Tuesday, August 2, 2011

Kujivua gamba sasa mwisho Septemba






Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
KAMATI Kuu ya CCM (CC) imewataka wanachama wake wengine wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi kuwajibika kabla ya Septemba mwaka huu, vinginevyo wataumbuka.

Onyo hilo la CC linakuja baada ya kupitia kwa siku 90 zilizotangazwa Aprili mwaka huu na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), ikiwataka watuhumiwa hao kujiondoa wenyewe kabla ya siku hizo vinginevyo wataondolewa.

Hadi sasa, ni aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ambaye amejizulu hatua ambayo imeridhiwa na kupongezwa na CC.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema chama kimeridhia uamuzi wa kujihudhulu kwa Rostam na kuongeza kwamba hiyo ni sehemu ya uamuzi wa chama ambao wengi wanatakiwa kuufuata.

“Ni heri kupoteza jimbo au kata halafu tukarudi kwenye uchaguzi maana ndiyo njia pakee ya kukisafisha CCM kuliko kuendelea kung’ang’ania wachafu kwenye chama chetu.”
Alisema CCM hakioni tabu ya kurudi kwenye mchakato wa uchaguzi katika majimbo na kata katika eneo lolote kama itabidi kwani wananchi wanatambua nini mustakabali wa chama chao na kutamba: “Tukirudi huko bado tutashinda.”


“Nasisitiza hata ninyi nendeni mkasome katika Biblia imeandikwa kuwa, kama kidole kitakukosesha amani ni bora kukikata ili mwili uwe salama kuliko kukiacha mwisho wa siku ikawa balaa. Hivyo nasi tuko tayari kuwatimulia mbali hao wanaotuhumiwa kwa mambo mbalimbali ili chama kibaki salama.’’
Nape alisema CCM kiko tayari kuwatimua muda wowote watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi na mambo mengine lakini, akatahadharisha kuwa hakiwezi kufanya hivyo kwa sasa bali kinasubiri kikao cha Nec ambacho kitakutana Septemba mwaka huu.

Alisema chama siku zote kimekuwa kikisitiza suala la maadili na kuongeza kwamba hiyo ni ajenda ya kudumu kwa kila kiongozi pamoja na wanachama wake.Alisema CCM hakipo tayari kuwaacha wanachama wake ambao wanalalamikiwa waendelee kutamba na kuonya kwamba kiama chao kinakuja Septemba Nec itakapokutana.

“Samaki ana nguvu akiwa ndani ya maji tu, ukimtoa hakuna kitu tena wala hana ujanja na hivyo hata hawa wanatusumbua wakiwa ndani ya chama lakini tukiwatimua hawana mahali pa kuegemea,’’ alisema na kuongeza:
“Hakuna maarufu kuliko chama. Wanaotaka tuwatimue tutafanya hivyo na chama kitabaki imara hivyo hivyo na huenda kikawa imara zaidi maana tunalenga kujijenga chama chetu wakati wote.’’

Malalamiko ya ziara za mikoani
Akijibu hoja kuhusu malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wanaCCM na viongozi kuwa sekretaieti ya chama hicho imekuwa ikifanya mambo ambayo hayakuamuliwa kwenye vikao husika, Nape alisema huo ni uongo.Alisema CC imepongeza kazi nzuri inayofanywa na sekretarieti ikiwa ni pamoja na mikutano hiyo ambayo imekuwa ikifanya kwenye mikoa mbalimbali na kusema: “Kamati imeagiza wakaze buti bila ya kuyumba.”

Nape alisema kama sekretarieti ingekuwa hairidhishwi na mikutano inayofanyika sehemu mbalimbali isingekubali kuwapongeza na badala yake ingewazuia... “Kitendo cha kutaka mikutano iongezeke zaidi ni ishara ya kazi nzuri iliyofanywa.”

Mchakato wa uchaguzi Igunga
Nape alisema jambo jingine ambalo lilijadiliwa na CC ni pamoja na kuweka ratiba ya mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho kwa ajili ya kumpata mgombea ubunge katika Jimbo la Igunga kupitia CCM.“Tulichokubaliana ni kwamba kule Igunga mchakato wote tutawachia wenyewe watu wa Mkoa wa Tabora pamoja na Wilaya ya Igunga lakini, sisi taifa tutakwenda kuongeza nguvu ya ushindi na tuna imani tutashirikiana na Rostam katika kufanikisha ushindi huo kwa kuwa alisema atabaki kuwa mwanachama wetu mwaminifu,” alifafanua Nape.

Umeme na migogoro ya ardhi

Katibu huyo mwenezi wa CCM alisema suala la migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini lilijadiliwa kwa kina na CC ambayo iliiagiza Serikali kushughulikia migogoro hiyo ikiwa ni pamoja na ile ya sehemu za migodini na kuimaliza kwa muda muafaka.

Alisema Kamati Kuu imeagiza kuwa migogoro hiyo ishughulikiwe katika ngazi ya mikoa kabla ya kupelekwa ngazi ya Taifa.Aidha, CC imeitaka Serikali kuja na majibu ya uhakika siku itakaporudisha tena bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kukidhi mahitaji ya Watanzania na kufufua matumaini yao yaliyoanza kutoweka.

Kamati ya maadili.
Kamati Kuu imefanya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Maadili kwa kuwateua Abdulrahman Kinana na Pindi Chana. Wajumbe wengine kutoka Zanzibar hawakutaja mara moja.


No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa