonye alisema kuna klabu nyingi ambazo si wanachama wa Baraza hilo zimeomba kushiriki michuano hiyo, lakini kutokana na hali ilivyo zimeteuliwa TP Mazembe inayoshiriki kwa mara ya pili na Heartland kuwawakilisha. Michuano hiyo itaanza Mei 15 hadi Mei 29 mwaka huu Kigali, Rwanda. Alisema Serikali ya Rwanda pamoja na wadhamini wa soka nchini humo ndio watadhamini michuano hiyo kwa kutoa dola za Marekani milioni moja ambazo zitatumika katika kugharamia tiketi za ndege kwa timu shiriki, viongozi wao na waamuzi, malazi pamoja na fedha za zawadi. "Tunachukua nafasi hii kumshukuru Rais Paul Kagame wa Rwanda kwa kuendelea kudhamini michuano hii kwa mwaka wa 15 sasa na kuendelea kuipa Cecafa uhai,"alisema. Mwaka jana ilifanyika Sudan ambapo Atraco ndio iliibuka bingwa. Simba itabidi ijizatiti zaidi maana ipo pamoja na mabingwa hao watetezi Atraco, pia itakumbana na timu za URA na Sofapaka ambazo imewahi kukutana nazo kisha ikafungwa. Sofapaka ilikutana nayo mwishoni mwa mwaka jana katika michuano ya Kombe la Tusker, wakati URA ilikutana nayo katika michuano ya Kombe la Kagame mwaka juzi yote jijini Dar es Salaam. |
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa