Wednesday, April 28, 2010


   


 

WAZIRI MKUU ATAKA SINGIDA WACHANGAMKIE KILIMO, MIFUGO NA UFUGAJI NYUKI

 


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema mkoa wa Singida una fursa nyingi za kilimo na ufugaji nyuki ambazo zikitumiwa vizuri zitasaidia kuinua pato la mwananchi wa kawaida wa mkoa huo na pato la Taifa.

 

Amesema hatua hiyo haiwezi kufikiwa kama viongozi wa mkoa huo na hasa walioko katika Halmashauri hawatajipanga na kuapa kuwasaidia wananchi waondokane na hali ya umaskini inayowazunguka kila kukicha.

 

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Aprili 27, 2010) wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Singida na ya wilaya ya Manyoni katika ukumbi wa Misheni ya Lusilile ulioko wilayani Manyoni.

 

"Mkoa huu una una hekta milioni nne zinazofaa kwa kilimo, mifugo, ufugaji wa samaki na ufugaji wa nyuki... kati ya hizo hekta milioni 1.1 zinafaa kwa kilimo lakini nyie mnalima hekta 280 tu, sawa na asilimia sita ya eneo lote," alisema.

 

Alisema kama mkoa huo utaendelea kuwaacha walime kwa kutumia jembe la mkono, hakuna jinsi watajikomboa na umaskini. Aliwataka watendaji wa Halmasharu za mkoa huo, watumie nafasi walizonazo kujiuliza wanawasaidia vipi wana Singida kutumia wanyama-kazi kwenye kilimo.

 

"Watu wa Halmashauri mnapaswa kujiuliza mmejipanga vipi kutumia mifugo ya mkoa huu ili kuongeza eneo la uzalishaji (acrage), lazima mfanye kazi ya kuhimiza matumizi ya wanyamakazi na powertiller," alisema.

 

Alisema katika kuhimiza matumizi ya power tillers wanakabiliwa na changamoto ya kuanzisha vituo vya matengenezo ya power tillers hizo (after-sale service centres/

mechanisation centres) na kuhimiza mfumo wa 'block-farming' ili iwe rahisi kulima eneo kubwa kwa wakati mmoja.

 

Alisema itabidi maafisa husika wawahamasishe wakulima waunganishe mashamba yao (block farming) ili kuepuka powetillers hizo kulima eneo dogo na kuhama kwenda kutafuta shamba la mkulima mwingine eneo jingine.

 

Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bw. Parseko Kone alimweleza Waziri Mkuu kwamba mkoa huo unatarajia kuzalisha tani 652,472 za mazao ya chakula na tani nyingine 272,915 za mazao ya biashara katika msimu huu wa kilimo.

 

Kuhusu jitihada za mkoa kuhifadhi mazingira, Bw. Kone alisema vijiji 30 vya wilaya ya Singida vimeweza kupanda miti ya asili katika hekta 275,700 ikiwa ni jitihada za mkoa huo kuhifadhi uoto wa asili ambao unastahimili hali ya hewa ya nyanda kame.

 

Pia Waziri Mkuu alizindua filamu inayohusu uhifadhi wa mazingira iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambayo imelenga kuhimiza wakazi wa mkoa watunze misitu kwa ajili ya kufuga nyuki na kuhifadhi unyevu. Mkoa huo unakabiliwa na biashara haramu ya uchomaji mkaa na uuzaji mbao holela hali inayochangia ukataji miti hovyo.

 

Kesho Jumatano, Aprili 28, 2010 Waziri Mkuu atazuru wilaya ya Singida ambako atakagua mradi wa umwagiliaji maji kwa njia ya matone katika shamba lililoko Mkiwa; atazindua hosteli ya wasichana ya shule ya sekondari ya Issuna na kuhutubia mkutano wa hadhara. Baadaye ataenda kijiji cha Msungua ambako atafungua kiwanda kidogo cha kusindika ngozi na kingine cha kusindika maziwa.

 


 
 
 



No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa