Thursday, March 8, 2012

WAMBURA AFINGIWA MILELE KUONGOZA SOKA


ELECTIONS COMMITTEE

TAARIFA KWA VYOMBO YA HABARI
06 MACHI 2012


UFAFANUZI KUHUSU MAJUKUMU, WAJIBU NA MAMLAKA YA KAMATI YA UCHAGUZI NA
MAELEZO YA KINA KUHUSU MAAMUZI YA KAMATI ZA UCHAGUZI ZA TFF KUHUSU MAOMBI
YA NDG. MICHAEL RICHARD WAMBURA KUGOMBEA UONGOZI KWENYE UCHAGUZI WA
TFF 2008, UCHAGUZI WA KLABU YA SIMBA 2010 NA FAM 2011.


1. USIMAMIZI WA CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF

Muundo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umeelezwa wazi kwenye Katiba ya TFF Ibara ya 18. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni moja kati ya vyombo sita vilivyoainishwa katika Muundo wa TFF. Majukumu, wajibu na mamlaka ya vyombo vya TFF yameainishwa katika Katiba ya TFF na Kanuni zilizotungwa na kuidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuzingatia Ibara ya 34 ya Katiba hiyo.

Majukumu, wajibu na mamlaka ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF yameainishwa kwenye Katiba ya TFF Ibara ya 49 na kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Mbali na majukumu na wajibu wa kusimamia uchaguzi wa TFF na chaguzi za wanachama wake na kuishauri Kamati ya Utendaji ya TFF kuhusu Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Uchaguzi ya TFF inao wajibu wa kulinda Katiba na Kanuni za uchaguzi za TFF na Katiba ya FIFA na Katiba za wanachama wa TFF kama ilivyotamkwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 6 na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26. Uchaguzi Mkuu wa TFF hufanyika kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa TFF. Chaguzi za wanachama wa TFF na wanachama wao hufanyika kwa mujibu wa Kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF na si vinginevyo. Kanuni hizi zimeainisha taratibu mbalimbali ambazo lazima zizingatiwe kikamilifu, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa ukataji rufaa katika ngazi mbalimbali za uchaguzi. Vyombo na Kamati zote za TFF, Wanachama wote wa TFF na wanachama wao, na wadau wote wa soka wanao wajibu wa kuheshimu Kanuni mbali mbali za TFF ambazo ni pamoja na Kanuni za Uchaguzi.

2. MAAMUZI KUHUSU MAOMBI YA UONGOZI YA NDG. MICHAEL WAMBURA

Kwa muda mrefu pamekuwepo na taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari zenye lengo la kuwafanya wadau na wapenzi wa soka na umma wa watanzania kwa ujumla kuaminishwa kuwa Ndg. Michael Wambura huonewa na vyombo vya TFF vinavyosimamia uchaguzi kila anapoomba nafasi za uongozi katika TFF. Baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya wapenzi wa soka wamesikika wakisema kwamba kuenguliwa kwa Ndg. Michael Wambura kugombea uomgozi ni kutokana na kuogopwa na viongozi wa TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inapenda kufafanua kwa kina maamuzi yote yaliyofanyika kuhusu maombi yote ya uongozi ya Ndg. Michael Wambura na kuweka wazi vielelezo vilivyotumika kufikia maamuzi hayo ili umma wa watanzania wafahamu kinagaubaga ukweli kuhusu maamuzi hayo:

UCHAGUZI MKUU WA TFF 2008

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilimwengua Ndg. Michael Wambura kugombea nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa TFF kwa kutokidhi matakwa ya uadilifu kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF. Ndg. Michael Wambura hakuridhika na uamuzi huo na alikata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya TFF. Hata hivyo baada ya Kamati ya Rufaa kupitia nyaraka mbali mbali zilizowasilishwa kwenye Kamati hiyo ikiwa ni pamoja na ripoti ya ukaguzi wa maheabu ya TFF/FAT kwa mwaka 2002, 2003 na 2004 rufaa yake ilishindwa baada ya Kamati ya Rufaa kuridhika na kuweka bayana kuwa mwomba rufaa, Michael Richard Wambura aliipa Zabuni kampuni yake iitwayo Min Investments & Commercial Services Co. wakati akiwa Katibu Mkuu wa FAT/TFF na hivyo kushindwa kukudhi kigezo cha uadilifu. Katika kufikia maamuzi yake, Kamati ya rufaa pia ilibaini kuwa Ndg. Michael Richard Wambura alionyesha kuwa alikuwa amechana na umiliki wa kampuni hiyo kuanzia tarehe 12 Novemba 2003 kwa mabadiliko yaliyotekelezwa tarehe 28 Februari 2007 kwa malipo ya Shs. 34,500/= ya “exchequer receipt No. 28173444’. Hata hivyo, Kamati ya Rufaa iliridhika kuwa utekelezaji wa mabadiliko ya umiliki wa kampuni hiyo ulichukua takribani miezi arobaini (40). Baada ya majadiliano ambayo yalikuwa yamekitwa (pegged) kwenye uadilifu (integrity), Kamati ya Rufaa iliridhika kuwa taswira inayojitokeza kwenye muktadha imegubikwa na wingu jeusi la mashaka kuhusu “integrity” ya Muomba Rufaa (Ndg. Michael Richard Wambura).

Uthibitisho kwamba mmilki wa Kampuni ya Min Investments & Commercial Services Co ni Ndg. Michael Richard Wambura ulitolewa na Msajili wa Makampuni (Business Registration and Licensing Agency-BRELA) kwa barua yenye Kumbukumbu Na. MITM/RBN/93017 ya tarehe 16 Agosti 2006. Kampuni hiyo ilisajiliwa tarehe 17 Julai 1992.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF inatoa sehemu ndogo tu ya ubadhirifu uliokuwa unafanywa kwa kutumia Kampuni hiyo (Min Investments & Commercial Services Co) ya Michael Wambura kinyume na utaratibu wa utoaji tenda wa FAT/TFF na malipo aliyojilipa bila maelezo yoyote kama ilivyoainishwa kwenye Ripoti ya Ukaguzi wa Mahesabu iliyowasilishwa na wakaguzi tarehe 19 Septemba 2005 na Ripoti maalumu ya ukaguzi iliyowasilishwa Novemba 2006, kama ifuatavyo:

(i) Tarehe 28 Julai 2004 Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa TFF alilipwa Dola za Kimarekani 16,548.00 (US$ 16,548 sawa na Tshs. 17,170,040 wakati huo) kwa ununuzi wa samani (furniture) za Hosteli ya TFF. Pesa hizo zilizoombwa kulipwa kwa Michael Wambura zimeonyeshwa kwenye fomu ya malipo ya TFF ya tarehe 28 Julai 2004. Pesa hizo zilipokelewa na Kampuni ya Min Investments & Commercial Services Co na kuthibitisha kupokelewa na kampuni hiyo kwa risiti Na. 020 ya tarehe 21 Julai 2004 ya kampuni hiyo, ingawa hapakuwa na maombi ya manunuzi (order) iliyokuwa imefanywa na TFF kwa kampuni hiyo.

(ii) Baada ya kujilipa pesa zilizotajwa hapo juu, kesho yake tarehe 29 Julai 2004 Ndg. Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa TFF alijilipa Dola za kimarekani 25,000.00 (US$ 25,000.00 sawa na Tshs. 25,937,500 wakati huo), kama ilivyoonyeshwa kwenye vocha ya malipo ya TFF Na. 5324 ya tarehe tajwa hapo juu, ikionyesha kuwa ni kwa ajili ya malipo ya samani za Hosteli (US$ 15,000.00) na malipo ya awali ya Gari (US$ 10,000.00). Ndg. Michael Wambura alithibitisha kupokea malipo hayo. Ripoti ya Ukaguzi inabainisha wazi kuwa vifaa vichache vilivyonuliwa kwa hosteli ya TFF thamani yake haikuainishwa na hapakuwa na gari lililolipiwa malipo ya awali katika vitabu vya mahesabu ya TFF.

(iii) Katika kipindi cha mwaka 2002 Ndg. Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT alijikopesha jumla ya Tshs. 36,850,750 bila idhini ya Kamati ya Utendaji.

(iv) Tarehe 20 Mei 2002 Ndg. Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT alijilipa Tshs. 12,147,837 ambazo hazina maelezo yoyote.

(v) Imebainishwa wazi kuwa FAT/TFF ilikuwa mfilisi katika kipindi cha 2002-2004 (Nukuu: “The Association was actually insolvent during the period.”)

Kamati inaweka wazi tena kwamba maamuzi yaliyofikiwa na Kamati ya Rufaa ya kumuengua Michael Wambura kwenye uchaguzi Mkuu wa TFF yanaweza tu kubadilishwa na Mahakama ya usuluhishi wa masuala ya michezo (CAS) endapo Michael Wambura atakata rufaa CAS kupinga maamuzi hayo na kushinda rufaa, na si vinginevyo.

MAAMUZI YA MKUTANO MKUU WA TFF 2007

Mkutano Mkuu wa TFF ambacho ndicho chombo cha juu kabisa cha TFF (Supreme Authority of TFF) katika kikao chake mwaka 2007 kilipitia ripoti za ukaguzi wa mahesabu ya FAT/TFF kwa kipindi cha mwaka 2002 hadi 2004 na baada ya kujiridhisha kuhusu ubadhirifu uliofanywa na Ndg. Michael Wambura, Mkutano Muu wa TFF uliamua kwamba Ndg. Michael Wambura afikishwe kwenye vyombo vya dola kwa ubadhirifu wa fedha za FAT/TFF alioufanya kama ilivyoainishwa kwenye ripoti za ukaguzi wa Mahesabu. Sekretarieti ya TFF mwaka 2007 ikitekeleza maagizo ya Mkutano Mkuu wa TFF na suala hilo lilpelekwa Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi ilithibitisha maombi ya TFF kwa barua yake ya tarehe 18 Januari 2008 na kumfungulia jalada Ndg Michael Wambura kwa kosa la wizi akiwa Mtumishi. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaheshimu maamuzi ya Mkutano Mkuu wa TFF na hadi sasa haijataarifiwa kwa maandishi na chombo chochote kama suala hilo limefikia ukomo wa aina yoyote.

UCHAGUZI WA KLABU YA SIMBA MWAKA 2010

Ndg. Michael Richard Wambura aliomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba. Hata hivyo alikatiwa rufaa na Ndg. Daniel T. Kamna kwa kutotimiza matakwa ya Ibara ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF kama ilivyoamuliwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na pia Kamati ya Rufaa ya TFF mwaka 2008 wakati alipoomba kugombea nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa TFF. Kamati ilikubaliana na maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi na Kamati ya Rufaa ya TFF mwaka 2008 kwamba Bw. Michael R. Wambura si mwadilifu kama ilivyonyeshwa kwenye aya ya 2.1 na 2.2 hapo juu na hivyo hakukidhi matakwa ya Ibara ya 29(7) ya Katiba ya TFF na Ibara ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kamati ilimuondoa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Simba SC.

Baada ya maamuzi hayo ya Kamati, Ndg. Michael Richard Wambura alikwenda Mahakamani na akafungua kesi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam dhidi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba kuzuia uchaguzi wa klabu ya Simba usifanyike. Kwa kufanya hivyo alivunja Katiba ya Klabu ya Simba na kukiuka Katiba ya TFF Ibara ya 12(2) (e) na Katiba ya FIFA Ibara ya 64(2). Klabu ya Simba ilichukua hatua za kikatiba, na katika kikao chake cha 5/5/2010, ilimsimamisha uanachama Ndg. Wambura kwa kukiuka katiba ya klabu hiyo. Klabu ya Simba iliitaarifu TFF uamuzi huo kwa barua yenye Kumbukumbu Na. SSC/MMKT/162/Vol.40/10 ya tarehe 06 Mei 2010 iliyoambatanishwa na Muhtasari wa kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanya uamuzi huo. Uamuzi wa kumrudishia uanachama unafanywa na Mkutano Mkuu wa Klabu ya Simba. TFF haijapokea taarifa yoyote kutoka Klabu ya Simba kwamba Mkutano Mkuu wa Klabu hiyo ulikwisha msamehe. Kwa hali hiyo taarifa ya kusimamishwa kwake iliyotumwa TFF mwezi Mei 2010 itaendelea kuzingatiwa hadi hapo Klabu ya Simba itakapo ijulisha TFF mabadiliko ya maamuzi hayo.

3. MAAMUZI KUHUSU UCHAGUZI WA FAM

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilimuondoa Ndg. Michael Wambura kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa FAM kwa kuwa alifungua kesi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam dhidi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba akiwa ni mwanachama wa Klabu ya Simba kuzuia uchaguzi wa klabu ya Simba usifanyike, jambo ambalo ni uvunjaji wa Katiba ya Klabu ya Simba, ukiukwaji wa Katiba ya FAM, TFF na FIFA.

Pia, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliweka wazi kama ilivyobainisha kwenye uchaguzi wa Klabu ya Simba kwamba suala la uadilifu wa Ndg. Wambura lilishafanyiwa maamuzi na Kamati ya Rufaa ya TFF mwaka 2008 kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi Mkuu wa TFF. Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi huo na Katiba ya TFF Mamlaka pekee inayoweza kutengua uamuzi huo ni Mahakama ya Usuluhishi wa masuala ya Michezo (CAS) iliyo na makao yake Lausanne, Switzerland.

Baada ya uamuzi huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeshuhudia baadhi ya vyombo vya TFF vikishughulikia masuala ya uchaguzi kinyume na matakwa ya Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi, kama ifuatavyo:

(i) Katika hali isiyozingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF, Kamati ya Nidhamu ilipokea malalamiko ya Ndg. Michael Wambura yaliyoitwa ‘rufaa’. Kwa kuwa hakuna utaratibu wa masuala ya uchaguzi kukatiwa rufaa kwenye Kamati za nidhamu katika ngazi zote za uchaguzi na hivyo pia kutokuwepo ada ya ‘rufaa’ za aina hiyo, mlalamikaji alilazimisha kupokelewa ada ya Tshs 300,000/= ambayo ni ada inayotumika kwa rufaa za Ligi Kuu ya Vodacom ambayo imeainishwa katika Ibara ya 17 ya kanuni za mashindano hayo. Ada hiyo iliwekwa (deposited) kwenye Akaunti ya TFF bila ridhaa ya TFF. Pamoja na mapungufu hayo “rufaa’ hiyo ilisikilizwa na Kamati ya Nidhamu na kutolewa maamuzi. Mlalamikaji hakuridhika na maamuzi ya Kamati hiyo na aliamua kukata ‘rufaa’ katika Kamati ya Rufaa ya TFF.

(ii) Kamati ya Rufaa ya TFF ilipokea na kusikiliza ‘rufaa’ ya Ndg. Michael Richard Wambura, kinyume na matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kwa kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF hakuna rufaa inayokatwa kwenye Kamati hiyo, hivyo kutokuwapo ada yoyote kwa “rufaa” ya aina hiyo, ili kutimiza azma ya kusikiliza ‘rufaa’ hiyo, palifanyika juhudi za kulazimisha kupokelewa ‘ada’ ya Shilingi 500,000/= ambayo ni ada ya rufaa za mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom ambayo imeainishwa pia katika Ibara ya 17 ya kanuni za mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom. Hata hivyo, ada hiyo ambayo si halali, haikupokelwa na Sekretarieti ya TFF baada ya kushindikana kuainisha ada ya mashindano ya Ligi Kuu ya Vodacom na masuala ya Uchaguzi. Bila kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya TFF Ibara ya 47(4) inayotamka na kuikataza Kamati ya Rufaa kusikiliza rufaa kwa mambo yaliyowekewa ukomo na Kanuni husika; Ibara hiyo inatamka; ‘The Appeal Committee shall be responsible for hearing appeals against decisions from the Disciplinary Committee that are not declared final by relevant regulations as well as decision passed by the players’ Status Committee concerning the eligibility of players for the teams’, Kamati hiyo ilisikiliza malalamiko ya Ndg. Michael Richard Wambura na kutoa uamuzi bila kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF ambazo ni ‘relevant regulations’ na Ibara ya 12(4) ya Kanuni hizo kutamka wazi kuwa; ‘The decisions of the TFF Elections Committee are final and conclusive and shall not be monitored by any other body’.



(iii) Kamati ya Uchaguzi ya TFF inatamuka wazi kuwa utaratibu mzima uliotumika kupokea rufaa hiyo toka Kamati ya Nidhamu hadi ya Kamati ya Rufaa haukufanyika kwa mujibu wa taratibu za ukataji rufaa zilizoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Ukataji rufaa huo uliongozwa zaidi na hila kuliko dhamira ya kuheshimu taratibu zilizowekwa. Mbali na kutumia kanuni za Ligi kuu ya Vodacom kusikiliza ‘rufaa’ hizo, uthibitisho mwingine wa hila na ujanjaujanja ni pale mlalamikaji alipokwenda kuweka kwenye akaunti ya TFF ada ya rufaa ya mashindano ya Ligi Kuu ambayo haitambuliki kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na kutumia vyombo vya habari kutangaza kitendo hicho, lakini baada ya kutolewa maamuzi na Kamati ya Rufaa alienda kimya kimya TFF kuchukua ada hiyo ambayo ni ya rufaa kwa mashindano ya Ligi kuu.

(iv) Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa mamlaka yaliyo kasimiwa kwake na Katiba ya TFF Ibara ya 49(1) , Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 6, Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 8(2), 10(6), 12(4) na 26(2), na pia kwa mamlaka yaliyoainishwa katika Katiba za wanachama wa TFF kuhusu uchaguzi, katika kikao chake kilichofanyika 03 Desemba 2011 iliamua na inatamka wazi kuwa maamuzi yaliyofanywa na Kamati ya Rufaa ni BATILI kwa kuwa hayakuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaziagiza Kamati zote za Uchaguzi za wanachama wa TFF na wanachama wao kuendelea kuzingatia Kanuni za Uchaguzi katika utendaji wa kazi zao za kuendesha na kusimamia chaguzi zote za vyama vya mpira wa miguu nchini, ikiwa ni pamoja na kutozingatia maamuzi yoyote ya uchaguzi yatakayofanyika kinyume na Kanuni za Uchaguzi.


4. TAARIFA ZA UDANGANYIFU KUTOKA KWA BAADHI YA WAGOMBEA UONGOZI KWENYE VYAMA WANACHAMA WA TFF.

Kamati ya Uchaguzi inapenda kuwakumbusha wadau wote wa soka wenye nia ya kugombea uongozi TFF na vyama wanachama wa TFF kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TFF ibara ya 25(8) na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26(8) ni makosa kuwasilisha taarifa za udanganyifu kwenye Kamati ya Uchaguzi. Kanuni hizo zinatamka kuwa; During the election process any person or member who contravenes this code or provides false particulars or qualification, may be penalized to a fine not exceeding five hundred thousand shillings or be barred to participate in the election process for 2 years or for both a fine and such barring, provided that the General Secretary lodges a complaint to the TFF judicial organ for disciplinary action.

Kamati imebaini kuwa baadhi ya wagombea walifanya udanganyifu kuhusu vyeti halisi walivyowasilisha kwenye uchaguzi wa FAM na pia baadhi ya waombaji uongozi katika uchaguzi wa klabu ya Villa. Kwa mfano mwombaji aliyeomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Villa cheti chake cha Elimu ya Msingi alichowasilisha kwenye Kamati ya Uchaguzi kina utata. Vyote hivyo viko katika hatua za uhakiki kwenye mamlaka husika, uhakiki utakapokamilika Kamati itachukua hatua kwa mujibu wa Kanuni tajwa hapo juu.

Kamati imebaini na kujiridhisha kuwa Ndg. Michael Wambura alitoa taarifa zinazokinzana kwenye Kamati ya Uchaguzi kuhusu umri wake. Katika Uchaguzi wa Klabu ya Simba mwaka 2010, aliwasilisha taarifa kwamba amezaliwa mwaka 1967 lakini katika uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara aliwasilisha taarifa kwamba alizaliwa mwaka 1965. Taarifa za umri zinazokinzana za mwombaji uongozi zinashiria mashaka ya umakini na uadilifu wa mgombea hasa ikizingatiwa kuwa nafasi ya uongozi ya mwenyekiti kwa vyama wanachama wa TFF na Rais wa TFF zina ukomo wa wa umri. Kamati itachukua hatua zilizoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi tajwa hapo juu.






5. KAULI ZENYE LENGO LA KUVURUGA CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF.

Katika siku za karibuni Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeshuhudia kauli amabazo si za kiwanamichezo zenye lengo la kuleta vurugu katika michakato ya Uchaguzi. Kwa mfano kauli za kuwahamasisha wadau wa soka kwenda mahakamani kwa masuala ya michezo, hususan, kupinga michakato ya uchaguzi ni uvunjaji wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF na FIFA. Kamati inawataka wadau wote wa soka kuheshimu na kuzingatia Kanuni na taratibu za uchaguzi na Katiba ya TFF, vinginevyo Kamati haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.





Deogratias J. Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa