Send to a friend |
Send to a friend |
0digg Fidelis Butahe BAADA ya Bunge kuikabidhi Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, jukumu la kuchunguza ufisadi wa zaidi ya Sh205.9 bilioni unaodaiwa kufanywa kupitia Kampuni ya Meremeta, wasomi na wanasiasa nchini wamepinga uamuzi huo wakidai kuwa ukweli utapindishwa. Spika wa Bunge, Anne Makinda aliamua kuwa Kamati hiyo ya Bunge ifanye uchunguzi huo kwa kuwa ndiyo inayohusika na suala hilo la Meremeta. Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Jumapili jana, wasomi na wanasiasa hao walidai kwamba, tatizo sio suala hilo kupelekwa katika kamati hiyo, bali ni mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye walisema hawaamini kama atafanya kazi hiyo vizuri. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sengondo Mvungi alisema, “Inakuwaje mtu anatuhumiwa kwa mambo mbalimbali halafu kamati yake inapewa jukumu la kuchunguza suala hilo zito?” Mvungi ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema kuwa, ni vyema kiongozi akiwa na tuhuma za kifisadi achunguzwe kwanza kabla ya kupewa majukumu. “Hapa ndio utaona jinsi Serikali ya Tanzania inavyougua ugonjwa wa saratani ni lazima ife…, jambo hili katika taaluma ya sheria na katiba tunaliita kuwa ni ‘ishara ya dola inayokufa’,” alisema Mvungi. Aliongeza: “Siku hizi si ajabu kuona jaji anahongwa na Takukuru… Ni wazi kuwa Serikali inayumba”. Alisisitiza kwamba, ndani ya kamati hiyo atakayejiona hawezi kufanya kazi hiyo kwa kuwa ana maslahi binafsi na Meremeta aachie ngazi mapema ili kuondoa maswali kutoka kwa wananchi, kinyume chake uchunguzi wa kamati hiyo hautakuwa na faida yoyote. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema, “Jambo linaloibuliwa na kundi jingine na kuhitaji ufumbuzi si vyema likasimamiwa na kundi linalolalamikiwa”. Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema kwa kiasi kikubwa sakata la Meremeta liliibuliwa na wabunge wa upinzani, lakini anashangaa kuona suala hilo linapi pelekwa katika kundi ambalo linaweza kuwa lilihusika. “Simhukumu Lowassa kuwa ni fisadi…, lakini wakati Serikali inaingia mkataba na kampuni hii yeye alikuwa katika Baraza la Mawaziri, sasa suala hili kurejeshwa tena kwake ni sawa?” alihoji Mbowe. Mbowe alisema kuwa huu ni wakati wa Bunge kutambua kuwa si lazima kila Kamati iongozwe na wabunge wa CCM na kusisitiza kuwa ni vyema ikaundwa Kamati itakayoongozwa na upinzani ili kuchunguza Meremeta. Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema si lazima ufisadi wa Meremeta ukachunguzwa na Kamati ya Bunge. “Takukuru si wapo wanaweza kufanya kazi hii…, hili ni jambo nyeti ambalo linatakiwa kuchunguzwa na watu wenye taaluma kama Takukuru, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Jeshi la Polisi,” alisema Mbatia. Mbatia alidai kuwa ndani ya CCM hakuna wa kumfunga mwenzake kengele. Alidai kuwa chama hicho kimekithiri kwa ufisadi na kwamba walio salama ni wachache. “Hakika uamuzi huu utazidi kuwachanganya Watanzania, inakuwaje mtu anatuhumiwa kwa mambo fulani halafu anachaguliwa kuwa Mwenyekiti Kamati ya Bunge, halafu kamati yake inapewa jukumu hili?” Alihoji Mbatia Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, alidai kuwa kamati hiyo haiwezi kuja na majibu ya kuwaridhisha Watanzania. “Ni usanii mtupu, hata vyombo vingine vya Serikali haviwezi kulichunguza jambo hili kwa kuwa kwa muda mrefu vimekuwa vibaraka wa mafisadi, labda vivunjwe na kuundwa upya,” alidai Mtikila Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana, alisema ingawa uamuzi huo wa Bunge utazua maswali mengi kwa wananchi, sheria za Tanzania zinaeleza wazi kuwa mtuhumiwa sio mkosaji. “Mbona Lowassa anakwenda kanisani na kuchangisha mamilioni ya fedha watu hawasemi lolote?” Alihoji Bana na kuongeza: “Watanzania wasimhukumu mtu kwa hisia, sidhani kama hata hiyo kamati yake ina watu wasafi…, Lowassa kisheria na kisiasa yuko safi ila kihisia si safi, tunatakiwa kufanyia kazi hali halisi si hisia,”. Hata hivyo, alisema pamoja na Bunge kupeleka suala hilo kwa kamati inayoongozwa na Lowassa, Serikali pia inaweza kuunda tume yake ya kuchunguza ufisadi huo. Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Bashiru Ally alisema kuwa unyeti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama unaweza kufanya majibu ya uchunguzi huo yakawa wazi au kuwa siri. “Wanaweza kusema kuna mambo hawawezi kuyasema kwa ajili ya usalama wa nchi, ila binafsi nilidhani suala hili lingepelekwa Kamati ya Nishati na Madini au ile ya Mashirika ya Umma, sijui Spika wa Bunge katumia vigezo gani kulipeleka suala hili katika kamati hii,” alihoji Bashiru. |
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa