Monday, April 23, 2012

MAWAZIRI WALIPUANA


Wabunge wakiendelea na kikao cha Bunge mjini Dodoma hivi karibuni
NI NUNDU NA MFUTAKAMBA, NYALANDU NA CHAMI, IKULU YASEMA RAIS HAPUUZI TUHUMA, WABUNGE WATAKA BUNGE LA DHARURA
Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu ametuhumu Naibu wake Athuman Mfutakamba akisema ndiye mhusika mkuu wa tuhuma za ufisadi zilizoelekezwa kwake kiasi cha wabunge kufikia hatua ya kumshinikiza ajiuzulu.

Mbali ya mawaziri hao, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu ametoa waraka unaombebesha mzigo Waziri wake, Dk Cyril Chami akisema alimpa ushauri wa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege kupisha uchunguzi, lakini hakutekeleza.

Nundu na Mfutakamba
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa jana, Waziri Nundu alisema Mfutakamba amekuwa akishinikiza Kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC), ipewe kazi ya kujenga gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa
ilimgharamia safari kadhaa kwenda nje.

Waziri Nundu pia alishangazwa na shinikizo la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wake, Peter Serukamba nayo kushinikiza CCCC ipewe kazi hiyo akihoji, “Kuna nini?”

“CCCC walinipa mwaliko nikaangalie miradi yao mingine wanayofanya nikakataa na walipoona nimekataa wakamfuata Naibu wangu, wakampeleka China wakamlipia gharama zote akaenda yeye na msaidizi wake tu, bila kibali changu,” alisema na kuongeza:

“Waliporejea nikamwuliza wamekwendaje huko bila kibali change? Akasema eti wakati wanaondoka mimi nilikuwa sipo, kwa hiyo kibali amepata ofisi nyingine lakini hizo tarehe alizodai sikuwepo mimi nilikuwepo ofisini.”


Waziri Nundu alisema, kampuni hiyohiyo ilimpeleka tena Naibu wake Mauritania na Equatorial Guinea na kumgharamia kila kitu na aliporejea nchini ndipo alipoandika ripoti akishinikiza ipewe kazi hiyo.

“Naibu wangu alipoanza kupelekwa huko nje na CCCC tena kwa kugharamiwa kila kitu ndipo matatizo yalipoanza…, mtu niliyefanya naye kwa ukaribu, matatizo yakaanzia hapo mpaka nikajiuliza kuna nini hapa kati ya naibu wangu na hii CCCC?”

Alifafanua kuwa walipotaka kuanzisha mradi wa upanuzi wa bandari hiyo kwa kujenga Gati namba 13 na 14, ilijitokeza kampuni ya CCCC ambayo ni mjenzi na si mwekezaji wala mkopeshaji na kudai itafanya upembuzi yakinifu wa mradi kwa gharama zake.

“Alivyotafutwa haijulikani mpaka leo…, aliingia mkataba gani na TPA (Mamlaka ya Bandari Tanzania) mimi sijui…, huo mkataba ulisema atafanya nini na nini hakuna hadi leo lakini, nashinikizwa tu ooh hiyo CCCC ndiyo ifanye kazi hiyo… mimi nashangaa!”

Alisema baada ya kufanya upembuzi huo yakinifu, CCCC ilibainisha kuwa gharama za mradi huo ni Sh542 bilioni na kusema ingeitafutia TPA mkopo wa fedha kutoka Exim Bank ya China lakini, tangu mwaka 2008 hadi sasa hakuna mkopo wowote uliopatikana.

Waziri Nundu alisema kwa kuwa yalikuwa yamejitokeza makampuni 11 ambayo ni wakopeshaji na wawekezaji, alishauri kampuni hizo zishindanishwe ili ipatikane moja itakayofanyakazi hiyo na ushauri huo ndiyo ulioanza kumletea maadui wengi ndani ya TPA na wizarani.

Alisema miongoni mwa kampuni hizo, ipo ya China Merchant ambayo ilisema ingejenga kwa Sh300 bilioni lakini bado shinikizo likawa ipewe CCCC kwa Sh542 bilioni.

“Tulipofikia hatua sasa ya kutangaza ili makampuni yashindane ndipo kulipoanza kujitokeza msukumo kutoka TPA kuwa kazi hiyo isitangazwe, bali apewe CCCC na kuhoji” Yaani CCCCndiyo afanye upembuzi na yeye ajenge, atutafutie mkopo?”

Alisema kuna wakati alitaka kuingizwa mkenge katika mradi wa ujenzi wa maegesho ya magari bandarini, lakini akasema anamshukuru Mungu kuwa alimsaidia kwani aliushtukia na tayari Rais Jakaya Kikwete alishaamuru ufutwe na usiwepo.

Kuhusu hoja ya kujiuzulu, Waziri Nundu alisema:”Najiuliza kwa kosa gani? Kama kuna jambo lolote la ufisadi halinihusu …, Wizara yangu inaendeshwa kwa maadili na nikigundua kuna mtu amehongwa nitasimamisha mradi huo mara moja,” alisema.

Waziri Nundu alisema hajaambiwa na mtu yeyote ajiuzulu… “Inawezekana ukaambiwa utafakari kujiuzulu na hiyo, haina maana umeambiwa ujiuzulu.” Alisema itambidi atafakari zaidi na kusisitiza kuwa hana shida na uwaziri, bali aliomba ubunge.

Akijibu madai ya Waziri wake, jana Mfutakamba alikiri kusafirishwa na kampuni hiyo lakini akasema ilifuata taratibu zote za kiserikali… “Nimesafiri kwenye maeneo hayo uliyosema… CCCC ilitoa mwaliko na mimi nilifuata taratibu zote na kanuni za kiongozi kusafiri kwa kuomba ruhusa kwa mamlaka husika kwa vile niliona ni safari yenye manufaa kwa nchi na mamlaka ilinipa ruhusa.”

Alisema katika safari hiyo alitembelea miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa reli na magati na aliporudi aliieleza Serikali uwezo wa kampuni ya CCCC na kwamba kampuni ya China Merchant si wajenzi, bali ni waendeshaji tu wa ndege.

Alikanusha kuwa na maslahi yoyote na kampuni hiyo na kusisitiza kuwa kibali cha kwenda katika safari hizo zilizogharamiwa na CCCC alipewa na Waziri Mkuu na hakitolewi na waziri wake.

Chami na Nyalandu
Nyalandu naye ameonakana kumtwisha mzigo wa Ekelege akisema alimshauri Waziri wake, Dk Chami kumsimamisha kazi ili achunguzwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Katika barua ya Nyalandu ya Februari 10, mwaka huu kwenda kwa Cham,i alimweleza kuwa wabunge walikuwa wanashuku kuwa mkurugenzi huyo alitoa taarifa zisizo sahihi.

“Kikao cha briefing cha CAG na waheshimiwa wabunge, TBS imeshutumiwa kuhusiana na ukaguzi wa magari nje ya nchi na mchakato wote unaohusiana na suala hilo,” inasomeka dokezo hilo la Nyalandu.

Alisema wabunge walioshiki katika ziara ya nchi za Hong Kong na Singapore wametoa madai kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS aliwadanganya juu ya kampuni zinazofanya ukaguzi wa magari na bidhaa nyingine nje ya nchi na wakatoa madai kuwa, TBS imetoa taarifa tofauti na yale waliyoyaona katika ziara.

“Wabunge wameoa mapendekezo ya kuomba wizara imsimamishe kazi kwa muda Mkurugenzi wa Mkuu wa TBS ili kupisha uchunguzi wa CAG juu ya tuhuma hizo,” inasema sehemu ya barua hiyo na kuongeza:

“Kutokana na unyeti wa TBS na tuhuma zilizotolewa, nashauri uangalie uwezekano wa kumsimamisha kazi kwa muda Mkurugenzi wa TBS ili apishe uchunguzi huo wa CAG na endapo hatakuwa na tuhuma za kujibu, basi arudishwe kazini mara moja.”

Dk Chami alikiri kupokea ushauri huo lakini, akasema wakati anautoa kulikuwa hakuna tuhuma zozote za kamati kuhusu Ekelege.

“Ushauri ulikuwa mzuri lakini, Ekelege ni mteule wa Rais hivyo huwezi kwenda kwa Rais kumtaka amwondoe wakati hakuna taarifa yoyote inayoonyesha tuhuma zake. Kuna njia mbili za kumsimamisha kwanza, kumshauri Rais na hizo ripoti dhidi ya Ekelege zipelekwe kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya TBS na baada ya hapo wakitoa maazimio ndiyo waziri anaweza kwenda nayo kwa Rais,” alisema Dk Chami.

Alisema kukosekana kwa ripoti iliyomchunguza Ekelege inamfanya akose nguvu ya kumshauri Rais.

Wabunge wataka Bunge la dharura
Licha ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kupinga hoja ya wabunge ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu akisema ni batili, baadhi ya wabunge wamesema kwamba leo watawasilisha orodha yao kwake kutaka Kikao cha Bunge la dharura ndani ya siku 14 kuanzia leo.

Wakizungumza jana na waandishi wa habari katika Ofisi ya Kambi ya Upinzani, wabunge hao walisema kitendo cha Spika kufikiria kuwa anaweza kuuzima moto wao, hakitasaidia kitu na badala yake kinazidi kuchochea ari na msukumo wao.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alisema kama Spika hatakubaliana na ombi lao, watakuwa tayari kurudi kwa wananchi na kukusanya maoni ya zaidi ya watu milioni moja.

Zitto alisema hadi jana jioni, wabunge 73 wakiwemo watano kutoka CCM, walikuwa wameweka sahihi za kutokuwa na imani na Waziri Mkuu na kwamba wabunge wengi zaidi walikuwa njiani kuelekea Dodoma kwa ajili ya kuweka sahihi.

“Hadi sasa ni chama kimoja tu kati ya sita vyenye uwakilishi bungeni ndicho kilichogoma kuweka sahihi. ni UDP na Mzee (John) Cheyo hajatuambia sababu, lakini vyama vyote vitano wabunge wao wameweka sahihi na watano kati yao wanatoka CCM,’’ alisema.

Zitto alisema mkakati huo wameuita 'Operesheni Uwajibikaji' na wameamua kupambana hadi kuhakikisha  wanashinda huku wakijiita kuwa ni wabunge wazalendo bila ya kujali itikadi za vyama vyao.

Alisema kiini cha makakati huo ni mfumo mbovu ndani ya Serikali ambao hauruhusu watu kuwajibika na badala yake kuendelea kufuja fedha za wananchi.

Katibu wa wabunge wa CUF, Magdalena Sakaya alisema uongozi wa chama hicho uliwaagiza wabunge wake wote kusaini karatasi hiyo.

Alisema Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba aliwaagiza wabunge wake kusaini kwa kile alichokiita ni maslahi ya nchi na kuwa wasiposaini watakuwa ni wasaliti wa maslahi ya nchi yao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alisema chama chao hakikuona tabu kusaini majina hayo na akazungumzia umuhimu wa mpango huo kuwa ni kulifanya Bunge kutokuwa kichwa cha mwendawazimu.

Wakati kukiwa na shinikizo hilo, taarifa zisizo rasmi zinasema Rais Kikwete amekataa kujiuzulu kwa mawaziri hao akisema kama ni matatizo kwenye halmashauri au mashirika wanaopaswa kuwaibika ni watendaji wa taasisi hizo.

Ikulu: Rais hapuuzi tuhuma
Akizungumzia shinikizo hilo la Wabunge, Balozi Sefue alisema baada ya wabunge kutoa tuhuma hizo ni wakati wa Serikali nayo kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria.

Balozi Sefue ambaye ndiye mamlaka ya nidhamu katika utumishi wa umma, alisema wabunge hawakutoa tuhuma hizo kisiasa kwani karibu zote walizipata kutoka kwenye ripoti ya CAG ambaye ni sehemu ya Serikali, hivyo wao hawawezi kuzipuuza.

“Mimi ni mamlaka ya nidhamu katika utumishi wa umma, ninachoweza kusema ni kwamba sasa hivi taarifa zote zinazohusu tuhuma za rushwa au ufujaji wa fedha za umma tunazichambua. Watakaopaswa kuwajibishwa tutawawajibisha na watakaokutwa na makosa ya jinai watapelekwa mahakamani,” alisema.

Alisema wabunge walichofanya ni kutekeleza majukumu yao ya kikatiba na Serikali inachofanya ni kuchambua kwa kina kila tuhuma ili kuona ni hatua gani zinapaswa kuchukuliwa kwa kila mhusika.

Kuhusu hatima ya mawaziri hao, alisema ingawa jukumu hilo haliko mikononi mwake, anaamini Rais hatapuuzia tuhuma zozote zitakazobainika kuwa ni za kweli.

Dk Slaa
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa amesema kama Rais Kikwete angesikiliza ushauri wake wa kuvunja Baraza lake la Mawaziri, alioutoa mapema mwaka huu, hayo yanayotokea sasa bungeni ya kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, yasingekuwapo.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Sahara, Mwanza, Dk Slaa alisema uozo wa Serikali unatokana na baadhi ya mawaziri kufanya ubadhirifu bila ya kuchukuliwa hatua muda mrefu.

Alisema hakuna mtu mwingine wa kulaumiwa kwa kushamiri kwa ubadhirifu serikalini, bali Rais mwenyewe kwa kuwa ameshindwa kulivunja mara moja.

Imendikwa na Daniel Mjema, Habel Chidawali, Dodoma; Frederick Katulanda, Mwanza na Ramadhan Semtawa, Dar

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa