Translate in your language

Wednesday, January 25, 2017

Tamasha la Sauti za Busara 2017 kurindima Februari9-12, Wasanii 400 wa Afrika jukwaani Zanzibar

Uongozi wa Busara Promotions wenye makao yake Visiwani Zanzibar, mapema leo 24 Januari 2017, umetoa taarifa kwavyombo vya habari juu ya kufanyika kwa tamasha hilo mwezi ujao yaani 9-12 Februari mwaka huu huku likitarajia kupandisha wasanii 400 kutoka kwa vikundi 40 vya muziki kutoka Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Busara Promotions ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Bwana Yusuf Mahmoud ‘DJ Yusuf’ amebainisha kuwa, watu wengi wamekuwa na shahuku kubwa ya kuliona tamasha hilo hivyo kwa mwaka huu watalifurahia kwa kiwango kikubwa litakapolindika ndani ya viunga vya Unguja, Zanzibar.

“Watu wa rangi na umri tofauti kwa mara nyingine tena wataungana, kusherehekea muziki wa Afrika. Zanzibar itakuwa kwenye shamrashamara na mikusanyiko mikubwa ya wageni mbalimbali na mahoteli na maeneo mengine ya malazi na vyakula pamoja na sehemu za biashara zitaendelea kujaa maradufu” amesema Mkurugenzi wa tamasha hilo Yusuf Mahmoud.

Na kuongeza kuwa, kauli mbiu ya tamasha hilo kwa mwaka huu ni #AfricaUnited. Ikiwa na maana kuwa Muziki unaunganisha : Mtu na mtu, moyo na moyo. Katika dunia inayozidi kugawanyika, lugha ya muziki unaohamasisha umoja na urafiki na mshikamano kwenye mipaka yetu.


Mkurugenzi Mtendaji wa Busara Promotions ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud ‘DJ Yusuf’ akionesha kitabu chenye progamu ya tamasha hilo kwa mwaka huu wa 2017 kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema leo Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tamasha la Sauti za Busara, Mh. Simai Mohamed Said amewashukuru wadau wote kwa kuendelea kuliunga mkono tamasha hilo kwani uwepo wake umesaidia na linaendelea kusaidia fursa za kiuchumi na kuinua tamaduni za kiafrika Duniani kote.

“Tunaishukuru Serikali, Mabalozi, wadhamini wote, Wanahabari na wadau wenginekwapamoja kwa kuendelea kutuunga mkono na kufanikisha tamasha hili kubwa kabisa barani Afrika ambalo ni la 7 kwa ukubwa. Kwa ukubwa huo lakini tunapata changamoto hasa kwa kuwapata wafanyabiashara kujitokeza kuwekeza kwa tamasha letu kwani licha ya kuwanufaisha wafanyabiashara hao lakini wamekuwa nyuma sana kujitokeza kudhamini tunatoa wito kujitokeza na milango ipo wazi.

Mh. Simai Mohamed Said pia amebainisha kuwa, ametoa maombi rasmi kwa Serikali hasa kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli akipata nafasi aweze kutembelea Zanzibar kujionea tamasha hilo kubwa kabisa Barani Afrika la Sauti za Busara.

“Napeleka maombi yangu rasmi kwa Rais wetu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, kumuomba akipata nafasi basi aje kujionea mwenyewe jinsi gani vijana, wananchi wake tunavyoitangaza Tanzania ili kutambulika katika mipaka tofauti na kuvutia fursa za kiuchumi, utamaduni na kiuwekezaji kwani pia tumekuwa tukipokea mabalozi kutoka sehemu mbalimbali Duniani kote kuja kwenye tamasha hili na wawekezaji ambao wanafika Visiwani Zanzibar.” Amebainisha Mh. Simai Mohamed Said.


Mwenyekiti wa Bodi ya Tamasha la Sauti za Busara, Mh. Simai Mohamed Said akizungumza katika mkutano huo na wanahabari Jijini Dar es Salaam. Anayemfuatia ni Mkurugenzi wa tamsha hilo Dj Yusuf Mahmoud na mwisho ni Meneja wa tamasha, Journey Ramadhan
Naye Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mh. Hanne Marie Kaarstad ambao ni wadhamini wakuu na wa muda mrefu wa tamasha hilo wamepongeza juhudi za uongozi wa Sauti za Busara za kuinua utamaduniwa Mtanzania, Mzanzibar pamoja na tamaduni za Kiafrika kwa kupitia sanaa za muziki unaowakutanisha watu wote pamoja na kufurahia ala hizo za muziki ambapo pia amebainisha kuwa wataendelea kutoa sapoti kwa tamasha hilo.

Kwa upande wake, Meneja wa tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhan amesema kuwa, wasanii wote watatumbuiza ‘Live’ kwa asilimia 100 na hali hiyo hufanya tamasha hilo kuwala kipekee na tofauti kwani uonyesha uhalisia na ufanisi huku kipaumbele kikitolewa kwa wasanii chipukizi wanaofanya muziki unaotambulisha utamaduni.

Journey Ramadhan amebainisha kuwa,kipaumbele cha tamasha hilo ni kuhakikisha kila mmoja anamudu kiingilio hivyo kwa watanzania wataweza kulipia TSh. 6,000 kwa siku huku kwa atakayetaka kulipia kwa siku zote nne atalipa Tsh. 20,000.



Meneja wa tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhan akizungumza katika tamasha hilo leo


Monday, January 23, 2017

DK. KIGWANGALLA ASHIRIKI MAULIDI YA KUADHIMISHA KUZALIWA MTUME MUHAMMAD (SAW) DAR ES SALAAM

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla leo 22 Januari 2017 (jana), ameshiriki Maulid ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), yaliyoandaliwa na kampuni ya Nida Textile Mills Ltd, ambapo pia hafla hiyo mgeni rasmi alikuwa Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa kiserikali akiwemo Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohammed Gharib Bilal na viongozi wa Dini nchini.

Katika hafla hiyo, Al-Haji Ali Hassan Mwinyi amewataka watanzania kuwa na tabia ya kuyafanyia muendelezo yale mema wanayoyafanya, kama walivyofanya kampuni hiyo ya Nida na kuwakutanisha pamoja waislamu na kumsifu katika kumbukumbu hizo za kiongozi wa waislamu Mtume Muhammad (S.A.W).
Tazama MO tv kuona tukio hilo hapa:

Mbali na Dk. Kigwangalla, wageni wengine ni pamoja na Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Suleiman Jafo, Waziri wa zamani wa Ulinzi Profesa Juma Kapuya, Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahimu Lipumba, Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega huku kwa viongozi wa dini walikuwepo Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum na Kadhi Mkuu wa Tanzania Abdallah Mnyaa ambapo wote kwa pamoja walipewa zawadi maalum na kampuni hiyo.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na wageni mbalimbali wakati akiwasili kwenye hafla hiyo ya maulidi ya Mtume

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na wageni mbalimbali katika tukio hilo

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla akijadiliana jambo na wageni waalikwa wengine katika tukio hilo akiwemo Prof. Ibrahim Lipumba

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na wageni katika hafla hiyo ya maulidi ya Mtume

Baadhi ya vijana wa Madrasa mbalimbali kutoka Dar es Salaam na baadhi ya mikoa wakifuatiliatukio hilo

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na Naibu waziri wa Tamisemi, Mh. Suleiman Jafo wakati akiwasili kwenye hafla hiyo ya maulidi ya Mtume

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla akijadiliana jambo na Naibu waziri wa Tamisemi wakati wakiwasubiria wageni waalikwa akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi pamoja na Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohammed Gharib Bilal

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohammed Gharib Bilal wakati wa kumpokea alipowasili kwenye hafla hiyo.

dua zikiendelea

Dua zikiendelea

Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi, akizungumza katika tukio hilo


Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohammed Gharib Bilal akipokea zawadi kwenye hafla hiyo.


Dk. Kigwangalla akipokea zawadi katika hafla hiyo
Wageni mbalimbali wakifuatilia hafla hiyo ya Maulidi


Saturday, January 21, 2017

MO DEWJI ATANGAZWA KUWA MSHINDI WA TUZO YA AFRICAN LEADERSHIP MAGAZINE PERSON OF THE YEAR 2016

Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji ametangazwa na Jarida la African Leadership kuwa mshindi wa tuzo ya African Leadership Magazine Person of the year 2016 baada ya kuibuka mshindi katika kinyang'anyiro kilishohusisha watu nane.
MO Dewji ambaye ni Mtanzania anayejihusisha na biashara kupitia kampuni yake ya MeTL Group na kusaidia jamii kupitia Taasisi ya MO Dewji ameibuka mshindi kwa kupata asilimia 60.8 ya kura zote zilizopigwa akifuatiwa na Rais mstaafu wa Ghana, Dramani Mahama ambaye alipata asilimia 30.2.
Wengine waliowania tuzo hiyo ni Strive Masiyiwa, Chris Kirubi, Akinwumi Adesina, Cyril Ramaphosa, Atiku Abubakar na Aisha Mohammed.
Akizungumza kuhusu MO Dewji, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa Jarida la African Leadership, Joe Beasley amemtaja MO Dewji kama mtu ambaye anaumuhimu mkubwa kutokana na dhamira yake ya kusaidia bara la Afrika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa kutoa nafasi nyingi za kazi.
"Dhamira ya Dewji ni kutengeneza ajira jambo ambalo ni kiini cha tatizo kubwa linalokabili Afrika la ukosefu wa ajira … kupitia biashara zake amesaidia kupunguza ukosefu wa ajira, kupata utajiri na kutoa ajira kwa vijana ambao hawana ajira barani [Afrika]," alisema Beasley.
Mohammed Dewji anakuwa mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2016 ambapo kwa mwaka 2015 ilichukuliwa na Rais Mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan.

Imeandikwa na Andrew Chale

Monday, January 16, 2017

MO Dewji akanusha kuzungumza kuhusu pesa za tetemeko la ardhi Kagera

Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji amekanusha taarifa ambazo zimesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa amefanya mahojiano na kituo cha Redio cha Times FM kuhusu pesa zilizochangishwa katika Tetemeko la Ardhi la Kagera lililotokea mwezi Septemba, 2016.
Dewji amesema hajafanya mahojiano na kituo chochote cha habari kuhusu tetemeko la Kagera na habari hiyo haina ukweli wowote zaidi ni mbinu ambayo imetumiwa na baadhi ya watu kwa ajili ya kuchafua jina lake na kampuni yake ya MeTL Group ambayo mpaka sasa ina wafanyakazi zaidi ya watu 28,000.
Aidha Dewji amesema ana imani na Serikali ya awamu ya tano na kuwatoa hofu Watanzania kuwa ataendelea kushirikiana na Serikali kusaidia jamii yenye uhitaji ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya kutumia nusu ya utajiri wake kusaidia watu wenye uhitaji.
“Nitumie nafasi hii kuwajulisha Watanzania wenzangu kuwa hii habari ambayo inasambazwa na watu katika mitandao ni ya uongo na haina ukweli wowote, sijafanya mazungumzo na media yoyote na mimi nilichangia pesa kwa nia nzuri, nina imani na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa inafanya kazi kwa faida ya watu wote bila kufanya ubaguzi,” amesema Dewji.

Monday, January 2, 2017

DIWANI KAWE, Hitech WATOA MKOPO WA TREKTA, MASHINE KWA WAJASIRIAMALI

Diwani wa Kata ya Kawe, Mh. Mutta Rwakatale akimkabidhi funguo mmoja wa wajasiriamali Bwana Katala Maganga mkazi wa Kawe aliyekopeshwa  trekta kwa ajili ya shughuli zake za  ujasiliamali kutoka kwa  kampuni ya HiTECH. Wanaoshuhudia Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Maisha Finance, Bw. Deus Manyenye,  akifuatiwa na Bi. Jubilee Banda wa HiTECH na Mkurugenzi wa HiTECH International, Paul Mashauri (mwenye shati nyeupe).
Bi. Jubilee Banda wa HiTECH  akieleza kwa wanahabari namna kampuni yao inavyoweza kusaidia wananchi vifaa ikiwemo mashine za masuala mbalimbali katika shughuli za ujasiriamali na mambo mengine ya viwandani ikiwemo viwanda vya kati na vidogo. Wengine  Mtendaji Mkuu wa Maisha Finance, Bw. Deus Manyenye (kushoto) na kulia ni Mkurugenzi wa HiTECH International, Paul Mashauri
Mjasiriamali Bwana Katala Maganga mkazi wa Kawe aliyekopeshwa  trekta akiwa juu kwenye trekta hilo baada ya  kukabidhiwa.
Mtendaji Mkuu wa Maisha Finance, Bw. Deus Manyenye akielezea namna kampuni yao inavyowawezesha wajasiriamali katika kuwawezesha kimitaji. Wengine wanaoshuhudia ni pamoja na Bi. Jubilee Banda wa HiTECH na Mkurugenzi wa HiTECH International, Paul Mashauri
Diwani wa Kata ya Kawe, Mh. Mutta Rwakatale akionyesha funguo wakati wa zoezi hilo la kumkabidhi funguo mmoja wa wajasiriamali Bwana Katala Maganga mkazi wa Kawe aliyekopeshwa  trekta kwa ajili ya shughuli zake za ujasiliamali kutoka kwa  kampuni ya HiTECH. Wanaoshuhudia Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Maisha Finance, Bw. Deus Manyenye,  akifuatiwa na Bi. Jubilee Banda wa HiTECH na Mkurugenzi wa HiTECH International, Paul Mashauri (mwenye shati nyeupe).
Diwani Kawe, Hitech watoa mkopo wa trekta, mashine kwa wajasiriamali
Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Kampuni ya Hitech International kwa kushirikiana Ofisi Diwani wa Kata ya Kawe, Mutta Rwakatare, imetoa mkopo wa trekta wenye masharti nafuu ikiwa ni juhudi za kuwajengea uwezo wananchi kujiajiri na kukuza uchumi.
Hitech na ofisi ya diwani huyo zimeingia mkataba wa kuhamasisha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo kumiliki mashine za kutengeneza bidhaa za aina tofauti ili kujiajiri na kukuza kipato chao.
Akizungumza wakati wa kukabidhi trekta hilo, Mutta alisema kata yake kwa kushirikiana na sekta binafsi inatekeleza kwa vitendo ya uchumi wa viwanda kwa kuwawezesha wananchi kumiliki mashine zinazoongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha.
"Kwa udhamini wa ofisi yangu wananchi wa Kawe wanaweza kumiliki mashine waitakayo baada ya kulipa kati ya asilimia 10 mpaka 30 bila kuhitaji dhamana. Hii inasaidia kuondoa vikwazo vya kukuza mtaji vilivyopo kwenye taasisi za fedha na benki," alisema Mutta.
Kumiliki mashine kutoka Hitech, wananchi wanatakiwa kuwasiliana na ofisi ya diwani huyo ambayo itajiridhisha na makazi na uhalali wa biashara inayofanywa na mwananchi husika kabla hajatimiziwa haja za moyo wake.
Katala Mganga, mkulima wa mpunga aliyepata mkopo huo alisema anatarajia kwenda kuongeza ukubwa wa mashamba kwani gharama za kulima zitakuwa zimepungua kwa kiasi kikubwa na atapata fursa ya kuwasaidia wakulima wengine.
Kwa miaka minne aliyojikita kwenye kilimo hicho, Mganga alisema alianza na eka 10 ammbazo aliziongeza mpaka eka 60 kabla hajapata trekta hilo ambalo anaamini litasaidia kuongeza ukubwa wa shamba lake.
"Ukiwa na trekta gharama za kulima eka moja ni Sh15,000 ilhali ukikodi utatakiwa kulipa zaidi ya Sh50,000. Naishukuru ofisi ya diwani imenisaidia trekta hili," alisema.
Mkurugenzi wa kampuni ya Hitech International Tanzania, Paul Mashauri alisema kampuni hiyo ina mpango wa kutengeneza ajira milioni tatu mapaka mwaka 2020 jambo litakalofanikiwa kwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini na kati kujiajiri na kuajiri wengine.
"Endapo kila familia itakuwa inaongeza thamani ya bidhaa moja au mbili ama kutengeneza chochote na kukiuza kwa jamii inayoizunguka hili litawezekana. Tunazo mashine za aina tofauti ambazo zinawafaa watu wenye ndoto ya kumiliki kiwanda," alisema.
Alisema licha ya Kawe, mikopo ya namna hiyo inatolewa Dodoma, Mbeya na Arusha ambako tayari mafunzo yamefanyika. "Kadri siku zinavyoenda tutawafikia wananchi wengi zaidi," alisema Mashauri.
Kw amujibu wa Mashauri, trekta hilo limegharimu kiasi cha Dola 29,000 za Marekani (zaidi ya Sh58 milioni).


Thursday, December 29, 2016

Dstv yatoa zawadi ya sikukuu MO BLOG

Customer Retention Representative wa DStv,  Vida Msuya (kulia) akimkabidhi zawadi ya msimu wa Sikukuu ya ChristMas na Mwaka Mpya kwa mwandishi Mwandamizi wa mtandao wa MO BLOG, Bw. Andrew Chale katika ofisi za mtandao huo Jijini Dar es Salaam
Kampuni ya Multichoice Tanzania wasambazaji wa visambuzi vya kisasa vya DSTV mapema jana 28 Desemba 2016, wametoa zawadi ya msimu wa Sikukuu kwa wadau wao mbalimbali ikiwemo kwa mwandishi Mwandamizi wa mtandao (Blog) wa MODEWJIBLOG, Ndugu Andrew Chale.

Akikabidhi zawadi  kwa niaba ya uongozi wa kampuni hiyo ya Multichoice Tanzania,  Costomer Retention Representative,  Vida Msuya aliipongeza MO BLOG pamoja na mwanahabari huyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuitangaza vyema DSTV kwa muda wote, na zawadi hiyo ni moja ya kurudisha fadhila kwa wadau wao.

"Lengo la DSTV ni kuona tunazidi kuwa na wateja wengi ambao pia wanapata kitu bora kutoka kwetu. Huduma zetu nzuri na za kisasa hivyo kwa msimu huu wa Sikukuu wateja wetu na wadau tunawatembelea na kuwapatia zawadi." Alieleza Vida Msuya.

Aidha, DSTV pia imeweza kuwapatia wadau mbalimbali zawadi hizo za Sikuukuu na kuwatakia kheri ya Mwaka mpya wa 2017.

Aidha, kupitia  kwa Meneja Masoko wa Multichoice Tanzania, Bw. Alpha Joseph hivi karibuni amebainisha kuwa  katika msimu huu wa kusherehekea Sikukuu ya christmas na mwaka mpya wateja wao watapata kuangalia chaneli zaidi ya 70 za DStv ikiwemo mpira wa ligi ya Hispania (Laliga) na ligi ya Uingereza na zingine nyingi huku  wakishusha bei za vifurushi vyao kwa wastani wa asilimia 16, kifurushi maarufu cha DStv Bomba chenye chaneli zaidi ya 70 kikipunguzwa bei hadi sh.19,975 tu kwa mwezi.

Wednesday, December 14, 2016

WIZARA YA AFYA YAPOKEA MAGARI 58 KUSAIDIA AKINA MAMA WAJAWAZITO KANDA YA ZIWA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo amepokea magari hamsini ya kubebea wagonjwa  pamoja na magari 8 ya kuratibu shughuli za huduma za afya ya mama na mtoto yenye thamani ya shilingi   bilioni 5.9 ambayo yamekabidhiwa kwa Wabunge wa  Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Kagera, Mwanza, Mara, Simiyu, Geita na Kigoma
Waziri Ummy amelishukuru Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNFPA kwa kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania, ikiwemo vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga. 
Alizitaja changamoto zilizoonekana katika mikoa hiyo ni huduma hafifu ya rufaa kwa wanawake wajawazito kwa kukosa magari ya kubebea wagonjwa, ukosefu wa damu salama, ushiriki mdogo wa jamii katika mambo yanayohusu afya ya mama ikiwemo kutotambua dalili hatari za wakati wa ujauzito pamoja na baadhi ya watumishi wasiokuwa na stadi za kuokoa maisha ambayo yanachangia wingi wa vifo vitokanavyo na uzazi
Tafiti zilizofanyika mwaka 2010 na tathmini iliyofanyika mwaka 2015 wakati wa kuandaa mpango kazi wa matokeo makubwa sasa, Mikoa ya Kanda ya Ziwa  ikiwemo Kigoma ilionekana kuwa na viashiria hafifu vya afya ya mama na mtoto kwa mfano; utumiaji mdogo wa uzazi wa mpango, wanawake wachache wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya pamoja na vifo vingi vitokanavyo na uzazi.
Wizara ya Afya imekua ikifanya  jitihada mbalimbali katika kukabiliana na tatizo hilo ambapo kwa awamu hii ya tano  tumetengeneza mpango mmoja utakaohusika na masuala ya uzazi wa afya ya mama na watoto na vijana ambapo ndani ya miaka minne hadi kufikia mwaka 2020 tuwe tumepunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka 432 hadi 292 kutoka kila kizazi hai laki moja na kwa upande wa watoto chini ya miaka mitano Tanzania imefanikiwa kufikia lengo namba nne la malengo ya maendeleo ya milenia kwa  kupunguza vifo kutoka 50 hadi 40 katika vizazi hai 1,000.
Aidha Waziri Ummy amewataka Wabunge, Wakurugenzi na Waganga Wakuu wa Wilaya kuyatumia magari hayo ipasavyo yaani, kwa shughuli iliyokusudiwa, vilevile kuyakatia bima ya ajali pamoja na kuiomba jamii, Taasisi zisizo za kiserikali kuunganisha nguvu kwani vifo vitokananyo na uzazi vinazuilika.

IMETOLEWA NA

Nsachris Mwamwaja
MKUU WA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI-AFYA
14/12/2016





Kijiweni (nipe 5)