Wednesday, March 23, 2011

MAALIM SEIF ATOKA HOSPITALI INDIA BAADA YA UPASUAJI

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ametoka hospitali baada ya kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Apolo nchini India na anatarajiwa kuwasili Zanzibar keshokutwa.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar jana ilisema Maalim Seif atawasili Zanzibar Ijumaa saa 10:30 alasiri na kufanya mkutano na waandishi wa habari.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kabla ya Maalim Seif kulazwa na kufanyiwa upasuaji wa goti, alitembelea nchi za Uholanzi, Umoja wa Falme za Kiarabu na Oman.

Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE, Katibu Msaidizi wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Issa Khari, alisema Maalim Seif aliruhusiwa kutoka hospitalini Machi 18, mwaka huu na kuendelea na ziara yake Dubai.

"Hali ya kiafya ya Maalim Seif ni imara na amesema siku atakaporeja Zanzibar kama ni siku ya kazi, ataendelea na kazi zake kama kawaida," alisema Katibu huyo.

Maalim Seif aliondoka Zanzibar Februari 7, mwaka huu akiwa na ujumbe wa watu 11 kwa ziara ya kikazi, ikiwa ni ya kwanza nje ya nchi tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Maalim Seif alikuwa arejee nchini Februari 23, mwaka huu lakini baada ya uchunguzi huo alishauriwa kufanyiwa upasuaji wa goti na kuendelea na mazoezi katika hospitali hiyo.

No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa