Translate in your language

Friday, September 9, 2011

CUF yakwama kuvizuia CCM, Chadema Igunga



 Send to a friend



Naibu Kamishina wa kitengo cha operesheni cha Jeshi la Polisi Isaya Mguru akifafanua jambo wakati wa mkutan o na viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mgodo Jimbo la Igunga
Boniface Meena na Geofrey Nyang’oro, Igunga
(Gazeti la Mwananchi)
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimewawekea pingamizi wagombea ubunge kupitia vyama vya Chadema na CCM kwa madai kuwa hawakurudisha fomu kwa kufuata kanuni na sheria za uchaguzi. Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Msimamizi wa Uchaguzi, Magayane Protas alisema ametupilia mbali pingamizi hilo.
“Mgombea wa CUF, Ndugu Mahona amewasilisha pingamizi dhidi ya wagombea wa Chadema na CCM akidai kuwa walirudisha fomu kinyume cha sheria. Lakini nimeangalia sheria inavyoeleza na kuona hawakufanya kosa lolote wakati wakirudisha fomu hivyo, nimelitupilia mbali pingamizi hilo.”

Pia alisema mgombea wa SAU, John Magid aliwasilisha pingamizi dhidi ya wagombea wa Chadema na CCM akidai kuwa si wanachama halali wa vyama hivyo kwa kuwa ni wafanyakazi wa Serikali. Akizungumzia madai hayo, Magayane alisema Magid alisahau kuwa kuna waraka namba 1 mwaka 2000 ambao unaruhusu mtumishi wa umma kugombea katika chama.


“Kwa bahati nzuri hawa wagombea wa Chadema na CCM walishaandika barua serikalini kuachia nafasi zao na barua zenyewe ni hizi hapa, hivyo ni halali wao kugombea,” alisema Magayane.

Alisema kuwa kutokana na kujiridhisha, ametupilia mbali pingamizi hilo pia. Hata hivyo, Magayane alisema kuwa kama walalamikaji hawajaridhishwa na uamuzi wake, wanaweza kukata rufaa ndani ya saa 24.

Alisema wagombea wa vyama vinane wamepitishwa kuwania ubunge wa jimbo hili ambao ni kutoka CCM, CUF, Chadema, Chausta, AFP, UPDP, SAU na DP.

Chadema kuzindua kampeni leo
Chadema kinatarajia kuzindua kampeni zake rasmi leo. Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa chama hicho, Waitara Mwita alisema kuwa watawapokea viongozi wa kitaifa kwa maandamano kuanzia saa 6:00 mchana ili kuelekea kwenye eneo la mkutano katika Uwanja wa Sokoine.

“Tutaanza maandamano yatakayoongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na wajumbe wa kamati kuu pamoja na wabunge na mkutano utaanza saa 8:00 mchana na kumalizika saa 12:00 jioni,” alisema

Polisi yavifungulia mashtaka Chadema, CUF

Jeshi la Polisi limefungua jalada la mashtaka dhidi ya vyama vya Chadema na CUF, kutokana na madai ya kukiuka taratibu za uchaguzi wakati wa urudishaji fomu za wagombea wao katika uchaguzi huo mdogo wa Jimbo la Igunga.
Mbali ya kufungua jalada hilo, jeshi hilo pia limetoa onyo kwa vyama hivyo kuhusu mabaunsa wao na kuwataka wahakikishe wanafanya ulinzi kwa kufuata utaratibu, sheria na kanuni zilizowekwa.

Mkuu wa Operesheni Maalumu wa Polisi, Simon Sirro alisema walifungua jalada dhidi ya Chadema akidai kwamba baada ya kumaliza kurudisha fomu walifanya mkutano wa hadhara kinyume cha sheria.

Juzi, mashabiki wa vyama vya Chadema na CUF walitunishiana misuli wakati wa urejeshaji fomu za wagombea wao kwenda Ofisi ya Tume ya Uchaguzi, hatua ambayo nusura isababishe ghasia na uvunjifu wa amani na baadaye Chadema kilifanya mkutano wa hadhara.

Sirro alisema: “Tumefungua madai hayo kama polisi dhidi ya Chadema kwani baada ya kumaliza kurudisha fomu, walifanya mkutano wa hadhara na nilikwenda kuwaambia hiyo si sawa,” alisema Sirro.
Alisema Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Kigaila Benson alihojiwa na polisi kuhusu tukio hilo hivyo maelezo yake yako polisi. Benson alikiri kukutana na polisi kuzungumzia suala la Chadema na CUF kuingilia msafara wao juzi.

Kigaila alisema katika mkutano huo aliwaambia polisi kuwa Chadema haikufanya mkutano, bali ilikuwa ikiwashukuru wananchi na kuwatawanya baada ya kumaliza kurudisha fomu na kurejea nao kwenye viwanja vya ofisi yao, vilivyopo katika Barabara ya Singida.

“Nilimweleza Sirro kuwa hatukufanya mkutano kwa kuwa kabla hatujapeleka fomu tulikuwa na watu wengi ofisini kwetu na tuliondoka nao kwenda kuchukua fomu na kurudi nao kisha tukawashukuru na kutawanyika,” alisema Benson.
Sirro alifafanua kuwa CUF imefunguliwa jalada la madai kutokana na kitendo chake cha kuingilia msafara wa Chadema wakati wa kurudisha fomu za mgombea wao juzi. Alisema kutokana na tukio hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alihojiwa na polisi.

“Tumefungua pia jalada dhidi ya CUF kuingilia msafara wa Chadema na mhamasishaji wa CUF Bwana Mtatiro, alihojiwa kuhusu kilichotokea jana (juzi),”alisema Sirro.

Alisema juzi aliviita vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu na kuvitaka vifanye kampeni kwa amani kwa kuwa mbunge wa jimbo hilo hawezi kupatikana kwa vurugu.

“Wote ni viongozi hivyo lengo ni kufanya kampeni kwa amani na utulivu. Hatutegemei kupata mbunge kwa njia ya vurugu, bali kampeni ziwe za utulivu na amani na kuongeza: “Tuko nao muda wote wa kampeni wajue hilo.”
Juzi, Sirro aliwasili jimboni Igunga kwa ajili ya kuhakikisha kampeni za uchaguzi huo zinakwenda sawa na kuweka usalama hadi utakapokamilika.

Alisema jeshi la polisi limejipanga vyema kusimamia usalama katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu.

“Tumejipanga vizuri na kazi inaendelea vizuri, nitakuwapo muda wote kwa kuwa ndiyo kazi yangu ila nikitoka mkuu wa FFU ndiye atakayekuwa akisimamia haya,” alisema Sirro.
mwisho

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)