MBUNGE wa Jimbo la Rungwe Mashariki ambaye pia ni Waziri wa Maji na umwagiliaji Prof, Mark Mwandosya, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Benson Mpesya na Mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi wametajwa kuwa vinara wa siasa za mkoa wa Mbeya ambapo mpaka sasa wanauhakika wa zaidi ya asilimi 80 kurejea kuongoza majimbo yao .
Tathimini hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa wanasiasa wengi kujitokeza katika majimbo mbalimbali ya mkoa huo na kuonesha nia zao za kuweza kutinga katika kinyag’anyiro cha Ubunge majimboni mwao.
Jimbo la Rungwe linaloongozwa na Prof,Mwandosya amejitokeza mwanasiasa mchanga Stephen Mwakajumilo ambaye ni mtumishi wa Benki kuu tawi la Mbeya ambaye hata hivyo duru za siasa jimboni humo zimeeleza kuwa hataweza kutoa ushindani kwa Mwandosya ambaye amepewa jina la Baba wa Mbeya.
Kwa upande wa Jimbo la Mbeya Mjini linaloongozwa na Benson Mpesya tayari wanasiasa zaidi ya saba wamejitokeza akiwemo Mbunge wa kuteuliwa Tom Mwang’onda na Frank Mwaisumbi ambao wote ni wanyakyusa na jimbo hilo linawapiga kura wengi kabila la wasafya ambao ni watani wao.
Kutokana na uwingi wa wapiga kura kuwa wasafya katika jimbo hilo imeelezwa kuwa Mpesya ana asilimia kubwa ya kunyakua kiti hicho kwa mara nyingine kwasababu ya ukabila na utii wa machifu wa Jimbo hilo.
Jimbo la Mbeya Vijijini linakabiliwa na siasa za ajabu ambapo mpaka sasa zaidi ya wanachama nane wa CCM wameonesha nia ya kumvaa Mchungaji Luckson Mwanjale.
Baadhi yao ni Petro Mwashusa, Maiko Mponzi, Jeremiah Mwaweza, Kasim Mzumbe, Dickson Sinkwembe na Andrew Sayile na kati ya hao Petro Mwashusa, Maiko Mponzi na Andrew Sayile wanahitai kujaribu tena bahati zao baada ya kubwagwa katika chaguzi kuu zilizopita kupitia kamati ya siasa ya wilaya hiyo.
Licha ya wanachama hao wote, Mwanjale atakabiliana na upinzani mkali kutoka wanachama wenzake akiwemo Kasim Mzumbe, Andrew Sayile na Alan Mwaigaga huku Mwanasiasa machachari kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Sambwee Shitambala akimsubiri kwa hamu mgombea yeyote atakayepitishwa kupeperusha bendera ya CCM jimboni humo.
Kwa upande wa Jimbo la Mbozi Mashariki linaloongozwa na Mbunge machachari Godfrey Zambi bado upinzani hautishi ingawa duru za siasa zikendelea kumtaja Aloyce Mdalavuma kuwa anaweza kuleta mvuto ndani ya chama hicho jimboni humo licha ya mbunge Zambi kuendelea kuwa na asilimia kubwa ya kurejea na kuongoza tena jimbo hilo .
Licha ya Aloyce Mdalavuma, pia wanachama kadhaa wamejitokeza na kutangaza nia zao akiwemo Willium Kapenjama na Mganga mkuu wa hospitali ya Mission ya Mbozi Dr. Charles Mbwanji.
Mbozi Magharibi ni jimbo ambalo kwasasa ni linaitia tumbo joto CCM kwa kuhofia jimbo hilo kuchukuliwa na wapinzani hususani chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema)
Jimbo hilo ambalo kwa sasa linaongozwa na Lucas Suiame limeelezwa kuwa ni kati ya majimbo yaliyowekwa rehani na sasa Mbunge huyo anawatazama wanaCCM wenzake ambao wameelezwa kuwa tayari wamejitokeza jimboni humo akiwemo mbunge wa zamani wa jimbo hilo Eliakim Simpasa, Aglipa Senka na Aden Mwakyonde.
Jimbo la Ileje linaloongozwa na mbunge Gideon Cheyo tayari makada wa CCM wamejitokeza akiwemo Aliko Kibona, Frank Kibona, Victory Kanama, Ulimbakisya Shimwela, Pilika Fumbo, Dr, Mbwaga, Lwakege Minga na wengine waliotajwa kwa jina moja moja akiwemo Mwenigole, Mkondya na Msongwe.
Jimbo la Kyela linaloongozwa na Dr , Harrison Mwakyembe ni jimbo pekee linalotarajiwa kujazwa mashushushu kwa ajili ya usalama wa jamii ya wananchi wa Kyela katika kura za maoni kutokana na hali ya uhasama wa makundi yanayoasimiana wilayani humo.
Baadhi ya makada wa CCM waliojitokeza na kuonesha nia zao za kuwania nafasi ya ubunge Jimboni humo ni pamoja na Elias Mwanjala na George Mwakalinga.
Majimbo mengine yaliyobaki likiwemo Jimbo la Mbarali linaloongozwa na Esterina Kilasi, Songwe linaloongozwa na Guido Sigonda na Jimbo la Lupa wabunge wake wameelezwa kuwa katika mtego mzito wa kuenguliwa katika kura za maoni.
Hata hivyo duru za siasa mkoani hapa zimetanabaisha kuwa mbunge wa Jimbo la Rungwe Magharibi Dr , David Mwakyusa anategemea zaidi upako wa chama chake kutokana na hulka yake ya kutoegemea katika makundi yanayoendelezwa katika mkoa wa Mbeya.
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa