Madai wastaafu EAC yatupwa
MADAI mapya yaliyowasilishwa na wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kulipwa sh trilioni mbili badala ya sh bilioni 117, yamegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kukataa madai hayo.
Wazee hao kwa mujibu wa hukumu ya maridhiano ya Mahakama Kuu ya Septemba 12, 2005 iliyotolewa na Jaji Catherine Urio kwenye kesi ya msingi namba 93 ya mwaka 2003, wanatakiwa kulipwa sh bilioni 117.
Jaji John Utamwa jana alitupilia mbali madai ya kulipwa sh trilioni mbili kutokana na kutoona sababu za msingi ya kulipwa kiasi hicho, kwani mahakama ilikwishatoa uamuzi wa kulipa sh bilioni 117.
Katika maelezo yake, Jaji Utamwa alisema Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam haiko tayari kukubali maombi ya wastaafu hao ya kutoa hati za malipo ya kiasi hicho kipya wanachodai kwani ni kinyume cha makubaliano.
Alisema upande wa mahakama unakubali madai ya awali ya wazee hao ya sh bilioni 117 na kwamba malipo hayo ni halali.
Hata hivyo, mara baada ya uamuzi huo, kundi la wazee hao lililokuwa nje ya mahakama lilipinga uamuzi huo huku baadhi yao wakitaka wamfuate Jaji Mkuu Agustino Ramadhani kueleza kutoridhika kwao na uamuzi huo.
Hata hivyo uamuzi wa kutaka kwenda kumuona Jaji Mkuu uligonga mwamba baada ya gari la askari wa usalama kuwataka waondoke kwenye viwanja vya mahakama.
Wastaafu hao walifungua kesi wakitaka walipwe sh bilioni 117, lakini baada ya kulipwa walifungua tena kesi kudai malipo mengine, kitu ambacho serikali ilipinga.
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa