Wednesday, July 13, 2011

Wanafunzi wanywa sumu kupinga kuzuiwa ngono

Wanafunzi wanywa sumu kupinga kuzuiwa ngono

Na Cresensia Kapinga, Songea

WANAFUNZI wawili wa Shule ya Sekondari Zimanimoto, mkoani Ruvuma wamenusurika kufa baada ya kunywa sumu ya panya na vidonge saba vya panadol, kwa
kile kinachodaiwa walionywa na wazazi wao kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya ngono.


Inadaiwa wazazi walitoa onyo kwa wanafunzi hao, baada ya kugundulika wana uhusiano wa kimapenzi, huku mmoja wao akifukuzwa nyumbani na mama yake mzazi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Bw. Michael Kamuhanda alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5 asubuhi eneo la Msamala, ambapo binti mhusika alifukuzwa nyumbani na mama yake mzazi baada ya kushindwa kuelewana mara kwa mara.

Alisema hali hiyo ilitokana na mama huyo kutoridhishwa na tabia ya mwanawe na siku ya tukio alishikwa na hasira baada ya kumuonya mara kwa mara kuhusu tabia ya kujihusisha na vitendo viovu, lakini ilishindikana, hivyo kuamua kumfukuza nyumbani.

Alisema kuwa baada ya binti huyo kufukuzwa alienda kwa mpenzi wake
ambaye ni mwanafunzi mwenzake.

Alisema wakiwa Msamala, binti huyo alikunywa sumu ya panya kwa lengo la kujiua, na mpenzi wake kuona hivyo naye aliamua kunywa sumu hiyo na vidonge saba aina ya panadol kwa lengo la kutaka wafe wote.

Hata hivyo, alisema baada ya muda mfupi wasamalia wema walifanikiwa kuwaona na kuwakimbiza katika Hospitali ya Mkoa kwa ajili ya matibabu.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Songea (HOMSO) Dkt. Gideon  Njowoka alikiri kupokea wagonjwa hao na kuongeza kuwa hali za wanafunzi hao zinaendelea vizuri.

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa