Patricia Kimelemeta (Gazeti Mwananchi)
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limewafikisha kwenye Kamandi ya Wanamaji Dar es Salaam (Navy) maharamia saba, waliotaka kuteka meli ya Sam S Allgood inayofanya utafiti wa mafuta Kaskazini Mashariki mwa Kisiwa cha Mafia.Maharamia hao walikamatwa Oktoba 3, mwaka huu saa 2:00 usiku umbali wa kilomita 40 mwa Kisiwa cha Mafia, Mkoa wa Pwani, wakiwa na silaha wakitaka kuteka meli hiyo.
Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Kapambala Mgawe, alisema kutokana na hali hiyo, maharamia hao watahojiwa ili kubaini chanzo cha utekaji huo, ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kanali Mgawe alisema hadi sasa hawajafahamu nchi wanayotoka maharamia hao, licha ya kuonekana kuwa na asili ya Kisomalia, jambo ambalo limewafanya wawe karibu nao ili waweze kuwahoji kwa undani zaidi.
“Hivi sasa (jana mchana) wanatarajiwa kuwasili Navy wakati wowote kwa ajili ya mahojiano zaidi, lengo letu ni kutaka undani wao, nchi wanayotoka na sababu za kutaka kuteka meli hiyo, jambo ambalo tunaamini wanaweza kutupa ushirikiano,” alisema Kanali Mgawe.
Aliongeza maharamia hao wana asili ya Somalia, lakini wanashindwa kuwabaini nchi wanakotoka kutokana na kusambaa karibu nchi zote za Afrika Mashariki na Kati.
Kanali Mgawe alisema kutokana na hali hiyo wataendelea kufanya mahojiano kwa ukaribu zaidi, ingawa wanaonekana wajeuri na kwamba wanaweza kujitoa mhanga wakati wowote, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya askari waliowakamata kwenye zoezi hilo.
“Kila nchi ina Wasomali, iwe Tanzania, Kenya na Uganda, hivyo basi kubaini kama ni Wasomali wa wapi kwa kipindi kifupi siyo rahisi, wanaonekana wana roho ngumu kweli. Hivyo wanaweza kujitoa hata mhanga kutokana na hali hiyo tunapaswa kuwa makini ili tusihatarishe maisha ya askari wetu,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa sheria za kimataifa, wameshindwa kuwashughulikia zaidi kwa sababu tayari waliwahi kusalimisha silaha zao, jambo ambalo lilifanikisha zoezi zima la kuwakamata.
Msemaji huyo alisema iwapo watathibitisha kuwa ni maharamia, watawakabidhi polisi kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria, suala ambalo wanaamini litapunguza matukio ya utekaji nchini.Alisema wanajeshi hao walifanikiwa kuwakamata maharamia hao baada ya nahodha wa meli ya Sam S Allgood kuonyesha ishara ya kupata matatizo baada ya kuona wamevamiliwa. |
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa