Kanali Muammar Gaddafi SERIKALI YALAANI YASEMA TANZANIA HAIPASWI KUSHANGILIA
Waandishi Wetu
NANI alimuua Kanali Muammar Gaddafi? Hili ni swali ambalo limeibua mjadala mkubwa tangu kutangazwa kwa taarifa za kifo cha kiongozi huyo wa Libya juzi. Wakati baadhi ya mitandao ya nchi za Magharibi, ikisisitiza kuwa aliuawa na wapiganaji wa Baraza la Mpito (NTC), kuna taarifa nyingine zinazosema kwamba aliuawa na mlinzi wake.
Taarifa za Gaddafi kuuawa na mlinzi wake zilipatikana katika mahojiano ya baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo na waandishi wa habari la Reuters katika Mji Mkuu wa Libya, Tripoli jana. Hata hivyo, picha zinazoonyesha mauaji hayo zimesambaa katika mitandao mbalimbali duniani, zikionyesha namna alivyoshambuliwa na wapiganaji wa NTC akiwa na majeraha ya risasi.
Moja ya picha hizo inamwonyesha akijitetea kabla ya kuuawa kwa kusema “Hii siyo sawa, hii siyo sahihi katika sheria za Kiislamu. Hivi mnajua haki katika ubaya?” Maneno hayo ya Gaddafi yalijibiwa na mpiganaji mmoja wa NTC, aliyemwambia, “Nyamaza we mbwa.”
Katika tukio hilo, Gaddafi alikutwa na bastola iliyotengenezwa kwa dhahabu, pia kulikuwa na miili 50 ya watu waliokufa katika shambulio hilo.
Mmoja wa wapiganaji wa NTC alikaririwa akisema kuwa baada ya mapambano makali na walinzi wa Gaddafi kuzidiwa nguvu, kiongozi huyo wa zamani wa Libya alipiga kelele akisema: “Tafadhali, msiniue wanangu, msiniue wanangu.” Tangu mapambano hayo yaanze Februari mwaka huu, Gaddafi anaelezwa kwamba alibadilisha walinzi kutokana na kikosi chake cha awali kusambaratika kadri siku zilivyosonga, amekuwa akitumia zaidi askari mamluki hasa baada ya kukimbiwa na askari wake wengi akiwa katika mji wa Sirte, ambako ndiko alikozaliwa.
Waandishi waliokuwapo katika eneo la tukio walieleza kwamba waliona magari kadhaa ya msafara wa Gaddafi yakitokea katika Mji wa Sirte yakiwa na mizinga ya kutungulia ndege iliyokuwa imeteketea moto. “Kwanza tuliwashambulia kwa mabomu ya kutungua ndege, lakini haikusaidia sana.
Tuliamua kushuka katika magari na kuanza kuwashambulia tukiwa ardhini,” alisema mmoja wa wapiganaji wa vikosi NTC, Salem Bakeer na kuongeza: “Baada ya majibizano makali ya risasi, tulisikia sauti ikitokea kwenye mtaro. Nadhani Gaddafi aliwaamuru waache kujibu mashambulizi. Mmoja wa askari wake alisema: “Mkuu wangu yuko hapa, mkuu wangu yuko hapa.”
Msimamo wa Tanzania
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe, amesema Tanzania haiwezi kushangilia kifo cha Gaddafi kwa kuwa mila na utamaduni wetu, hauruhusu kufurahia vifo. Membe alisema hayo kwa nyakati tofauti jana Dar es Salaam, katika mahojiano na Televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) katika kipindi cha Jambo Tanzania na wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya Miaka 50 ya Uhuru ya Wizara yake kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja.
“Watanzania hatuna tabia na utamaduni wa kusherehekea kifo cha mtu, hata kama ni adui wetu,’’ alisema Waziri Membe na kuongeza: “Pia nina hofu kuwa sasa ni mwanzo wa mapigano na machafuko mapya nchini humo.” “Hatuna utamaduni wa kusherekea kifo hata kama mtu ni adui yetu kifo cha Gaddafi tumekipokea kwa masikitiko makubwa. Kiongozi huyu atakumbukwa kwa kuleta amani na umoja wa Afrika,” alisema Membe.
Waziri Membe alisema Gaddafi aliuawa kikatili na kwamba NTC limekiuka maazimio na mwongozo wa Umoja wa Afrika uliotaka matumizi ya njia ya amani katika kukabiliana na tatizo hilo.
“Watanzania watambue kuwa Tanzania kama taifa, hatuwezi kufurahia kifo cha Gaddafi. Serikali iliunga mkono azimio namba moja la Umoja wa Mataifa la kumfungia Gaddafi kutumia anga ya kimataifa, lakini hatukuunga mkono Azimio namba mbili ambalo lilitoa nafasi kwa Majeshi ya NATO na USA, kuingia nchini Libya na kushambulia,” alisema.
Alionya kuwa waliomuua Gaddafi wasidhani kuwa ndiyo mwisho wa matatizo katika nchi hiyo, kwani kuna watu waliofiwa na ndugu zao ambao watajitokeza kulipiza kisasi na mapigano kuendelea. “Haiwezekani nchi yenye makabila zaidi ya sita iongozwe na kabila moja baada ya vifo vya watu 3,000 hawa watu lazima watagombana tu na hii inaashiria mwendelezo wa vita nchini Libya,” alisema Membe.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema anasikitika juu ya kifo hicho... “Ni heri angekamatwa akiwa hai na kufikishwa mahakamani ili haki itendeke kuliko kumwua.” Kuzikwa kwa siri NTC limesema kuwa mwili wa Gadaffi utazikwa kwa taratibu zote za dini ya Kiislamu lakini katika kaburi la siri.
Taarifa hizo zilipatikana jana kupitia shirika la habari la Reuters, zimemkariri msemaji wa NTC akieleza pia kwamba mwili wa Kanali Gaddafi bado utaendelea kuhifadhiwa kwa siku kadhaa kabla ya kuzikwa.
Hatua ya kuficha kaburi yake inaelezwa kuwa na lengo la kuzuia wale wanaomwamini na kumpenda hofu ikiwa kwamba huenda wakaifanya sehemu hiyo kuwa takatifu kwao na kusababisha jina lake kuendelea kutawala miongoni mwa Walibya.
Rais Chavez amlilia
Rais Hugo Chavez wa Venezuela ambaye ni miongoni mwa viongozi waliokuwa marafiki wa karibu wa Kanali Gaddafi, ameeleza masikitiko yake kutokana na kifo hicho.
“Wamemuua kinyama. Wameibua hasira mpya,” alisema Chavez ambaye kwa sasa anaendelea kufanyiwa uchunguzi wa afya huko na kuongeza: “Tutamkumbuka katika maisha yetu yote kama mpiganaji shupavu, mwanamapinduzi na mwanasiasa aliyeteswa kwa sababu ya misimamo yake.”
Chavez amekuwa akimtetea na kumuunga mkono Gaddafi tangu kuanza kwa vuguvugu dhidi ya utawala wake Februari mwaka huu na amekuwa akilaani kitendo cha Nato kujiingiza katika mgogoro huo. “Suala la kutia huruma ni kwamba, ili kujaribu kuutawala ulimwengu, dola kubwa na washirika wake wanajiingiza katika moto bila kujua,” alisema. Habari za kifo cha Gaddafi zimetawala katika mitandao mbalimbali ya kijamii na watumiaji wa mtandao wa intaneti wamekuwa wakieleza hisia zao kuhusiana na kifo hicho.
Watumiaji wa mitandao hiyo kote Afrika wamekuwa wakiitumia kuwasiliana na wenzao kote duniani kuelezea tukio hilo hatua kwa hatua. Wamekuwa wakichukulia tukio la kifo chake kwa mitizamo tofauti, wengine wakimsifu na kuihurumia Libya na wengine wakimlaumu na kuitakia heri Libya bila Gaddafi.
AU yaialika serikali mpya ya Libya Baada ya kifo hicho, Umoja wa Afrika (AU), umeialika rasmi Serikali mpya ya nchi hiyo. Mwenyekiti wa Tume ya AU, Dk Jean Ping alisema umoja huo umeialika, Serikali hiyo mpya Alhamisi.
Alisema viongozi wa serikali ya mpito wanapaswa kutayarisha uchaguzi wa kidemokrasia na wakati huohuo kuyaleta pamoja makundi hasimu ya kikabila na makundi ya kisiasa ya nadharia mbalimbali.
Habari hii imekusanywa na Andrew Msechu, Aziza Masoud, Kelvin Matandiko, Michael Jamson |
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa