NI PROF SAITOTI, NAIBU WAKE NA MAOFISA WA JUU WA SERIKALI YA KENYA
Mwandishi wetu, Nairobi
WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kenya, Profesa George Saitoti na Naibu wake, Orwa Ojode pamoja na maofisa wengine watano, wamefariki dunia baada ya helikopta ya Polisi waliyokuwa wamepanda kuanguka msituni.
Profesa Saitoti ambaye ni mmoja wa mawaziri waandamizi katika Serikali ya Rais Mwai Kibaki na mmoja wa wanasiasa wakongwe wanaoheshimika Kenya, aliwahi pia kuwa Makamu wa Rais kati ya mwaka 1976 hadi 1979 na alishatangaza kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Jana, Saitoti ambaye ni mchumi aliyebobea na bingwa hisabati, akiwa na naibu wake na maofisa hao wa wizara walipata ajali wakati wakielekea katika eneo la Sotik kwa ajili ya mkutano wa usalama.
Ajali hiyo ilitokea asubuhi katika eneo la Kibiku, karibu na Mji wa Ngong, kilometa 20 kutoka Nairobi.
Taarifa zilisema helikopta hiyo ya polisi ilikuwa imebeba abiria saba ambao wote walifariki dunia huku miili yao ikiharibika vibaya.
Profesa Saitoti alikuwa Mbunge wa Kajiado tangu mwaka 1988 hadi mauti yalipomkuta.
Mashuhuda
Walioshuhudia ajali hiyo, walisema waliona helikopta hiyo ikizunguka angani kabla ya kuanguka katika Msitu wa Ngong.
Baada ya kutokea ajali hiyo, polisi walilizingira eneo la ajali huku Kamishna wa Polisi, Mathew Iteere ambaye na yeye alikuwapo katika eneo hilo akisema atatoa taarifa kamili kuhusiana na ajali hiyo kwa waandishi wa habari baadaye.
Ajali hiyo imetokea ikiwa ni miaka minne tu tangu kutokea kwa ajali nyingine ya helikopta Juni 10, 2008 ambayo ilisababisha vifo vya mawaziri wawili.
Mawaziri walipoteza maisha katika ajali hiyo ni pamoja na Kipkalya Kones na Lorna Laboso.
Mambo muhimu kwa Saitoti
Saitoti ambaye alizaliwa mwaka 1945 kabla ya kupatwa na mauti hayo, aliwahi kutoa wito kwa raia wa Kenya kuwachagua viongozi ambao ni watendaji wa kazi bila ya kuangalia kabila, rangi na dini.
Kiongozi huyo ambaye kabla ya kuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, alikuwa Waziri wa Fedha na pia Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia kati ya mwaka 1990 hadi 2001, alisema Wakenya wanapaswa kuwachunguza viongozi kabla ya kuwachagua ili kuepuka kuchagua wala rushwa.
Profesa Saitoti alibainisha kuwa kuna haja ya wanasiasa wote kutowagawa Wakenya wakati wa kampeni zao ili kuepuka kile kilichotokea katika uchaguzi 2007.
Alisema kutokana na uzoefu wake, yeye ndiye aliyekuwa na uwezo wa kumrithi Rais Mwai Kibaki.
“Mataifa yote yanatuangalia sisi sasa hivi, nini tunachokifanya wakati huu na nini kitakachotokea wakati wa uchaguzi mkuu mwakani,” alisema.
Marehemu Saitoti ndiye aliyekuwa akiongoza jeshi la nchi hiyo kwa ajali ya kuwatafuta wafuasi wa kundi la Al Shabab, Somalia
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa