Translate in your language

Friday, September 23, 2011

Kampeni Chadema, CCM zafika pabaya




Daniel Mjema, Igunga (Mwananchi)
JOTO la uchaguzi mdogo katika Jimbo la Igunga, mkoani Tabora linaendelea kupanda baina ya vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo, huku kampeni zinazoendelea zikichukua sura ya mapambano baina ya vyama viwili vikubwa nchini, CCM na Chadema.Katika kile kinachoonekana kuwa hofu kadri siku ya uchaguzi inavyokaribia, jana CCM kupitia Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama, kiliendeleza tuhuma dhidi ya Chadema ambacho kwa upande wake kilijibu mapigo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.Mukama akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Igunga, alitoa tuhuma nzito kwa Chadema, akisema chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kimeingiza kundi la makomandoo 33 kwa lengo la kuvuruga uchaguzi.

Katibu Mkuu huyo aliyekuwa akizungumzia tathmini ya kampeni za uchaguzi huo mdogo, alitumia muda mwingi kukizungumzia Chadema, huku akivisahau vyama vingine sita ambavyo pia vinashiriki uchaguzi huo.
Hata hivyo, Mbowe akizungumza na Mwananchi alijibu tuhuma hizo kwa kumshangaa Mukama na kueleza kuwa kauli zake katibu mkuu huyo wa CCM ni matokeo ya “kushiriki siasa za uzeeni”."Sasa hili Mukama hawezi akajua kwa sababu yeye anafanya siasa za uzeeni. ..Yeye (Mukama) hajawahi kugombea udiwani, uenyekiti wa mtaa, ubunge au nafasi yoyote ndani ya chama chake zaidi ya huu ukatibu mkuu ambao alipewa tu.. atayajuaje hayo?" Alihoji na kuendelea:
Lakini muulize (Mukama), CCM hawafanyi hayo?"
Tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga, CCM kimekuwa kikitoa shutuma kadhaa kwa Chadema, baadhi yake zikiwa ni kuhusika na uchomaji moto wa banda la kuku la Katibu wa CCM, Kata ya Nyandekwa, Hamis Makala na kumwagiwa tindikali kwa kada wa chama hicho, Mussa Tesha (24).
Hata hivyo, mjadala miongoni mwa wanasiasa, wasomi na wanaharakati ni mtiririko wa tuhuma dhidi ya Chadema, ambazo zimekuwa zikitafsiriwa kuwa ni “mbinu chafu” dhidi ya chama hicho ambacho ni mpinzani mkubwa wa CCM kwa sasa.Vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo ni CUF, Chausta, DP, UPDP, SAU na AFP.

Tuhuma za Mukama
Mbali na madai kwamba Chadema kimeingiza nchini makomandoo 33 aliodai kuwa wamepata mafunzo katika nchi za Libya, Palestina na Afghanistan, Mukama aliufananisha uongozi wa Chadema na ule wa Rais wa Libya Muammar Gaddafi na kwamba uongozi wa aina hiyo, unapaswa kubezwa na kuondolewa.
Mukama alidai CCM kinafanya kampeni za kiungwana ikilinganishwa na wapinzani wao Chadema, ambao alidai wameingiza makomandoo hao 33 wanaofahamika kwa majina na nchi walizosomea ugaidi huo.Huku akinukuu barua aliyodai ni ya Chadema, Mukama alisema makomandoo hao wamewekwa katika maeneo ya Itobo, Bulinde, Sakamaliwa, Bukene na Chuma cha Mkore katika jimbo hilo.
“Ni kweli sisi CCM tunashambulia Jimbo la Igunga kama nyuki, lakini hatujaleta mamluki kutoka nje… tunao viongozi wa CCM kwenye vijiji na kata hao ndio tunaowatumia,”alisema.
Aliongeza: “CCM hatujaleta makomandoo waliopata mafunzo Afghanistan kuja kutisha watu na kuwamwagia tindikali…Wenzetu wamewaleta, wapo na tunayo orodha na mahali walipopata mafunzo hayo…hii hapa orodha.”
 Bila kuwataja majina, Katibu mkuu huyo alisema baadhi yao walipata mafunzo Palestina mwaka 2001, Libya (1990) na kusisitiza kuwa tayari orodha hiyo wameikabidhi vyombo vya dola.Wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, alisema Chadema hakiwezi kukiondoa madarakani chama makini kama CCM na kutoa mfano kuwa uongozi wa Chadema ni kama wa kifamilia ambao haufai.
“Uongozi wa Chadema unatofautianaje na wa Gaddafi (Muammar)?" Alihoji Mukama na kusema ni uongozi wa baba, mkwe na watoto bila kufafanua alikuwa akimlenga kiongozi gani ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Alifafanua kuwa pamoja na vurugu zote wanazofanyiwa wanachama na makada wake, CCM kitaibuka na ushindi kutokana na mfumo mpana wa uongozi ilionao kuanzia ngazi ya matawi, kata na wilaya.
CCM kimemsimamisha Dk Dalaly Kafumu kupeperusha bendera yake katika uchaguzi huo mdogo ambao umetawaliwa na ushindani mkubwa baina ya chama hicho, Chadema na CUF. Jambo lingine ambalo alisema litakisaidia CCM kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huo ni kuwatumia wenyeji kufanya kampeni huku viongozi wa kitaifa wakisaidia tu kuongeza nguvu.
  “Tunaye mgombea mwenye sifa ya mahitaji ya nchi na mahitaji ya Igunga, hatuna mashaka kabisa na hata huko tunapopita wananchi wanatuambia ameshakuwa mbunge wanasubiri tu kumthibitisha Oktoba 2,”alisema Mukama.
 Majibu ya Mbowe
Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu tuhuma hizo, Mbowe alimshangaa Mukama na kueleza kuwa kauli zake ni matokeo ya siasa za uzeeni.Alisema katika kipindi cha uchaguzi ni jambo la kawaida kwa chama chenye wapenzi wengi kama Chadema na CCM yenyewe kupokea mashabiki, makada na wapenzi kutoka nje ya eneo la uchaguzi.
Mbowe alisema Chadema kina wapenzi na mashabiki kadhaa kutoka nje ya wilaya ya Igunga, lakini akaeleza kuwa siyo makomandoo kama anavyodai Mukama vinginevyo atoe ushahidi na kuwataja kwa majina.
"Igunga ni eneo dogo sana watu wengi wanalala nje ya mji, wabunge wetu wanalala kwenye magari, sasa inakuwaje ajabu Chadema kuwa na wageni wanaolala nje ya mji? Haya haifanyi Chadema tu hata CCM ina wapenzi wake kutoka nje ya Igunga... anyway simlaumu Mukama, hii ni kwa sababu hana experience (uzoefu) wa masuala ya uchaguzi.
Katika hatua nyingine, Mbowe alipuuza madai ya Mukama kwamba Chadema kinafanana na Utawala wa Gaddafi akisema:
"Akumbuke wiki tatu kabla Bunge halijaahirishwa, Waziri Membe alimsifia sana Gaddafi na akatamka kwamba Tanzania inamuunga mkono, hakuishia hapo, alishawahi kuagiza ubalozi wa Libya nchini ushushe bendera ya waasi.
Iweje leo Mukama apingane na misimamo ya Serikali ya chama chake kwa kumponda kiongozi huyo?"
Mbowe alisema kauli hiyo ya Mukama inaonyesha kuwa CCM ni chama legelege ndiyo maana hata hakitambui misimamo ya Serikali yake na kwa kumfanya Mukama kuwa Katibu Mkuu, ndiyo kinapoteza mwelekeo.Tangu kuanza kwa kampeni wiki mbili zilizopita, vyama vya CCM na Chadema vimekuwa vikishutumiana kwa matukio mbalimbali ya uhalifu yanayoendelea katika Jimbo la Igunga.

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)