Rais wa Chama cha Madaktari nchini (MAT), Dk Namala Mkopi (kushoto), akiwatangazia waandishi wa habari kuanza rasmi kwa mgomo wa madaktari nchi nzima baada ya kumalizika mkutano wa madaktari uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari, Dk Godbless Charles. Picha na Fidelis Felix UPATIKANAJI wa huduma za afya nchini uliendelea jana isipokuwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza na Amana Ilala, Dar es Salaam huku Muhimbili huduma zikitolewa kwa kusuasua.Jana, ilikuwa siku ambayo madaktari hao walitangaza kuanza mgomo nchi nzima wakishinikiza madai yao ya kutaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya wajiuzulu au wawajibishwe licha ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwasihi wabadili msimamo huo kwa maslahi ya wananchi.
Hata hivyo, akizungumzia na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa madaktari uliofanyika Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi alisema wamekubaliana kurejea kwenye mgomo kuanzia jana mchana hadi hapo dai lao la msingi la kuwajibika au kuwajibishwa kwa mawaziri hao litakapotekelezwa.
“Madaktari wanasikitika kutoa taarifa kuwa sasa wanarejea kwenye mgomo na utakuwa kwa nchi nzima hadi dai lao litakapotekelezwa. Wanawaomba wananchi kuelewa kuwa lengo lao ni kutaka kuboresha huduma za afya nchini. Uzorotaji wa huduma za afya nyote mnaufahamu, hata wakilazimishwa hakuna kitakachoendelea tunaomba nia ya madai yetu yasipotoshwe.”
Alisema hayo akipinga kauli ya Waziri Mkuu, Pinda aliyoitoa juzi kwamba madai hayo ya kutaka Dk Mponda na Dk Nkya wang’olewe ni mpya na kusema imewafanya pia watilie shaka utekelezwaji wa madai mengine.
“Madaktari wamesikitishwa na kauli ya Waziri Mkuu Pinda kuwa dai la madaktari kutaka Waziri, Dk Mponda na Naibu wake, Dk Nkya ni jipya. Hii si kweli dai hilo lipo kwenye madai yote ya madaktari na yeye alilipata katika nyaraka zake zote alizokabidhiwa. Hata kauli yake aliyoitoa Februari 9, mwaka huu inaonyesha anatambua dai hilo na kuonyesha nia ya kulitatua.”
Alisema kinachofanyika sasa ni kushinikiza kutekelezwa kwa dai la kwanza kati ya matatu waliyokubaliana na wawakilishi kutoka serikalini ambalo ni hilo la kuwajibika au kuwajibishwa kwa viongozi hao.
Serikali imejiandaa
Akizungumzia mgomo huo jana, Pinda aliwaambia waandishi wa habari, Dar es Salaam kwamba Serikali imejipanga kukabiliana nao.Alisema juzi alipozungumza na waandishi ofisini kwake, tayari Serikali ilikuwa na mipango yake na ilichokuwa ikisubiri ni kuona matokeo ya mgomo huo kuanzia jana.
“Serikali imejipanga kukabiliana na mgomo huo. Pale jana (juzi) nilipozungumza na waandishi ofisini kwangu sikutaka kueleza mipango yote na kila kitu, lakini tulikuwa tunawasubiri tu wagome,” alisema Pinda.
Hata hivyo, alisema ni matumaini yake kwamba bado milango ya mazungumzo iko wazi na jambo hilo linaweza kupatiwa suluhu bila mgomo na kuwataka madaktari waendelee na kazi.
Alisisitiza kwamba ni makosa kitaaluma kwa daktari kugoma na kusababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia: “Ningewashauri madaktari waendelee na kazi.”
Dar es Salaam
Jana katika Hospitali ya Amana kulizuka vurugu baada ya wagonjwa na jamaa zao kuvamia mlango wa mapokezi huku wakitishia kuvunja vioo vya majengo ya hospitali hiyo baada ya kuelezwa kuwa hapakuwa na huduma.
Hali ilionekana kuwa mbaya hadi wanamgambo wa Manispaa ya Ilala walipofika. Hali ya hewa ilianza kuchafuka baada ya wahudumu wanaopokea wagonjwa na kuwaandikisha kabla ya kuonana na madaktari kuwaeleza wagonjwa kuwa huduma zimesitishwa.
Kauli hiyo iliwafanya baadhi ya wagonjwa wa nje kuondoka hospitalini hapo na baadhi yao wakiendelea kubishana na wahudumu hao, jambo ambalo lilileta tafrani.
“Sisi tuna makosa gani kwa nini tuambiwe huduma zimesitishwa. Sisi tunaonewa tumetangaziwa tangu jana (juzi) kwamba kuna mgomo lakini wanaoumia ni sisi,” alisema Justine Mushi.
Alipoulizwa kuhusu mgomo huo, Kaimu Mganga Mkuu wa Amana, Dk Christopher Mnzava alikanusha akidai huduma zinaendelea kama kawaida lakini alielezwa kwamba wahudumu wa mapokezi wamesema kwamba zimesitishwa.
Alifika mapokezi na kuonana na wagonjwa ambao walimweleza walivyoambiwa kuhusu kusitishwa kwa huduma na kutakiwa waondoke lakini Dk Mnzava alisema hizo ni kauli zilizotolewa baada ya kutokea vurugu na si kutokana na mgomo wa madaktari.
Katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, (Moi) utoaji wa huduma ulikuwa wa kusuasua na baadhi ya madaktari walisema walikuwa katika maandalizi ya kuanza mgomo.
Bugando
Madaktari waliopo katika mafunzo ya vitendo Bugando jana walitangaza kuanza mgomo kuungana na wenzao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kumaliza kikao cha kujadili mgomo huo, mmoja wa madaktari ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini alisema wameamua kurejea katika mgomo wao mpaka hapo madai yao yatakapotekelezwa na Serikali.
Jana hospitalini hapo kulikuwa na tangazo lililokuwa likieleza kuanza kwa mgomo huo ambalo hata hivyo, uongozi wa Bugando umesema ni la kihuni na haulitambui.
Ofisa Tawala wa hospitali hiyo, Joachim Wangabo alisema mgomo huo ni batili na kwamba watafuatilia kila hatua kujua ni nani wameingia katika mgomo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe.
“Naomba niseme Bugando hakuna mgomo, haya matangazo yanabandikwa tu na wahuni, ofisi yangu inafuatilia kujua waliogoma. Wakibainika tutawachukulia hatua,” alisema.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Omary Salehe alisema waliogoma ni wanafunzi 65 walioko katika mafunzo ya vitendo na kwamba licha ya mgomo wao, huduma zinaendelea kutolewa na madaktari bingwa licha kuwepo na hatihati ya kuzidiwa kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa.
Hali ya upatikanaji wa huduma hospitalini hapo jana ilikuwa imezorota kwa kiasi kikubwa na katika baadhi ya maeneo hapakuwa na huduma kabisa.
Mmoja wa wagonjwa, James Paul alisema alikuwa amepangiwa kufanyiwa upasuaji leo, hivyo alitakiwa afike jana kwa ajili ya kulazwa lakini aliambiwa aondoke na arejee baada ya wiki tatu. |
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa