Sunday, May 2, 2010

MEI MOSI YA VITUKO TANZANIA!!!

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam William akizungumza na wafanyakazi katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dar es salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam William Lukuvi (katikati) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani akishiriki kuimba wimbo wa Mshikamano Daima pamoja na viongozi wa vyama vya wafanyakazi ambavyo havishiriki katika mgomo ulioitishwa na Shrikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA)

Wafanyakazi kutoka Mashirika na Taasisi mbalimbali na vyama vya wafanyakazi ambavyo havishiriki katika mgomo ulioitishwa na Shrikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) wakiwa kwenye maadamano kuelekea viwanja vya Mnazi mmoja kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani inayoadhimishwa leo kitaifa jijini Dar es salaam.

Maandamano yakiendelea kuelekea viwanja vya mnazi mmoja

 

 

VITUKO VYA  TUCTA MEI MOSI 2010 HAIJAWATOKEA

 

 

Na Wansblog wetu

 

KWA mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, maadhimisho ya sherehe za Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) zimefanyika kitaifa jijini Dar es Salaam kwa mafungu mawili baada ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) kugoma katakata kuwaalika viongozi wa kitaifa  akiwemo Rais Jakaya Kikwete.

Sherehe hizo ambazo kitaifa zilifanyika katika Uwanja wa Uhuru na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa bila kuwepo viongozi wa serikali huku  mgeni rasmi akiwa Rais wa TUCTA, Omar Ayoub Juma.

Vyama vilivyokataa kujiunga na TUCTA, vimeanzisha chama kipya cha wafanyakazi kutoka katika sekta ya fedha, viwanda huduma za benki, maji, biashara na viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo (FIBUCA).

Katika sherehe hizo ambazo baadhi ya watu walizielezea kuwa ni kituko cha karne na huenda taifa likaingia kwenye mtikisiko mkubwa wa uchumi kama wafanyakazi hao  wataanza  kugoma Mei 25 kama walivyoahidi.

Akiwahutubia maelfu ya wafanyakazi waliohudhuria sherehe hizo, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Omar Ayoub Juma, alisisitiza  kuwa  mgomo wao uko palepale kama serikali haitokubali kuwaongezea mishahra pamoja na kupunguza makato ya fedha zinazopelekwa katika mifuko ya pensheni.

Katika kundi la pili ambalo lilisherehekea sherehe hizo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, lilishuhudiwa kuwa na watu wachache huku Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya akishindwa kutokea dakika za mwisho kama alivyoahidi juzi.

Taarifa za Waziri Kapuya, kuongoza maandamano hayo, ilitolewa juzi jioni na Idara ya Habari (MAELEZO) kuwa angeongoza  maandamano ya wana wa vyama vya wafanyakazi ambavyo havishiriki mgomo uliyoitishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Taarifa hiyo ilisema, Waziri Kapuya angeongoza maandamano hayo kuanzia  eneo la Mamlaka  ya Majisafi na Majitaka (DAWASCO) eneo la Gerezani na kuwa yangeshirikisha wafanyakazi kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), NMB, Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

Baada ya kukosekana kwa Waziri Kapuya, maandamano hayo yalipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi.

Habari za kuaminika ambazo Tanzania Daima Jumapili, ilizipata zinasema, Waziri Kapuya, alitakiwa kuwa mgeni rasmi tena katika sherehe hizo kwenye Uwanja wa Uhuru, ingawa nako hakuonekana.

Hata hivyo vyanzo vya habari vilidai kuwa inawezekana Waziri Kapuya alishindwa kutokea kwa sababu ya kutokuwa na majibu sahihi ya tishio la mgomo wa wafanyakazi unaotarajiwa kufanyika kuanzia kesho kutwa.

Akiwahutubia katika kilele cha Mei Mosi viwanja vya Mnazi Mmoja wafanyakazi wa chama kipya cha wafanyakazi kutoka katika sekta ya fedha, viwanda huduma za kibenki, maji, biashara na viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo (FIBUCA), Lukuvi aliitaka (TUCTA) na vyama vingine kutafuta suluhu ya namna nyingine ya kudai maslahi yao kuliko kufanya mgomo.

Lukuvi alisema, njia pekee ni kukaa mezani ili hoja hizo zijadiliwe na madai husika yapatiwe uvumbuzi badala ya kuandaa mgomo.

Naye Kaimu Rais wa FIBUCA, Doscar Vuhahula, alisema chama kinaamini uhusiano mzuri kati ya waajiri na wafanyakazi kazini ni nyenzo muhimu katika mpango mzima wa ukuzaji tija.

Alisema FIBUCA pamoja na uchanga wake, leo imesherehekea na vyama vingine nje ya TUCTA na kuthibitisha kwamba umuhimu wa ushirikiano wa pande zote kwa nia ya kuinua tija na kuongeza pato la taifa na mfanyakazi kwa jumla.

Mkoani Mbeya, wafanyakazi wa serikali, mashirika ya umma na sekta binafsi jana waliungana pamoja na kula kiapo cha utii cha kubariki maandamano ya mgomo wa kitaifa utakaofanyika Mei 5 ili kuishinikiza serikali kuboresha mishahara kwa watumishi wa umma inayolingana na hali halisi ya maisha.

Kiapo hicho cha utii kiliwajumuisha wafanyakazi wote wanaotoka kwenye vyama vyao ambavyo ndivyo vinavyounda Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi  Nchini (TUCTA), maadhimisho ambayo yalifanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine.

Katika hali ya kuonyesha wamedhamiria kuanza mgomo usiokuwa na kikomo, wote kwa pamoja walisimama huku wakiwa wamenyoosha mikono juu na kulishwa kiapo kilichotolewa na viongozi wa TUCTA ngazi ya mkoa.

Sherehe hizo hazikuhudhuriwa na mgeni yeyote kutoka serikali ya mkoa, ambapo mgeni aliyepokea maandamano hayo alikuwa mjumbe wa Baraza  Kuu la Taifa (TUCTA), Joachim Massami.

Huko mkoani Iringa, sherehe hizo  zilionekana kuzorota baada ya wafanyakazi wachache pamoja na wananchi kujitokeza kwenye Uwanja wa Samora.

Baadhi ya watu waliohudhuria sherehe hizo, walitumia maadhimisho  hayo kuimba nyimbo za kejeli dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na  kushabikia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kumwimba mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kama rais wao mtarajiwa katika uchaguzi mkuu ujao.

Maadhimisho yalihudhuriwa ma mgeni rasmi mjumbe wa TUCTA taifa  kutoka Chama cha RAAWU, Lameck  Chengula,  ambaye alihutubia wananchi wachache tofauti na ilivyokuwa mwaka jana.

 


No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa