Saturday, May 14, 2011

Mgonjwa ajinyonga chooni Muhimbili

BAADHI ya wagonjwa na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, jana walishikwa na simanzi baada ya kukuta mwili wa mwanamke Suzan Chiganga (51), ukining'inia bafuni katika wodi ya Sewa Haji ambapo marehemu alikuwa amelazwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, amesema tukio hilo limetokea Mei 13, mwaka huu,saa 6.00 za usiku wodi namba 20 Sewa Haji, marehemu aliamua kujinyonga kwa upande wa khanga.

Amesema kuwa, marehemu alitumia bomba la maji kujitundika na khanga hadi kufa na uchunguzi wa awali umebaini kuwa, alikuwa amelazwa hospitalini hapo tangu Aprili 24, mwaka huu akitokea Hospitali ya Ocean Road, ambapo alikuwa akisumbuliwa na uvimbe kwenye jicho la kulia.

Kamanda amesema sababu za kifo hazijafahamika kwa kuwa marehemu hakuacha ujumbe wowote na maiti imehifadhiwa hospitalini hapo, huku jeshi la polisi likiendelea na upelelezi.

Katika tukio lingine, Jeshi hilo limewakamata wanawake 19 na mwanaume mmoja katika eneo la Buguruni kwa kosa la kuuza miili yao.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile amesema tukio hilo limetokea Mei 12, mwaka huu, eneo la Buguruni Madenge na Chama, askari wakiwa katika msako walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Kamanda amewataja watuhumiwa hao ni Jamila Swed (20),Eva Lucas (18), Rehema Ubrahim (22), Yasinta Nyenza (24),Rehema Issah (18), Selina Hamis (27), Tatu Urembo (15) na Zaina Hassan (20) na wenzao upepelezi unaendelea.

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa