Wednesday, January 25, 2012

kuanza kurejeshwa kwa wanafunzi MUHAS

Wanafunzi 78 waliofukuzwa Muhas warejeshwa

Nora Damian wa Mwananchi
UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), umewarejesha wanafunzi 78 waliokuwa wamesimamisha masomo kwa tuhuma za kuwa vinara wa vurugu. Wanafunzi hao walisimamishwa masomo mwishoni mwa mwaka jana baada ya vurugu zilizotokea chuoni hapo Desemba 8, wakati wa sherehe ya utafiti na Desemba 10 wakati wa mahafali. Ofisa Uhusiano wa Muhas, Hellen Mtui, alisema wanafunzi hao wamerejeshwa baada ya kusikiliza utetezi wao.

Alisema kinachofanyika sasa ni kusikiliza utetezi wa mwanafunzi mmoja mmoja na kwamba, wale watakaokutwa na makosa makubwa watapelekwa kwenye kamati ya nidhamu kwa hatua zaidi. “Wengine bado wanaendelea kusikilizwa utetezi wao na wengine wameelekezwa kwande kwenye kamati ya nidhamu,” alisema Mtui.

Alisema wanafunzi waliorejeshwa ni wale waliokutwa na makosa madogo na kwamba, wale waliokutwa na makosa makubwa wamepelekwa kamati ya nidhamu. Kuhusu suala la kurejeshwa kwa Serikali ya Wanafunzi (Muhasso) ambayo ndiyo chanzo cha vurugu hizo, Mtui alisema suala hilo halijajadiliwa na kusisitiza kuwa kinachoshughulikiwa hivi sasa ni kusikiliza utetezi wao.


Chanzo cha vurugu hizo ni madai ya wanafunzi hao kutaka kurejeshewa Serikali ya wanafunzi iliyovunjwa na baraza la chuo hicho tangu Juni mwaka jana, kutokana na kukaidi maagizo ya Serikali yaliyotaka vyuo vikuu vyote kubadili katiba zao. Mwaka 2009, Serikali ilitoa waraka kwa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu vyote nchini kubadilisha katiba zao, lakini serikali nyingi ikiwamo Muhasso hawakukubaliana na uamuzi huo.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao walikwenda Mahakama Kuu na kufungua kesi wakimshtaki Makamu Mkuu wa chuo hicho, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Manasheria Mkuu wa Serikali (AG). Uongozi wa chuo hicho uliwataka wanafunzi hao kuondoa kesi mahakamani ili kukaa kujadiliana jinsi ya kurejesha Muhasso.

Hata hivyo, baada ya kukaa kwa wiki tatu nyumbani, mwanzoni mwa mwaka huu wanafunzi waliosimamishwa waliomba radhi uongozi wa chuo, Serikali na wananchi kutokana na usumbufu uliojitokeza. Pia, wanafunzi hao walitangaza uamuzi wa kwenda kuondoa madai yao Mahakama Kuu yaliyolenga kurudishiwa serikali yao, ili kuongeza uwanja wa majadiliano baina yao na uongozi wa chuo.

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa