WASTAAFU EAST AFRIKA WATINGISHA MAHAKAMA KUU
MAMIA ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki jana walifanya vurugu kubwa katika Mahakama Kuu Dar es Salaam wakati walipokwenda mahakamani hapo kusikiliza kesi ya madai ya mafao yao.
Wastaafu hao walikuwa wamepandwa na jazba kubwa huku mama Habiba Kirumbi alikipiga mayowe wakati wenzake wakivutana na askari polisi waliokuwa wakijaribu kuwatuliza, huku mzee mmoja akimkwida askari polisi.
Wastaafu hao ambao wamekuwa wakisotea malipo ya mafaoa yao hayo kwa miaka mingi tangu kuvunjika kwa jumuiya hiyo mwaka 1977, walifanya vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa 2:30 wakipinga maelekezo ya Mahakama Kuu ya kuwataka wakae pamoja na wawakilishi wao wa zamani katika kupata haki ya madai yao mahakamani.
Wakizungumza kwa jazba, wastaafu hao walidai hawawataki wala hawawatambui wawakilishi hao saba huku wakiwatuhumu kuwa wanatumiwa na serikali katika kukwamisha kupata haki zao.
Licha ya askari polisi wa mahakamani hapo kufanikiwa kuwazuia wastaafu hao, wasiingie ndani ya mahakama ili kuwatafuta wawakilishi wao wa zamani waliokuwa wamehifadhiwa ndani ya mahakama hiyo, polisi walishindwa kuwatoa nje ya eneo la mahakama hiyo na badala yake askari hao pamoja na watumishi wengine wa mahakama walibaki wametanda katika lango la kuingilia mahakamani.
Saa 4:45 Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kati Wilbroad Mutafugwa aliwasili mahakamani hapo na kujaribu kuwatuliza huku akiwashari waache vurugu hizo na badala yake kama wana malalamiko yao, wafuate taratibu za kisheria kutoa malalamiko yao.
Kama kuna upande ambao haujaridhika kuna taratibu za kisheria za kupinga kwa kutumia mawakili wenu na kuandika hoja zenu. Utaratibu huu mnaotumia wa kupiga kelele hautasaidia. Hii ni ofisi ya serikali na mahakama haishughulikii kesi yenu tu bali ziko nyingi zinazopaswa kushughulikiwa kwa utulivu, lakini hivi mnazuia shughuli nyingine zisiendele," alisema Mutafugwa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya vurugu hizo, Msajili namba mbili wa Wilaya wa Mahakama Kuu Lameck Mlacha alisema awali wastaafu hao walifungua kesi ya madai namba 93 ya mwaka 2003, wakiwakilishwa na Karata Ernest na wenzake sita kwa niaba ya wadai wote 31,831, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG).
Mlacha alisema Septemba 21, 2005 ilitolewa hukumu ya maridhiano (conset judgement) kati ya pande hizo mbili (walalamikaji na mlalamikiwa) ambapo walikubaliana kuwa walipwe Sh117 bilioni.
Msajali huyo wa Mahakama Kuu aliongeza kuwa baadaye wastaafu hao hawakuridhika na hukumu hiyo, hivyo kupitia kwa mawakili wao, Jothan Lukwaro na Biamungu, wastaafu hao waliomba mapitio ya hukumu hiyo, lakini maombi yao yalitupiliwa mbali na Jaji Catherine Urio.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa