Tuesday, January 17, 2012

Mfumuko wa bei sasa wafikia 19.8



MFUMUKO wa bei nchini umezidi kuongezeka na sasa umefikia asilimia 19.8 kutoka asilimia 19.2 Novemba, mwaka jana.

Taarifa ya farahisi za bei za taifa ya Desemba, mwaka jana iliyotolewa jana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imeonyesha  kwa ujumla bei zimeongezeka hadi asilimia 121.79 kufikia Desemba mwaka jana kutoka asilimia 101.70 Desemba mwaka juzi.

Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula. Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa bei ni mchele, asilimia 10.6 na mikate asilimia 2.4.

Taarifa hiyo imeeleza pia kuwa bei ya vitafunwa imeongezeka kwa asilimia 1.9, nyama asilimia 4.0, samaki asilimia 2.4, maziwa asilimia 4.0, mafuta ya kupikia asilimia 3.2, limao asilimia 6.2, karanga asilimia 7.2, mbogamboga asilimia 5.5 na asali asilimia 3.1

Taarifa hiyo imeeleza kuwa vyakula na vinywaji baridi vimeongezeka bei hadi asilimia 27.1 kwa mwaka ulioishia Septemba, 2011 kutoka asilimia 26.1 kwa mwaka ulioishia Novemba, 2011.

“Badiliko la farahisi ya bei za bidhaa za vyakula nyumbani na katika migahawa limeongezeka hadi asilimia 25.6 kwa mwaka ulioishia Desemba mwaka jana ikilinganishwa na asilimia 24.7 kwa mwaka ulioishia Novemba, 2011,” imeeleza taarifa hiyo.

Ofisi ya Takwimu imeeleza katika taarifa yake hiyo kuwa kasi ya ongezeko kwa bidhaa zisizo za vyakula imefikia asilimia 12.7 kwa mwaka ulioishia Desemba, 2011 kutoka asilimia 12.6 kwa mwaka ulioishia Novemba mwaka jana.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa mwaka ulioishia Desemba, 2011 ambao umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 8.7 kutoka asilimia 8.8 kwa mwaka ulioishia Novemba, 2011.

Hata hivyo, mfumuko wa bei wa nishati uliongezeka hadi asilimia 41.0 kwa mwaka ulioishia Desemba, 2011 kutoka asilimia 39.2 Novemba, 2011.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula umekuwa na mwelekeo unaofanana na kuongezeka kwa kila mwezi kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana.

“Wastani wa mfumuko wa bei ya taifa umeongezeka kutoka asilimia 5.5 mwaka 2010 hadi asilimia 12.7 mwaka jana hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.2 wakati wastani wa mfumuko kila mwezi ulikuwa asilimia 1.4 kutoka Januari hadi Desemba mwaka jana,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 2.0 na bei za Desemba mwaka jana ziliongezeka kwa asilimia 2.0.

Kwa upande wa thamani ya Shilingi (kipimo cha Sh100), taarifa hiyo ilisema imepungua kutoka Septemba mwaka 2010 hadi kufikia Sh82.11 Desemba mwaka jana.

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa