![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiblexFLu18bi44CRETg4NObdS5na-RP6C_KuBgP54_PxdZPn3UsHQY-Bd9Z5zh8frDGfqXNgXkNzCkYsoCpSzKDaSNnl5viFuL2_6Mp5HQ4XeXExztnj386y3EdZeZOZFElkveeXqnAfDO/s400/Ndalichakoz.jpg)
JUMLA ya watahiniwa 55,764 sawa na asilimia 88.86 ya watahiniwa waliofanya mtihani wa Kidato cha Sita mwaka huu, wamefaulu ambapo idadi ya wasichana waliofaulu ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya wavulana.
Jumla ya wasichana 21,821 sawa na asilimia 90.39 ya wasichana waliofanya mtihani huo wamefaulu, wakati wavulana waliofaulu ni 33,943 sawa na asilimia 87.90 ya wavulana waliofanya mtihani huo.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako alisema idadi ya watahiniwa waliofaulu imeongezeka kwa 10,048 wakati asilimia ya ufaulu imepungua kwa asilimia 0.78 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2009 ambapo waliofaulu ni 45,716 sawa na asilimia 89.64.
Alisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 45,217 , sawa na asilimia 93.76 ya waliofanya mtihani na watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 10,547 sawa na asilimia 74.57.
Mwaka 2009 watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 9,244 sawa na asilimia 74.84 ya waliofaulu. Hivyo idadi ya waliofaulu imeongezeka kwa watahiniwa 1,300 ikilinganishwa na mwaka jana.
Ingawa wasichana wanawaburuza wavulana kwa idadi ya waliofaulu, kwa mujibu wa matokeo nafasi ya wanafunzi kumi bora kitaifa inashikiliwa na wavulana waliokuwa wanasoma shule za sekondari za wavulana ambapo Sekondari ya Mzumbe inang'ara kwa kutoa wanafunzi bora wanne kati ya 10.
Walioshika nafasi ya kwanza hadi ya kumi kitaifa na shule zao kwenye mabano ni Japhet John (Ilboru), Manyanda Chitimbo (Kibaha), Hassan Rajab (Minaki), Samuel Killewo (Feza Boys), Abdullah Tahel, Steven Elias na Paul Nolasco wote wa Mzumbe Sekondari, Alexander Marwa (Tabora Boys) Ephraim Swilla (Mzumbe) na Benedicto Nyato (Tabora Boys).
Matokeo hayo, kwa kiasi fulani yamepunguza utawala wa shule za binafsi katika mitihani ya kidato cha nne na cha sita katika siku za hivi karibuni.
Ndalichako alisema kundi hilo la wanafunzi kumi bora kitaifa linawakilisha pia nafasi ya wavulana 10 waliofaulu vizuri kitaifa.
Wasichana walioshika nafasi ya kwanza hadi ya kumi kitaifa ni Jackline Seni (Marian Girls) Khadija Mahanga (Marian Girls) Cecilia Ngaiza (St. Joseph Ngarenaro) Esther Mlingwa, Perpetua Lawi, Lilian Kakoko wote wa Marian Girls Sekondari, Gerida John na Subiri Omary kutoka Dakawa Sekondari, Ruth Pendael (Morogoro) na Elaine Kijoti (Ashira).
Alisema kwa kuangalia ubora wa ufaulu kwa madaraja waliyopata watahiniwa wa shule katika mtihani huo, unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 39,625 sawa na asilimia 82.17 wamefaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu, wakiwamo wasichana 15,650 sawa na asilimia 82.22 na wavulana ni 23,975 sawa na asilimia 82.13.
Ndalichako alisema kwa upande wa shule kumi bora zimegawanyika katika makundi mawili kulingana na idadi ya watahiniwa.
Kundi la kwanza lina shule 337 zenye watahiniwa 30 na zaidi ambapo kundi la pili lina idadi ya shule 81 zenye watahiniwa pungufu ya 30.
Alizitaja shule kumi bora katika kundi la shule zenye watahiniwa 30 na zaidi ni Marian Girls (Pwani) Mzumbe (Morogoro) Uru Seminari (Kilimanjaro), Kibaha (Pwani), Feza Boys (Dar es Salaam), Tabora Boys (Tabora) Tukuyu (Mbeya), Kifungilo (Tanga), Ilboru (Arusha) na Malangali (Iringa).
Kwa upande wa shule kumi bora katika kundi la shule zenye watahiniwa chini ya 30 ni Seminari ya Rubya (Kagera), Seminari ya Maua na Seminari ya Mtakatifu James (Kilimanjaro), Mtakatifu Joseph Kilocha (Iringa), Seminari Same (Kilimanjaro), Usongwe (Mbeya), Seminari ya Mtakatifu Petro (Morogoro), Vituka (Dar es Salaam) na Vwawa (Mbeya).
Ndalichako alizitaja shule kumi zilizoshikilia mkia katika kundi la shule zenye watahiniwa 30 na zaidi kuwa ni High-View International (Unguja) Fidel Castro (Pemba), Sunni Madressa (Unguja), Neema Trust (Dar es Salaam) Ufundi Mtwara (Mtwara), Muheza (Tanga), Tarakea (Kilimanjaro) Uweleni (Pemba), Arusha Modern (Arusha) ya kumi kutoka mwisho ni Maswa Girls (Shinyanga).
Katika kundi la shule zenye wanafunzi pungufu ya 30, ya mwisho kabisa ni Nkasi (Rukwa), Mount Kilimanjaro (Kilimanjaro), Mbarali Preparatory (Unguja), Lilian Kibo (Dar es Salaam), Ghomme (Dar es Salaam), Adolec (Kagera), Mzizima, Dar es Salaam Christian Seminary na EDP Royal za Dar es Salaam na Sekei ya Arusha.
Ndalichako alisema pia Baraza hilo limesitisha kutoa matokeo ya mtihani wa mwaka huu kwa watahiniwa 484 ambao hawajalipa ada ya mtihani na matokeo yao yatatolewa mara watakapolipa ada.
Pia Baraza la Mitihani limesitisha matokeo ya watahiniwa 49 waliofanya mtihani huku wakiwa na sifa zenye utata hadi hapo watakapowasilisha vyeti vyao halisi vya kidato cha nne kwa ajili ya uhakiki pamoja na vielelezo vya kuthibitisha uhalali wao.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa