Wanakijiji wavamia mgodi, wateka malori ya madini |
Wanakijiji wavamia mgodi, wateka malori ya madini |
0digg Masoud Masasi, DodomaVURUGU kubwa zimeibuka juzi baada ya wanakijiji wa Kitongoji cha Muungano wilayani Dodoma, kuyateka magari mawili yaliyokuwa yamebeba mawe yenye madini kisha kuyapeleka ofisi za kijiji hicho kutokana na kile walichodai kuwa mwekezaji aliyedai kupewa idhini ya kuchimba madini katika eneo hilo, amekiuka makubaliano. Tukio hilo ni mwendelezo wa ghasia ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini yenye maliasili hiyo ya madini kutokana na wananchi kupinga kile wanachokiita unyonyaji kutoka kwa wawekezaji na tayari ghasia kama hizo, zimewahi kutokea maeneo ya Nyamongo, Tarime, Geita na hivi karibuni wilayani Nzega. Juzi, wakazi hao Kijiji cha Muungano nao walifanya ghasia wakimpinga mwekezaji anayefahamika kwa jina la Edward Mgomba ambaye alifika eneo hilo la machimbo ya rubi akiwa na magari mawili aina ya Mitsubishi fuso na kuanza kupakia mawe hayo. Hata hivyo, wakati akiendelea kupakia, kundi la wanakijiji wapatao 200, walifika katika eneo hilo na kuyazingira magari hayo kisha kuamuru madereva kuyapeleka mawe hayo kwenye ofisi ya kijiji kwa ajili ya maelezo. Wakati madereva hao pamoja na mwekezaji huyo wakiendelea kuzozana na wanakijiji hao, kundi jingine la wanakijiji lililotokea hatua iliyofanya kutokea kwa vurugu hizo na baadaye kufanya madereva wa magari kukubali kupeleka magari hayo kwenye ofisi ya kijiji. Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alifika eneo la tukio wakati vurugu hizo zikiendelea na kufanikiwa kuzizima baada ya kuzungumza na wananchi hao kwa lugha ya Kigogo. Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, John Mandewa alisema mwekezaji huyo alianza kuchimba madini hayo tangu Novemba bila ya kufuata taratibu, jambo lililofanya uongozi kumzuia asiendelea kuchimba madini hayo, lakini baadaye alikuja na barua aliyodai kuwa imeandikwa na Mkurugenzi wa Wilaya kumtambulisha mwekezaji huyo kufanya shughuli za uchimbaji wa mawe hayo. “Mwanzoni baada ya kuona tumemzuia kuchimba, alikuja na barua aliyodai kuwa amepewa na Mkurugenzi Mtendaji kumtambulisha ili afanye shughuli za uchimbaji wa madini. Barua hiyo ilikuwa ikionyesha anatakiwa kuanza shughuli hiyo Januari mwakani. Baada ya kuiona barua hiyo tuliamua kuitisha mkutano wa kijiji na kumweleza mikakati yetu,”alisema Mandewa. Alifafanua kwamba walikubaliana kuwa shughuli hiyo iwe na mikakati ya kuzuia uchafuzi wa mazingira na kusaidia shughuli za maendeleo katika kijiji hicho, lakini mwekezaji huyo alianza kuchimba mawe hayo tangu wakati huo bila ya kutoa taarifa zozote, huku akienda kinyume na makubaliano yaliyofikiwa. Lusinde ambana Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Lusinde alianza kumhoji mwekezaji huyo kujua amepata wapi kibali cha kufanya kazi hiyo. Lakini mwekezaji huyo aliendelea kueleza kuwa alikipata kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Alisema kwa mujibu wa kibali hicho, alipaswa kuanza kazi hiyo Januari. “Leseni ya uchimbaji madini haya nilipewa na mkurugenzi wa halmashauri ambapo tulikuwa tunatakiwa kuanza rasmi mwezi Januari. Sasa tulikuwa tuko katika majaribio, huwezi kuamua kuingia makubaliano ya kuanza kuchimba bila ya kuangalia kama madini yapo au la, ndio maana tukaanza mwezi Novemba,”alisema Mgomba. Jibu hilo lilimfanya mbunge Lusinde kumpigia simu mkurugenzi huyo wa wilaya, Daudi Mayeji na kumweleza madai ya mwekezaji huyo kwamba alipata kibali cha kuchimba madini kutoka ofisini kwake. Mkurugenzi huyo aliagiza magari hayo yaliyokuwa na madini, yaendelee kushikiliwa kwenye ofisi za kijiji hicho na mwekezaji huyo aende ofisini kwake kwa ajili ya kukagua vibali hivyo akiwa na vielelezo vyote. Maelezo ya mkurugenzi huyo yalimfanya Lusinde kuamua kupiga simu polisi ili kuweza kuyalinda magari hayo pamoja na mwekezaji huyo, ili kuweza kupata ukweli halisi wa leseni hiyo ambayo mwekezaji huyo alidai kupewa na Halmashauri ya wilaya. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, mkurugenzi Mayeji alifika katika kijiji hicho na baada ya ukaguzi alimkana mwekezaji huyo na kusema hajawahi kuwaona watu hao hata ofisini kwake kwa ajili ya kuomba kibali cha shughuli za kuchimba madini katika kijiji hicho. Hatua hiyo ilifanya magari hayo pamoja na mwekezaji huyo kwenda katika Kituo cha Polisi cha Mvumi huku mwekezaji huyo akitakiwa kulipa kijiji hicho gharama zote za madini hayo tangu alipoanza kuchimba. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Steven alipoulizwa kwa kwa simu jana, alisema "Hadi sasa sina taarifa. Ndio kwanza nazipata kutoka kwako, lakini nashukuru kwa sababu sasa ndio naanza kuzifuatilia." |
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa