ASEMA WATUMIA UWEZO WAO KUMKWAMISHA, ATAMANI KUACHIA NGAZI
Waziri wa Ujenzi, Dr. John Magufuli WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amewashukia baadhi ya vigogo jiji la Dar es Salaam akiwatuhumu kutumia uwezo wao kifedha kukwamisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya ujenzi wa barabara na kutoa msimamo wake kwamba wakati mwingine anatamani kuachia ngazi ili awe mbunge wa kawaida.
Kauli ya Dk Magufuli inakuja kipindi ambacho amekuwa katika mgogoro na baadhi ya wafanyabiashara katika mpango wa bomoabomoa nyumba na mabango ya biashara.
Alisema baadhi ya maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kujenga vituo vya mabasi yaendayo kasi, sasa hivi yamejengwa vituo vya mafuta, akitoa mfano wa eneo la Urafiki.
Dk Magufuli aliyasema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia makadirio na matumizi ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2011/12.“Ndugu zangu wabunge kazi hii ya uwaziri ni ngumu sana msione hivi, hata wenzangu huko nyuma wanajua wazi (akimaanisha mawaziri wa wizara nyingine),” alisema.
Alisema kuliko kuonekana si mchapakazi kutokana na nguvu za vigogo wachache, wakati mwingine anafikia hatua ya kutamani hata kuacha uwaziri.“Kila kitu kinatakiwa kufanywa kwa kufuata sheria… wapo watu wanaokiuka sheria kwa sababu wanazozijua wao, bila kutekeleza sheria hakuna kitakachofanyika, huo ndiyo ukweli,” alisema Dk Magufuli.
Huku akinukuu vifungu vya sheria na kutaja barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami nchini, Dk Magufuli alisema: “Dar es Salaam ukijenga barabara watu nao wanajenga vibanda kando ya barabara hiyo, sasa hata barabara za juu (fly overs) zikijengwa wanaweza kujenga hata vibanda na vituo vya mafuta.”
Alisema katika kutekeleza mradi wa upanuzi wa barabara jijini Dar es Salaam, Serikali imetenga Sh3.47 bilioni kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi waliojenga katika barabara zilizopandishwa hadhi na kuwa barabara kuu.
Alisema kuwa utekelezaji wa ujenzi wa barabara nchini unafanywa na Serikali ya CCM, huku akisisitiza kuwa chama hicho tawala hakiwezi kufa na kitahakikisha kuwa kinajenga barabara zote kwa kiwango cha lami kwa kuzingatia ilani yake ya uchaguzi.Alisema kuna ulazima wa ujenzi wa barabara za Dar es Salaam kusimamiwa na kamati maalumu kwa kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wake umegubikwa na utata.
Sendeka azua balaa
Kauli ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka kwamba Serikali inaelekea kufa kutokana na mgawanyo mbovu wa rasilimali, imechafua hali ya hewa bungeni baada ya wabunge wenzake wa CCM akiwamo Kapteni John Chiligati kumpinga na kumshambulia.
Juzi, Sendeka akichangia hotuba ya makadirio ya Wizara ya Ujenzi alitoa hoja hiyo nzito ya kuitabiria kifo Serikali inayoongozwa na chama chake akiifananisha na mbwa mwitu aliosema kuwa wakipata kitoweo, hunyang'anyana bila kufuata utaratibu wa nani apate kipi, kiasi gani na kwa wakati gani.
“Nimesimama kuomba mwongozo wako kufuatia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli ya mwaka huu inayoashiria na kuweka rekodi ya kuendelea kuonyesha ubaguzi katika ugawaji wa barabara za lami katika nchi hii na kudhihirisha wazi kabisa kwamba Serikali inavyofanya kazi sasa na kwa miaka ya karibuni."
"Inafanya kazi (Serikali) katika mtizamo unaoonyesha kwamba imeanza safari kwenye kifo chake kutokana na sifa moja kubwa nitakayoitaja, kwamba barabara zilizogawanywa katika nchi hii zinatazama maeneo walikotoka viongozi wakubwa na walioko katika vikao vya maamuzi na wanakotoka watendaji wakuu wa Serikali na ukitaka nitatoa mfano."
Kama kuwasha moto kwenye petroli, hoja hiyo ya Sendeka jana ilijibiwa vikali na baadhi ya wabunge wa CCM. Kepten John Komba wa Mbinga Magharibi alisema anashangazwa na wanaopinga bajeti hiyo baada ya kuona kuna miradi ya barabara katika mikoa ya kusini wakati katika maeneo yao kuna lami hadi mazizini na kwenye kumbi za disko.
“Leo imekuwa nongwa watu wa kusini wanapokombolewa kwa barabara mbona tulikuwa na viongozi wa kitaifa kina Kawawa (hayati Waziri Mkuu na Makamu wa Rais), lakini waliona kwanza wasaidie maeneo mengine sasa leo hii kidogo imekuwa nongwa!” alihoji Komba.
Komba alisema safari hii kisungura kidogo kimeelekezwa kusini hivyo ni vyema wabunge wakubali badala ya kupiga kelele.
Chiligati na Aden Rage
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage alisema kwa mara ya kwanza Serikali imesikia kilio cha wakazi wa Mkoa wa Tabora na mikoa ya magharibi.
Alisema mikoa ya magharibi na kusini walikuwa wamesahaulika na sasa wanampongeza Rais Jakaya Kikwete na mawaziri wa ujenzi kwa kutenga fedha kwa ajili ya barabara mbalimbali za kanda hizo.
Mbunge wa Manyoni, John Chiligati akichangia mjadala huo alipinga lugha ya baadhi ya wabunge ya kusema kuna upendeleo katika utekelezaji miradi ya barabara, kwa kutaja kanda za kusini na magharibi.
Chilligati alisema lugha za baadhi ya maeneo kuwa yamependelewa siyo sawa, kwani zitawagawa wananchi.
“Bajeti hii ya mwanzo katika kipindi cha miaka mitano waliotaka mwongozo kama kina Sendeka tuwe wavumilivu, kwani hii ni bajeti ya kwanza,” alisema Chiligati, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara.
Chiligati aliwapongeza mawaziri wa wizara hiyo kwa kazi nzuri wanayofanya na kutolea mfano kukamilika barabara ya lami ya Dodoma- Manyoni, Manyoni-Singida na Singida hadi Mwanza.
Sendeka akosa uvumilivu
Hata hivyo, kauli za wabunge hao zilimwinua tena kitini Sendeka, safari hii akiomba kutoa taarifa tena kwa Spika, akisema wachangiaji zaidi ya watatu wamekuwa wakimtaja jina kuwa anataka kuigawa nchi kutokana na hoja yake jambo ambalo alisema si kweli.
“Niliomba mwongozo kuwa kuna maeneo yamependelewa na tusome ukurasa wa 14 wa kitabu cha bajeti, kuna barabara za Mkoa wa Kilimanjaro zinajengwa kwa lami za kuunganisha vijiji,” hata hivyo kabla ya Sendeka hajamaliza kutaja majina ya barabara hizo Spika Anne Makinda alimtaka aketi na kumpa nafasi Chiligati kuendelea kuzungumza.
Akijibu ombi hilo la Sendeka, Makinda alimweleza mbunge huyo kwamba hoja yake ya jana (juzi) ilikuwa bado haijajibiwa, hivyo ni vyema akasubiri.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kikao cha Bunge juzi, George Simbachawene alisema jana kwamba hoja hiyo ya Ole Sendeka huenda ikafikishwa kwanza katika kikao cha Wabunge wa CCM kabla ya kutolewa maelezo: “Mimi nimemkabidhi Spika nadhani itapelekwa kikao cha wabunge wa CCM.”
Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge jana, Sendeka alisema wabunge ambao wanapinga hoja yake wanaweza kuwa wanakabiliwa na matatizo mawili, kwanza inawezekana hawajamwelewa au wanajipendekeza serikalini.
Alisema katika hoja yake, hana ugomvi na barabara kuu za Katavi, Mtwara, Songea, Iringa na nyingine zote ambazo zinaunganisha mikoa na nchi jirani.
“Tatizo langu mimi ni barabara za lami za kuunganisha kijiji hadi kijiji au kata na kata ambazo zimetengewa fedha mwaka huu wakati kuna maeneo mengi hakuna hata barabara moja ya lami kama Simanjiro na Kiteto,” alisema.
Alisema anachotaka ni kutolewa fursa sawa katika kugawana rasilimali za nchi na siyo watu wachache kupendelewa.Mbunge huyo alisisitiza kwamba dola iliyoanza safari ya kuelekea kwenye kifo utaona viongozi wanafanyakazi kwa staili ya mbwa mwitu.
“Hapa kinachoonekana kila mwenye nafasi ananyofoa nyama kwa maslahi yake, sasa hii ni hatari na lazima tuseme,” alisisitiza Ole Sendeka.
Habari hii imeandikwa na Musa Juma na Habel Chidawali, Dodoma na Fidelis Butahe, Dar es Salaam.
|
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa