Friday, May 4, 2012

Polisi wapata mafunzo kukanyaga moto


MAOFISA wa ngazi za juu katika Jeshi la Polisi nchini wakiongozwa na Mkuu wa Jeshi hilo (IGP), Said Mwema jana walihitimu mafunzo ya kujijengea uwezo na ujasiri kwa kukanyaga moto.Mbali na IGP Mwema, maofisa wengine wa polisi walioshiriki zoezi hilo jana ni Mkurugenzi wa Upelelezi nchini (DCI), Robert Manumba na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Mafunzo hayo yanayoelezwa kuwa yataendelea kwa siku mbili mfululizo, yalifanyika katika bwalo la polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Katika mafunzo hayo yanayotolewa na taasisi ya Peak Performance ya jijini Dar es Salaam, maofisa hao wa polisi  walipita mmoja baada ya mwingine juu ya moto uliokuwa ukiwaka wakiwa wamevua viatu.
Mafunzo hayo ambayo yameshirikisha viongozi wa juu wa jeshi hilo kuanzia cheo cha kamishna wasaidizi (ACP) na makamishna wengine, pia yatashirikisha viongozi wengine na askari nchini kote.
Imeelezwa kuwa mafunzo hayo ni ya kujijengea uwezo na ujasiri kwani kupita kwenye moto ni kuonyesha hakuna linaloshindikana likiamuliwa kufanyika.
Taarifa ya jeshi hilo imeeleza kuwa  madhununi ni kuhakikisha askari wote wa jeshi hilo wanapatiwa mafunzo ya aina hiyo kwa awamu kulingana na uwezo wa kifedha ndani ya jeshi la polisi.

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa