Monday, February 13, 2012

TOKA GAZETI LA MAJIRA

Maombi yafichua ushirikina shuleni

*Wanafunzi wakiri kuchoma mabweni kishirikina
*Wafichua mpango wa kuua walimu wao watano
*Wasema uovu huo ni agizo la wazazi kulipa kisasi

Na Charles Mwakipesile, Mbeya

WANAFUNZI wawili wa kidato cha nne katika Sekondari Swila, mkoani Mbeya, (majina yamehifadhiwa), wamefukuzwa shule baada ya kukiri kuhusika na uchomaji mabweni mawili shuleni hapo kwa njia za kishirikina.

Akizungumza na Majira jana, Mkuu wa shule hiyo Bw. Omary Emanuel, alisema wanafunzi hao walikiri kufanya kosa hilo baada ya kutumwa na wazazi wao ili kulipa kisasa cha ndugu yao ambaye uongozi wa shule hiyo, ulimfukuza shule mwaka 2010.

Bw. Emanuel alisema mwanafunzi aliyefukuzwa, naye alikuwa akijihusisha na vitendo vya kishirikiana.

Aliongeza kuwa, mbali ya wanafunzi hao kukiri kosa hilo, waliueleza uongozi wa shule kuwa kazi nyingine waliyopewa na wazazi wao ni kuwaua walimu watano wa shule hiyo lakini wamekwama kufanya hivyo kutokana na nguvu za Mungu.

“Tunamshukuru Mungu ambaye siku zote amekuwa nasi, maombi ndiyo silaha yetu ndio maana hawa watoto wamejitokeza wenyewe na kukiri kosa la kuchoma mabweni na kutaka kuwaua walimu baada ya kudhibitiwa na askari wa Yesu na kujikuta hawana nguvu,” alisema.

Mwalimu mmoja (jina tunalo), ambaye alishiriki katika mahojiano na watoto hao, alisema wanafunzi hao walisema jukumu walilokuwa wamepewa ni kuchoma majengo ya shule nzima.

Mkurugenzi wa shule hizo Bi. Happy Nyemba, alisema bweni la kwanza lilichomwa Februari 5 mwaka huu na kuteketeza vifaa vya wanafunzi 40 wa kike lakini hakuna aliyekufa.

Alisema wakati uongozi wa shule ukitafakari juu ya tukio hilo, tukio jingine kama hilo lilitokea Februari 8 mwaka huu, ambapo kutokana na hali hiyo, waliamua kufanya maombi ambayo Mungu alitoa majibu ya haraka kwa kuwafichua wanafunzi hao.

“Hivi sasa vyombo vya dola vinaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hili na sisi tumeamua kupitia mifumo ya umeme, naomba wazazi waendelee kutuamini kwani tutahakikisha nguvu zote za giza zinashindwa kwa kufanya maombi,” alisema.

Habari za uhakika zinasema kuwa, Jeshi la Polisi mkoani humo lilikuwa likiwahoji watumishi wanne wa shule hiyo kuhusiana na matukio hayo lakini baada ya wanafunzi hao kujitokeza mbele ya walimu na viongozi wa shule na kukiri kosa, uongozi wa shule uliagiza watumishi hao waachiwe mara moja.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Advocate Nyombi na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro, walipata fursa ya kutembelea shule hiyo, kutoa pole na kuutaka uongozi wa shule hiyo, uendelee na mikakati yao ya kutoa elimu bora.

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa