Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo amepokea magari hamsini ya kubebea wagonjwa pamoja na magari 8 ya kuratibu shughuli za huduma za afya ya mama na mtoto yenye thamani ya shilingi bilioni 5.9 ambayo yamekabidhiwa kwa Wabunge wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Kagera, Mwanza, Mara, Simiyu, Geita na Kigoma
Waziri Ummy amelishukuru Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNFPA kwa kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania, ikiwemo vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.
Alizitaja changamoto zilizoonekana katika mikoa hiyo ni huduma hafifu ya rufaa kwa wanawake wajawazito kwa kukosa magari ya kubebea wagonjwa, ukosefu wa damu salama, ushiriki mdogo wa jamii katika mambo yanayohusu afya ya mama ikiwemo kutotambua dalili hatari za wakati wa ujauzito pamoja na baadhi ya watumishi wasiokuwa na stadi za kuokoa maisha ambayo yanachangia wingi wa vifo vitokanavyo na uzazi
Tafiti zilizofanyika mwaka 2010 na tathmini iliyofanyika mwaka 2015 wakati wa kuandaa mpango kazi wa matokeo makubwa sasa, Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Kigoma ilionekana kuwa na viashiria hafifu vya afya ya mama na mtoto kwa mfano; utumiaji mdogo wa uzazi wa mpango, wanawake wachache wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya pamoja na vifo vingi vitokanavyo na uzazi.
Wizara ya Afya imekua ikifanya jitihada mbalimbali katika kukabiliana na tatizo hilo ambapo kwa awamu hii ya tano tumetengeneza mpango mmoja utakaohusika na masuala ya uzazi wa afya ya mama na watoto na vijana ambapo ndani ya miaka minne hadi kufikia mwaka 2020 tuwe tumepunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka 432 hadi 292 kutoka kila kizazi hai laki moja na kwa upande wa watoto chini ya miaka mitano Tanzania imefanikiwa kufikia lengo namba nne la malengo ya maendeleo ya milenia kwa kupunguza vifo kutoka 50 hadi 40 katika vizazi hai 1,000.
Aidha Waziri Ummy amewataka Wabunge, Wakurugenzi na Waganga Wakuu wa Wilaya kuyatumia magari hayo ipasavyo yaani, kwa shughuli iliyokusudiwa, vilevile kuyakatia bima ya ajali pamoja na kuiomba jamii, Taasisi zisizo za kiserikali kuunganisha nguvu kwani vifo vitokananyo na uzazi vinazuilika.
IMETOLEWA NA
Nsachris Mwamwaja
MKUU WA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI-AFYA
14/12/2016
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa