▼
Friday, August 3, 2012
MJANE AMUOMBA IGP MWEMA AMPE ULINZI
Na. Bernard James, Dar es Salaam
SIKU mbili baada ya kukamatwa mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za mauaji ya Onesphory Kituly, mjane wa marahemu, Mary Kituly amemwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema kumhakikishia usalama wake.
“Ombi langu kwa sasa ni moja tu, IGP anisaidie kwa hali na mali juu ya usalama wangu. Hao watu ni hatari. Wana mtandao mkubwa,” alilalamika Kituly huku akitokwa machozi.
Aliongeza: “Mazingira ya mauaji ya mume wangu ni ya kutisha. Niliona dalili tangu siku nyingi kwa hiyo nina kila sababu ya kuhofia usalama wangu.”
Kabla ya kuuawa, marehemu Kituly (54), alikuwa akiwashtaki mfanyabiashara huyo anayeshikiliwa polisi Mkoa wa Kinondoni pamoja na wafanyabiashara wengine wawili, kwa madai ya kumdhulumu nyumba ya zaidi ya Sh600milioni.
Alidai Oktoba mwaka jana, mtu asiyejulikana alimmiminia marehemu Kituly risasi tano kifuani, tumboni na mdomoni wakati marehemu akijiandaa kuingiza gari lake katika uzio wa nyumba yake Magomeni Mapipa, Dar es Salaam.
Ndugu wa marehemu wanaamini muuaji huyo ambaye hakuchukua kitu chochote kutoka kwa marehemu alikodiwa kutekeleze mauaji hayo.
Inadaiwa muuaji alitumia muda mwingi kuvinjari katika maeneo alipoishi marehemu na alipata mwanya wa kutekeleza mauaji pale marehemu alipotoka nje kuingiza gari.
Muuaji alimsogelea Kituly na kuegemea mlango wa gari na kisha kummiminia risasi.
Polisi wanasema mauaji hayo yanaweza kutekelezwa na watu au mtu ambaye marehemu alimdai ili kuepusha usumbufu au yametokana na kutokuelewana kibiashara.
Siku moja baada ya tukio, shahidi mmoja aliiambia Mwananchi kuwa alimfuatilia muuaji kutoka Magomeni hadi eneo la Shekilango karibu na Chuo cha Ustawi wa Jamii, lakini hakuweza kumkamata baada ya kukosa msaada wa polisi.
Alidai walimfuatilia muuaji na kupanda naye daladala Kituo cha Magomeni Mapipa na alishuka na kumuacha kwenye daladala na kukimbia kuomba msaada wa kumkamata, lakini polisi walimtaka asubiri gari.
Polisi walipinga vikali tuhuma hizo na kuziita maneno ya mitaani yaliyohitaji uthibitisho wa kutosha.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela aliahidi kuzifanyia kazi taarifa hizo akisema “nia yetu ni kufanikisha kumkamata muuaji na kumleta kwenye mkono wa sheria.”
Juzi, takriban miezi kumi baaada ya mauaji, kamanda Kenyela amekaririwa na gazeti moja akisema polisi wanamshikilia mfanyabiashara maarufu Kituo cha Polisi Magomeni kuhusiana na mauaji hayo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa