Translate in your language

Tuesday, August 30, 2011

Tanzania yakiri Gaddafi kuangushwa



*Bendera ya waasi yapandishwa 'Dar' 
Bendera ya waasi ikipepea katika Ubalozi wa Libya nchini uliopo jijini Dar es salaam jana. Kushoto ni waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe akitoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa Tanzania na kuanguka kwa utawala wa Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.

 Na Charles  Lucas

TANZANIA imekiri utawala wa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, kuangushwa huku ubalozi wa nchi hiyo nchini, ukipandisha bendera ya waasi.Kuangushwa
kwa utawala wa Kanali Gaddafi, kumethibitishwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.


"Kimsingi utawala wa miongo minne wa kiongozi wa Libya Kanali Ghaddafi umeanguka kutokana waasi hao wanasaidiwa na mataifa ya magharibi kuteka na kudhibiti miji mingi ukiwemo Mji Mkuu wa Tripoli," alisema Bw. Membe na kuongeza kuwa mapigano bado yanaendelea ndani ya nchi hiyo.

Alisema Tanzania na Umoja wa Afrika (AU) zinasisitiza mazungumzo ya amani ili kufikia makubaliano. Aliongeza kuwa Tanzania  imekuwa ikifanya hivyo kutafuta suluhu la   migogoro mingi kwenye nchi nyingi za Afrika.

Alisema mgogoro wa Libya una sura ya koo mbalimbali kupingana, hivyo si rahisi kuutambua utawala wa waasi ambao bado haujawa na mfumo unaoeleweka.

"Unapozungumzia serikali si kikundi kinasimama na kusema ni utawala, hapana serikali ni lazima iwe mfumo unaokubalika wa Mahakama, Bunge na Utawala,  sisi tunataka wafikie hapo kwa faida ya Walibya," alisema Bw. Membe.

Alisema pamoja na nchi nyingi kutambua Baraza la Waasi, Tanzania haitafanya hivyo hadi hapo taratibu muhimu zitakapofuatwa kwa manufaa ya pande zote zinazohusika katika mgogoro huo.

Aliongeza kuwa awali AU ilionya hatua ya kuwaunga mkono waasi, lakini Balaza Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kudhibiti matumizi ya anga ya Libya, kwa nia ya kulinda usalama wa raia dhidi ya mashambulizi ya vikosi vya serikali, lakini baadhi ya mataifa ya magharibi yalitafsiri vibaya azimio hilo, kwa kutumia nafasi hiyo kushambulia utawala uliopo madarakani.

Alipoulizwa kuhusu hatua ya ubalozi wa Libya nchini kupandisha bendera ya waasi, Bw. Membe alisema Libya kama nchi ina haki ya kufanya jambo ndani ya ubalozi, bila kuathiri uhusiano wa kimataifa.

Alisema sehemu ile (ubalozini) kwa mujibu wa sheria za kimataifa ni ardhi ya nchi nyingine na kuwataka Walibya waliopo nchini kuwa watulivu katika kipindi hiki.

Bw. Membe pia alizungumzia tatizo  la njaa kwenye nchi ya Somaria na kuelezea kuwa ni janga la kutisha linalohitaji msaada wa haraka.

Alisema Tanzania inashiriki  kuhakikisha msaada wa chakula unapelekwa haraka kuokoa maisha ya binadamu.Alisema Tanzania itatoa kiasi cha dola za Marekani 200,000 kusaidia wananchi wa nchi hiyo.

Alisema ili kuunga mkono juhudi za jumuiya za kimataifa za kuokoa maisha ya Wasomaria wanaokufa kwa njaa, Tanzania imetoa msaada wa tani 300 za chakula na pia itauza kwa bei ndogo chakula cha akiba tani 11,000 kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) ili kisaidie kunusuru watu zaidi ya milioni 12 wanaokabiliwa na njaa.

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)