Wednesday, April 14, 2010

Balozi atoa changamoto kwa wanahabari

BALOZI wa Sweden nchini, Staffano Herrstrom, ametoa changamoto kwa wamiliki wa vyombo vya habari na waandishi nchini kuandika habari za kiuchunguzi pamoja na za kijamii, ili kuongeza tija ya sekta ya hiyo.

Balozi Herrstrom alitoa changamoto hiyo jana jijini Dar es Salaam alipomtembelea Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, na kuzungumza naye kuhusu ya sekta ya habari nchini.

"Mbali na changamoto mnazokabiliwa nazo wamiliki wa vyambo vya habari, bado mna nafasi nzuri ya kuendeleza kupanua wigo wa taaluma hii kuendelea kukua zaidi hapa nchini," alisema balozi huyo.

Alisema waandishi wa Tanzania wanahitaji kupatiwa uwezeshwaji ili kuweza kufikia jamii kubwa hasa zilizo vijijini ikiwemo na suala la kutafuta habari za kiuchunguzi ndani ya nchi bila kuvunja Katiba.

Kwa upande wake, Mengi alimhakikishia balozi huyo kuwa changamoto hizo zinafanyiwa kazi huku kwa upande wake kama mmiliki wa makampuni ya habari ametekeleza mambo mbalimbali ya msingi ikiwemo kutaka Baraza la Habari kuengezewa meno ili kupunguza migongano ya kesi za habari nchini.

"Fahari ya wamiliki wa vyombo vya habari ni kuona vyombo vyao vikiendelea na wala si kufa, hivyo kila mmiliki anatumia mbinu za kiushindani ili kukabiliana na soko," alisema Mengi.

Aidha, Mengi alishauri katika kuelekea uchaguzi mkuu vyombo vya habari vinapaswa kuhakikisha vinaandika ukweli bila kuwachafua watu kwa kutumiwa.



No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa