Wednesday, November 2, 2011

hatimaye baada ya kipindi kirefu !!!!

Hatimaye ndege ya ATCL yaonekana tena angani


Abiria wa wakipanda ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), kuelekea mkoani Kigoma baada ya shirika hilo kuzindua tena huduma zake jana, ambazo zilikuwa zimesimama kwa miezi minane iliyopita. Picha na Mpigapicha wetu
Mwandishi wetu
HATIMAYE ndege ya kwanza ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), imeanza kurusha kuruka kwenye anga ya Tanzania baada ya kusimamisha shughuli zake kwa miezi minane iliyopita.Uzinduzi huo ulifanyika jana baada ya ndege yake kuruka kwenda Kigoma na Tabora, ambako inaonyesha kupokelewa zaidi kutokana na kupata abiria wa kutosha.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa ATCL, Paul Chizi, alisema mapokezi waliyopata kutoka kwa abiria wa Kigoma na Tabora, imewapa imani kuwa mipango waliyojiwekea itatekelezeka.

“Kwa miezi minane tulikuwa nje ya soko, lakini leo (jana) tumepata idadi ya kutosha ya abiria tumelazimika kushusha wafanyakazi wetu wanne Tabora. Tunatarajia mwishoni mwa Desemba tutakuwa na ndege nyingine na tumejipanga huduma,” alisema Chizi.

Pia, Chizi alisema wanatarajia kuleta ndege nyingine aina ya CRJ kwa safari za nje na kwamba, hivi sasa matengenezo ya ndege yatakuwa yakifanyika nchini.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali mstaafu Issa Machibya, alisema kurejea kwa safari za ndege ni ukombozi na kuongeza kuwa, baada ya mwaka mmoja uwanja wa mkoa huo utakuwa ukiruhusu ndege aina ya Boing kutua hata usiku. Matengenezo ya uwanja huo yanaanza Desemba.
Kanali Machibya akiwa ameongozana na magavana (wakuu) wa mikoa minne ya Burundi inayopakana na Tanzania, alisema uzinduzi huo utakuza uchumi wa Kigoma na kuchochea zaidi uwekezaji.

Gavana wa Mkoa wa Makamba, nchini Burundi, Mbayubage Vincent, alisema uzinduzi huo siyo wa Kigoma, bali Mkoa wa Makamba na kwamba, wamekuwa wakipata usumbufu pindi wanapokwenda Dubai kufuata biashara.

“Sasa nasema tuna ndege ya kwenda Makamba, sisemi Kigoma. Huu ni ukombozi baada ya usumbufu ambao tumekuwa tukipata,” alisema Vincent.
Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Bunge ya Sheria, George Simbachawene, alisema kuzinduliwa kwa huduma hiyo kumewapa imani wabunge kwa sababu jinsi walivyosimamia kikamilifu shirika kufufuliwa na kupewa fedha, walikuwa wanahisi hakuna kitakachofanyika.

Simbachawene alisema licha ya wananchi kuingia kwenye mfumo wa ubepari, hawajasahau ujamaa hivyo wanapenda na kujivunia kitu chao. Kamati hiyo ipo mkoani Tabora kikazi.

“Nauli zenu zinaendana na hali halisi ya kipato cha Mtanzania. Nina uhakika washindani wenu watapata kazi kubwa, nasikia wengine wameshusha kuanzia leo. Ushauri wangu muwe na njia mtakazomudu maana mkianguka washindani wenu watashangilia na hilo ndilo wanaloomba.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Rajab Samatta, alisema wananchi wamekuwa wakipata shida kufuata huduma ya ndege Mkoa wa Mwanza.
“Mkoa umekuwa kama kisiwa, lakini urejeshaji wa huduma za ndege na hatua zinazochukuliwa na Serikali za kufungua barabara, tunaona sasa tunaelekea kwenye ukombozi kamili,” alisema Samatta.

1 comment:

Anonymous said...

hongera zao kwa kurudisha tena ndege mzigoni ila wahakikishe ziko poa zisije zikang'oka tena tairi?

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa