Translate in your language

Thursday, December 29, 2016

Dstv yatoa zawadi ya sikukuu MO BLOG

Customer Retention Representative wa DStv,  Vida Msuya (kulia) akimkabidhi zawadi ya msimu wa Sikukuu ya ChristMas na Mwaka Mpya kwa mwandishi Mwandamizi wa mtandao wa MO BLOG, Bw. Andrew Chale katika ofisi za mtandao huo Jijini Dar es Salaam
Kampuni ya Multichoice Tanzania wasambazaji wa visambuzi vya kisasa vya DSTV mapema jana 28 Desemba 2016, wametoa zawadi ya msimu wa Sikukuu kwa wadau wao mbalimbali ikiwemo kwa mwandishi Mwandamizi wa mtandao (Blog) wa MODEWJIBLOG, Ndugu Andrew Chale.

Akikabidhi zawadi  kwa niaba ya uongozi wa kampuni hiyo ya Multichoice Tanzania,  Costomer Retention Representative,  Vida Msuya aliipongeza MO BLOG pamoja na mwanahabari huyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuitangaza vyema DSTV kwa muda wote, na zawadi hiyo ni moja ya kurudisha fadhila kwa wadau wao.

"Lengo la DSTV ni kuona tunazidi kuwa na wateja wengi ambao pia wanapata kitu bora kutoka kwetu. Huduma zetu nzuri na za kisasa hivyo kwa msimu huu wa Sikukuu wateja wetu na wadau tunawatembelea na kuwapatia zawadi." Alieleza Vida Msuya.

Aidha, DSTV pia imeweza kuwapatia wadau mbalimbali zawadi hizo za Sikuukuu na kuwatakia kheri ya Mwaka mpya wa 2017.

Aidha, kupitia  kwa Meneja Masoko wa Multichoice Tanzania, Bw. Alpha Joseph hivi karibuni amebainisha kuwa  katika msimu huu wa kusherehekea Sikukuu ya christmas na mwaka mpya wateja wao watapata kuangalia chaneli zaidi ya 70 za DStv ikiwemo mpira wa ligi ya Hispania (Laliga) na ligi ya Uingereza na zingine nyingi huku  wakishusha bei za vifurushi vyao kwa wastani wa asilimia 16, kifurushi maarufu cha DStv Bomba chenye chaneli zaidi ya 70 kikipunguzwa bei hadi sh.19,975 tu kwa mwezi.

Wednesday, December 14, 2016

WIZARA YA AFYA YAPOKEA MAGARI 58 KUSAIDIA AKINA MAMA WAJAWAZITO KANDA YA ZIWA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo amepokea magari hamsini ya kubebea wagonjwa  pamoja na magari 8 ya kuratibu shughuli za huduma za afya ya mama na mtoto yenye thamani ya shilingi   bilioni 5.9 ambayo yamekabidhiwa kwa Wabunge wa  Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Kagera, Mwanza, Mara, Simiyu, Geita na Kigoma
Waziri Ummy amelishukuru Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNFPA kwa kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania, ikiwemo vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga. 
Alizitaja changamoto zilizoonekana katika mikoa hiyo ni huduma hafifu ya rufaa kwa wanawake wajawazito kwa kukosa magari ya kubebea wagonjwa, ukosefu wa damu salama, ushiriki mdogo wa jamii katika mambo yanayohusu afya ya mama ikiwemo kutotambua dalili hatari za wakati wa ujauzito pamoja na baadhi ya watumishi wasiokuwa na stadi za kuokoa maisha ambayo yanachangia wingi wa vifo vitokanavyo na uzazi
Tafiti zilizofanyika mwaka 2010 na tathmini iliyofanyika mwaka 2015 wakati wa kuandaa mpango kazi wa matokeo makubwa sasa, Mikoa ya Kanda ya Ziwa  ikiwemo Kigoma ilionekana kuwa na viashiria hafifu vya afya ya mama na mtoto kwa mfano; utumiaji mdogo wa uzazi wa mpango, wanawake wachache wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya pamoja na vifo vingi vitokanavyo na uzazi.
Wizara ya Afya imekua ikifanya  jitihada mbalimbali katika kukabiliana na tatizo hilo ambapo kwa awamu hii ya tano  tumetengeneza mpango mmoja utakaohusika na masuala ya uzazi wa afya ya mama na watoto na vijana ambapo ndani ya miaka minne hadi kufikia mwaka 2020 tuwe tumepunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka 432 hadi 292 kutoka kila kizazi hai laki moja na kwa upande wa watoto chini ya miaka mitano Tanzania imefanikiwa kufikia lengo namba nne la malengo ya maendeleo ya milenia kwa  kupunguza vifo kutoka 50 hadi 40 katika vizazi hai 1,000.
Aidha Waziri Ummy amewataka Wabunge, Wakurugenzi na Waganga Wakuu wa Wilaya kuyatumia magari hayo ipasavyo yaani, kwa shughuli iliyokusudiwa, vilevile kuyakatia bima ya ajali pamoja na kuiomba jamii, Taasisi zisizo za kiserikali kuunganisha nguvu kwani vifo vitokananyo na uzazi vinazuilika.

IMETOLEWA NA

Nsachris Mwamwaja
MKUU WA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI-AFYA
14/12/2016





Kijiweni (nipe 5)