Na mwanablog wetu |
Monday, 23 August 2010 09:20 | ||||
KATIKA kile kinachoonekana ni kutaka kumaliza mvutano wa muda mrefu kati ya serikali na wafanyakazi, Rais Jakaya Kikwete, amesema hajawahi kudharau wafanyakazi kuhusu madai yao ya mishahara. Rais Kikwete aliyasema hayo ikiwa bado kuna mvutano kati ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) na serikali ambayo Mei mwaka huu, mkuu huyo wa nchi aliwaonya wanaopanga mgomo akisisitiza serikali isingewavumilia. Akifafanua sakata hilo ambalo aliligusia juzi kwenye viwanja vya Jangawni kabla ya kukatisha hotuba kufuatia kukumbwa na ugonjwa wa kisukari, Rais ambaye aliambatana na viongozi waandamizi akiwamo makamu mwenyekiti bara Pius Msekwa pamoja na mgombea mwenza Dk Mohamed Ghalib Bilali, alisema anathamini hata kura moja. Rais ambaye tofauti na hofu iliyokuwa imetanda kwamba tukio la juzi lingemfanya ashindwe kuendelea na kampeni, katika hotuba yake takriban dakika 40 alionyeshwa kushangazwa na taarifa za yeye kukataa kura za wafanyakazi. Kwa mujibu wa Rais, mvutano ambao umekuwapo ni kuhusu kiasi gani cha mishahara ambacho serikali ingepaswa kulipa kima cha chini cha wafanyakazi na kuongeza kwamba, "Hapa ndipo penye mgogoro." Akisisitiza hilo, Rais alisema msimamo wa serikali siku zote uliangalia uwezo wake, ndiyo maana haikutaka kudanganya wafanyakazi kwamba ingeweza kuwalipa kiasi hicho walichotaka . Alifafanua kwamba, Tucta wamekuwa wakitaka mshahara wa kima cha chini kufikia 315,000, lakini msimamo wa serikali ulikuwa ni chini ya hapo (Sh 105,000), kitu ambacho kiliibua mvutano. "Sasa wenzetu wakafanya maandamano pale Dar es Salaam wakasema tutakayempa kura zetu ni yule atakayeweza kutupatia kiasi hicho. Haya yalikwemo katika mabango yao, sasa mimi nikasema kama ni hivyo kura nimezikosa," alifafanua na kuongeza:, "Ndiyo, kwasababu sisi tumesema hatuna uwezo huo wa kulipa kiasi wanachotaka wenzetu Tucta. Tumeamua kuwa wa kweli, kwanini tuseme uongo? Sasa leo hii mimi ndiye mbaya. Mimi nasema, tunathamini sana maslahi ya wafanyakazi na nathamini hata kura moja." Hata hivyo, Rais Kikwete aliweka bayana kwamba, chini ya uongozi wake ameweza kuongeza mishahara ya wafanyakazi kila ilipowezekana na kusisitiza kwamba, wapo wafanyakazi watakaofanya uchambuzi na kubaini chuya na mchele ni upi. "Miongoni mwa wafanyakazi wapo watakaofanya tathimini ya chuya ni ipi na mchele ni upi, kisha wataangalia na hatimaye wataamua kuipigia CCM kura, sisi tunathamini sana wafanyakazi kwani bila wao mambo hayawezi kwenda vizuri," alisisitiza. Alisisitiza kwamba, madai hayo ya wafanyakazi kama yangetimizwa serikali ingeweza kuathirika katika utekelezaji wa huduma nyingine muhimu zikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, huduma za afya na nyingine za kijamii. Kuhusu utekelezaji wa ilani ya mwaka 2005/2010, Rais alisema ahadi mbalimbali katika mkoa huo zikiwemo kupatia vivuko maeneo muhimu yaliyokuwa na matatizo ya usafiri yameweza kupatiwa ufumbuzi. Mkuu huyo wa nchi anayemaliza muda wake, alisema ahadi kubwa ilikuwa ni kuwapatia kivuko cha Kisorya, lakini vipo vingine vimeshughulikiwa na kuongeza kwamba, lengo ni kumaliza kabisa tatizo hilo. Kurugenzi ya Ufundi na Umeme chini ya Wizara ya Miundombinu katika miaka ya karibuni imetajwa katika ripoti mbalimbali za kiserikali kwamba, imeweza kwa sehemu kubwa kumaliza tatizo la usafiri katika maeneo yanayohitaji vivuko nchini ikiwemo mikoa ya kanda ya ziwa, mashariki na kaskazini. |
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa