Translate in your language

Wednesday, April 14, 2010

LUKUVI ALIFANYA 'SAPLYAIZII!! MW'NYAMALA Hosp
 

UONGOZI na wafanyakazi wa Hospitali ya Mwananyamala hawakutaarifiwa mapema kuhusu uhamisho wa watumishi 96 uliotangazwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, habari ambayo jana ilizua taharuki na kuzorotesha huduma kwenye hospitali hiyo ya wilaya.

 

Juzi mkuu huyo, William Lukuvi aliwaambia waandishi wa habari kuwa serikali ya mkoa wake imeamua kuwahamisha wafanyakazi 57 wa hospitali hiyo, ambayo imekuwa ikikumbwa na mikasa mingi inayoonekana kusababishwa na uzembe, kuwapeleka hospitali mbalimbali za jiji la Dar es Salaam na wengine 39 kwenda ya mkoa.

 

Lukuvi alisema ili kuziba pengo hilo, serikali imepeleka wafanyakazi wapya 58 katika hospitali hiyo ya serikali iliyo kwenye Manispaa ya Kinondoni.

 

Lakini mganga mkuu wa Mwananyamala, Suleiman Muttani aliwaambia waandishi wa habari hospitalini hapo jana kuwa hana taarifa zozote kuhusu uhamisho huo zaidi ya kusoma habari hizo kwenye magazeti.

 

Sina taarifa yoyote kuhusu uhamisho wala sijapokea mfanyakazi yeyote mpya katika siku za hivi karibuni hospitalini hapa," alisema Muttani.

 

Hata hivyo, Dk Muttani alieleza kuwa uhamisho wa watumishi wa hospitali hiyo ni wajibu wa katibu wa afya wa Manispaa ya Kinondoni ambaye hajawasiliana naye kuhusu suala hilo.

 

Nadhani mwenye majibu ya uhamisho huo ni katibu wa afya wa manispaa kwa sababu wao ndio wenye mamlaka ya kutoa taarifa ya mabadiliko hayo kwa mkuu wa mkoa na baadaye sisi tunaletewa taarifa tu. Lakini niseme kwamba mpaka sasa wafanyakazi wote hatuna taarifa,†alisema Dk Muttani.

 

Mganga huyo alisema kuwa anaupokea uhamisho huo kama kweli upo kama changamoto katika utumishi wa umma, akisema kuwa matatizo makubwa yanayofanya hospitali hiyo ionekane kuwa na sifa mbovu ni ufinyu wa bajeti ya uendeshaji na maslahi madogo kwa wafanyakazi.

 

Taarifa hizo za uhamisho hazikuwa nzuri kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo kubwa ya serikali wilayani Kinondoni na ilisababisha watumishi hao wakae kwenye vikundi kujadili habari hizo, huku huduma zikizidi kuwa mbovu.

 

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wafanyakazi hao walisema taarifa za uhamisho huo zimewastua na kwamba zinaweza kuchangia utendaji mbovu katika siku ambazo watakuwa wakiendelea kufanya kazi kwenye kituo hicho kusubiri barua za uhamisho.

 

“Sisi kama wafanyakazi tumepigwa na butwaa kiasi kwamba leo kila mtu hana morali wa kufanya kazi kwa kwa sababu idadi ya waliohamishwa ni kubwa mno na hakuna anayefahamu amepelekwa wapi katika uhamisho huo,†alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

Lukuvi hakupatikana jana kueleza kama serikali yake ilishawataarifu wafanyakazi hao kuhusu mpango wa kuwahamisha ili kuepuka kusababisha kudorora kwa huduma kwenye sehemu hiyo muhimu.

 

Hata hivyo baadhi ya wananchi wamefurahishwa na uamuzi huo wa serikali wakielezea kuwa unaweza kuongeza ufanisi katika utendaji wa wafanyakazi hospitalini hapo ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa uzembe unaosababisha kupotea kwa maisha ya watu, hasa watoto.

 

Mimi binafsi nimepokea uamuzi huo wa serikali kwa furaha sana kwa sababu mimi ni mmoja wa wananchi waliowahi kukumbwa na kero za hospitali hii, alisema Mustafa Shumu.

 

Shumu alisema uhamisho huo utaongeza ufanisi kwa watakaosalia na hata wafanyakazi wapya.

 

Hii ni mara ya pili kwa uongozi wa serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kuhamisha watumishi wa hospitali hiyo kwa lengo la kuongeza ufanisi baada ya kufanya hivyo mwaka 2008.

 

Uhamisho huo wa mwaka 2008 ulianzia kwa mganga mkuu na msaidizi wake pamoja na baadhi ya watumishi, huku aliyekuwa msaidizi wa mganga mkuu wa wakati huo, Dk Aisha Mahita akipandishwa kuwa mganga mkuu wa Hospitali ya Temeke.

 

Matatizo makubwa ambayo yamekuwa yakiripotiwa hospitalini hapo ni uzembe wa wafanyakazi wa kitengo cha uzazi, kukiwa na taarifa kadhaa za akina mama kuzidiwa wakiwa mapokezi na watoto kufariki kutokana na kuchelewa kupata huduma.


No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)