Friday, October 7, 2011

TBC chupuchupu kuungua moto




Askari wa kikosi cha zimamoto wa Kampuni ya Knight Support akiwa mbele ya jenereta lililoteketezwa kwa moto na kuunguza jengo la jirani katika ofisi za kampuni ya Star Times eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam jana. Picha na Zacharia Osanga
Zacharia Osanga
MOTO uliosababishwa na hitilafu ya umeme kwenye transfoma iliyopo ndani ya kampuni ya ving'amuzi ya StarTimes yenye ubia na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), jana ulizusha tafrani eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam  kabla ya vikosi vya zimamoto kuuzima moto huo.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, aliyefika eneo hilo la tukio kwa ajili ya kusimamia zoezi hilo, alisema moto huo ulianza saa 7:10 mchana.
Alisema kwamba chanzo cha awali cha moto huo ni kulipuka kwa transfoma hiyo iliyo ndani ya eneo la kampuni hiyo ambayo baadaye iliteketeza jenereta na ofisi zilizokuwa jirani.
Hata hivyo, Kenyela alisema jeshi lake linaendelea na uchunguzi na hakuna madhara yaliyotokea kwa binadamu kutokana na kuwasili mapema kwa vikosi vya zimamoto.

StarTimes
Akizungumzia mkasa huo, Ofisa Mkuu Mtendaji wa Star Times, William Lan alisema mafundi wa Tanesco walifunga transfoma mpya juzi  ambayo ililipuka siku moja baadaye.Lan alisema baada ya kulipuka kwa transfoma hiyo ya awali, Tanesco walirudi na kufunga nyingine iliyoanza kufanya kazi jana  saa 4:OO  asubuhi.
Hata hivyo, alisema transfoma hiyo nyingine nayo ilidumu kwa muda wa saa 3 na ndipo ilipolipuka tena jana.
‘’Inaonekana Transfoma ya zamani haikuwa na matatizo baada ya haya mabadiliko ya kuweka mpya ndio milipuko ikaanza,’’ alisema Lan.
Alisema tukio hilo litawaathiri wateja wao ambao kwa hapa nchini wapo 150,000  kutokana na chaneli 20 zinazorusha matangazo na kwa bara zima la Afrika wako 800,000.Lan alisema tayari wameunda timu ya uchunguzi ili wajue ni kwa kiasi gani vifaa vyao vimeathirika, baada ya hapo ndipo watakapojua hatua za kuchukua.
Tanesco wanena
Kwa upande wake, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kinondoni Kaskazini, Christopher Masasi alisema ni mapema mno kuzungumzia kwa kina sakata hilo, kwani bado inawabidi kufanya uchunguzi zaidi.Hata hivyo, Masasi alikiri kuwa walifanya mabadiliko ya transfoma juzi Jumanne, ambayo ililipuka na kuweka nyingine ambayo nayo ililipuka jana.

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa